Huwa naona kama naota ndoto nzito, ambazo hazina mwisho kila ninaposikia vioja vya watendaji wa Serikali yetu katika kulitendea haki Taifa hili.

Napata taabu kukubaliana kama hawa ndiyo viongozi tuliowapigia kura ama walichaguliwa na Mungu, kuja kutuhukumu tungali hai kama vile mwisho wa dunia umefika.

Nimewahi kulalamika katika waraka wangu huu juu ya mambo mengi ambayo naona hayaendi sawa, nimelalamika juu ya uadilifu, utendaji mbovu, uwajibikaji, umakini, wizi, utapeli na uongo, lakini ni kama vile nampigia mbuzi gitaa. Hakuna kinachoendelea na kuleta mabadiliko.

 

Hivi sasa mathalani Bunge linaendelea makao makuu ya nchi yetu. Wapo watakaopinga juu ya makao makuu lakini ndivyo tulivyokubaliana enzi zile za uamuzi wa wote na bado naamini katika hilo kwamba ni makao makuu ya nchi yetu. Hili ni moja ya mambo ambayo najaribu kuhoji juu ya uwajibikaji wa viongozi wetu katika hili na matokeo yake.

Bunge hili lina vioja vyake ambapo baadhi wanadiriki kutohudhuria kikao kwa sababu zao, zaweza kuwa za msingi ama la, lakini suala la kujiuliza ni juu ya uwajibikaji wa viongozi hawa waliochaguliwa na sisi wapiga kura wakatuwakilishe bungeni.

Nimesema wanaweza kuwa na sababu ya msingi ya kutoka bungeni lakini sina hakika kama sauti hiyo inaweza kusikika na kufanyiwa kazi kwa ukimya huo wa kutoka. Waswahili wana usemi kwamba unaweza ukamjibu mtu kwa kubaki kimya japokuwa katika maadili kukaa kimya ni utovu wa nidhamu.

Mimi naamini kuwa sauti ni njia ya kupitisha mawazo yawe yanasikika ama hawataki kusikia. Napenda mawazo ya kupingana kwa hoja, lakini yawe ya msingi si kila jambo la kupinga ili kuonesha ubabe wa hoja. Nakumbuka kuwa Julius alitumia sauti hiyo hiyo UN hadi tukapata Uhuru, na inawezekana walikuwapo ambao waliamua kutoka wakati alipopewa kipaza sauti.

Nashindwa kukubaliana na utendaji wetu wa kazi, na hasa kwa viongozi wetu ambao wengi wao badala ya kupingana na Serikali yao sasa wanataka kupingana na wananchi ambao tuliwachagua. Naona kama wanatumia hoja ya nguvu na si nguvu ya  hoja.

Nafikiria tulikotoka na wapi tupo na hatima ya safari yetu, nayaona mageuzi ya mawazo ya nchi za Kaskazini yanataka kuuteka umma wa Watanzania kwa nguvu ya viongozi wachache walioko madarakani na wawakilishi wetu, bila kujali athari zinazoweza kujitokeza kwa Watanzania hawa ambao wamekuwa katika kisiwa cha amani kwa muda mrefu.

 

Sipendi kubashiri nini kinakuja mbele lakini nataka kutoa tahadhari juu ya uwajibikaji wa viongozi wetu katika kipindi hiki, ambacho tumebarikiwa kuwa na wasomi wengi waliobobea katika taaluma mbalimbali. Katika kipindi hiki hatukutarajia tuwe na malumbano ya kupingana wakati tuna wasomi waliotakiwa kutupatia majibu ya safari yetu ya maendeleo.

Ni miaka mingi tangu tumepata Uhuru, na tulipopata Uhuru tulikuwa na viongozi ambao wengi wao hawakuwa wasomi, lakini waliweza kutufikisha pale mahali tulipoanzisha Azimio la Arusha kwa lengo la kuweza kujitegemea kwa kushika njia kuu za uchumi wa Taifa letu.

Viongozi wale ambao hawakuwa wasomi leo nawakumbuka kwa uzalendo wao, uzalendo ambao ulijenga uongozi kuwa taasisi na si uamuzi wa mtu mmoja mmoja kwa malengo yake. Nawakumbuka kwa kujali maisha ya mpigakura ambaye ni mkulima na mfanyakazi na ndiyo maana leo tumeweza kuwa na wasomi waliosoma shule tulizojenga kwa nguvu ya Ujamaa wetu wa kujitolea na uzalendo.

Nawakumbuka viongozi wazalendo waliokuwa na msimamo katika kulinda maslahi ya Taifa na si maslahi ya mtu mmoja mmoja kama  leo tunavyoshuhudia kiongozi anavyomiliki mali nyingi tena ikiwa ni njia kuu ya uchumi wa Taifa. Mtu anamiliki reli, bandari, viwanda vyetu, mashamba yetu ya kilimo na mifugo, majengo yetu na kadhalika.

Tuliwapata viongozi kwa vigezo mbalimbali lakini kikubwa tulichozingatia ni mtu anayeweza akajitolea akili yake na nguvu yake katika kuleta maendeleo ya Taifa na si vinginevyo.

 

Nawakumbuka kwa kuwa tulikubaliana kwamba kiongozi wa kweli ni yule asiye na maslahi yoyote katika biashara, na ndiyo maana tukasema kiongozi bora ni yule atakayewatumikia wananchi na si mali zake.

Nadhani umefika wakati ambapo sasa wananchi tunapaswa kuhoji uhalali wa kulivunja Azimio la Arusha, ambalo kimsingi ndilo lililokuwa na vigezo vya kiongozi bora. Tutafute kijitabu kile na kukipitia upya ili tuone kama kuna umuhimu wa kubadili Katiba ama kukirudisha kijitabu cha Azimio la Arusha.

Napata taabu ninavyowaona viongozi wakivurunda na kuharibu uchumi wetu kwa kisingizio cha sheria huku wakijua kigezo chetu cha uongozi kipo na walikizika kwa manufaa yao. Tusipokuwa makini Watanzania hawa walioishi katika kisiwa cha amani kipindi chote hiki, watatafuta amani kwa nguvu na ndipo tutakapokuwa tumechukua akili za watu wa Kaskazini wakiamni ndiyo suluhisho la kila kitu.

 

Mzee Zuzu 
Kipatimo.

 

1543 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!