Wanangu, wakati wa ujana wetu kulikuwa na starehe nyingi ambazo leo nyie hamuwezi kuzifanya kwa gharama yoyote ile labda mjigeuze na kuomba kwa Mwenyezi Mungu miaka irudi nyuma na mpate nafasi ya kufaidi kama tulivyofaidi sisi.

Leo wanangu na utu uzima wangu, naziona jinsi starehe zenu zilivyo na wakati mgumu kuzifanya, sababu zipo nyingi sana, lakini labda niseme tu kwamba mna nafasi ndogo ya kuamua mfanye starehe gani hasa kutokana na mazingira ambayo mmejiwekea kwa kitu ambacho mnaita maendeleo.


Wakati wa ujana wetu, tulikuwa na starehe ya kuwinda wanyama ambao ushindi wake ulikuwa ni kupata kitoweo cha familia na wazazi walikuwa wakitupongeza kama tumecheza vizuri mchezo wa siku hiyo. Tuliwinda ndege na wanyama ambao ni wajanja kama kware, kitoto, sungura, swala na wengineo.


Wakati wa ujana wetu, muda mwingi pia tulitumia maeneo ya wazi kwa michezo kama kulima vijibustani vya mboga mboga na mazao ya muda mfupi. Tulipongezwa kwa michezo hiyo kwa sababu ilikuwa ikitufundisha jambo fulani la maana. Tulifanya hivyo baada ya kuona sinema za ukulima wa kisasa kutoka Wizara ya Kilimo wakati huo.


Wizara ya Kilimo ilikuwa na utaratibu wa kutuletea sinema za kilimo cha mazao mbalimbali katika uwanja wa wazi au shule. Nakumbuka zilikuwa ni Land Rover zilizokuwa zikileta burudani hiyo iliyokuwa ikitoa kijiji kizima kwa siku hiyo. Kwa hakika ilikuwa ni burudani tosha kuona jinsi ambavyo kahawa inalimwa, inatunzwa, inavunwa na kuhifadhiwa.


Ilikuwapo michezo ya “kijinga kidogo” kama kucheza mpira. Wakati huo nakumbuka kulikuwa na mashindano ya Goseji tuliyojifunza kucheza mpira pamoja na kwamba sheria tulikuwa hatuzijui. Wakati huo jezi hazikuwapo, hivyo kutofautisha wachezaji ilibidi senti tano irushwe juu na kuangali je, imeangukia samaki au kichwa na matokeo yake aliyepata humuamuru kapteni awaeleze wenzake wavue mashati wabaki waache vifua wazi.


Michezo hii pamoja na mingine haikuwa na tija sana katika maendeleo, lakini pia tulijitahidi kucheza vizuri na kuleta heshima kwa Taifa hili mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970. Kwa wanaokumbuka watajua kuwa ni katika kipindi hicho ndipo tulipotoa wachezaji bora wengi. Sitaki kuwataja kwa kuwa wengi wao ndiyo nembo ya Taifa katika kujivunia ushindi tuliokuwa tukiupata nje na ndani ya nchi.


Wanangu, naomba nikiri wazi kuwa mimi na vijana wenzangu wengi hatukucheza michezo hiyo na hivyo starehe yetu kubwa ilibaki katika uwindaji, ujenzi, ukulima na matokeo yake ndiyo hayo baada ya miaka michache na kuwa watu wazima tulitumia uzoefu wa michezo ile katika kutekeleza uhalisia wa maisha.


Wanangu, leo nimeamua kusema hili baada ya kuona tofauti kubwa ya starehe za leo na zile za kale. Zipo zinazoelekea kufanana kama vile muziki na hiyo michezo ya mpira, kukimbia, kutupa mikuki na mingineyo, lakini baadhi ya michezo mingi iitwayo ya starehe leo ni tofauti kabisa.


Michezo yetu ililenga katika kutufundisha maadili mema ya kimaisha kila siku. Baada ya michezo na miaka kadhaa kupita tulijikuta ni wakulima mahiri, wawindaji hodari, wavuvi wazuri, na kadhalika.

 

Leo, wanangu, naiona michezo mingi sana ikiwamo ile ya kimaendeleo kutokana na teknolojia ya sasa, na wazazi wa leo ambao wengi wao ni vijana wa zamani wanashindwa kutofautisha michezo yao na hii ya kisasa na faida au hasara itakayopatikana katika siku za usoni kwa kizazi chao.

 

Tuliangalia sinema zenye maana katika maisha yetu. Tuliangalia sinema za kilimo, ufugaji, uvuvi, na vita kidogo. Wakati huo hatukutofautiana sana na zile sinema ambazo wenzetu Wachina walikuwa wakiziangalia kama sisi. Sina hakika leo watoto wetu wanaangalia sinema gani, inawezekana zikawa za kilimo, ufugaji, na uvuvi. Hili naomba kubaki kuwa swali kwa kila anayesoma waraka wangu huu wa leo.


Tulicheza bao kwa nia ya kujifunza kuhesabu na kujua jinsi gani umkwepe mwenzako unayecheza naye. Leo nasikia kwa kusimuliwa kuwa kuna mabao ambayo si ya kuchonga, lakini ni ya kununua na kuyapachika katika umeme ili ucheze nalo. Yapo katika kompyuta, simu na kadhalika.


Wanangu, siwaonei gere michezo yenu, lakini nataka tujiulize kama watu wazima wenye kutoa mustakabali wa Taifa la kesho ambalo ni la watoto wetu. Tujiulize tunawapeleka wapi watoto hawa ambao kesho watapaswa kujua jema na baya?


Tujiulize, maendeleo yaondoe utamaduni wetu? Hivi watoto wetu wa leo wanajua kuwinda ndezi? Sungura? Panya? Au kuua nyoka? Hivi watoto wetu wanajua kulima mahindi, pamba, korosho, mchicha na mazao mengine ambayo ni lishe yao ya kila siku? Au wanajua kucheza michezo ya “game” katika kompyuta tu?


Wakati wa ujana wetu tuliangalia sinema za kutufundisha ukulima wa kisasa, ufugaji bora. Hivi tujiulize watoto wenu leo wanaangalia sinema gani huko katika mabanda ya video yaliyofunikwa magunia? Na ni mafunzo gani mazuri wanayopata baada ya kutoka hapo bandani? Sisi tulikuwa tukifanya mazoezi katika vibustani vidogo na wazazi wetu walikuwa wakitupongeza baada ya kuona mafunzo yametuingia.


Wakati wa ujana wetu tulikuwa tukisikiliza miziki yenye mafunzo kiasi kwamba tulipeana majina ya kejeli kwa wenzetu waliokuwa hawaendi na maisha yaliyoaswa katika wimbo tuliousikia. Tujiulize wanenu leo wanasikiliza nyimbo gani zenye mafunzo na kupeana majina ya kejeli kama kuna mtu anayeenda kinyume cha maadili ya utamaduni wetu?


Najua nimepitwa sana na wakati na ninapaswa kuchekwa kwa kudhani kwamba lazima kizazi hiki kiishi kama tulivyoishi sisi, lakini swali la msingi tunalopaswa kujua je, watoto hawa watakuwa na maadili gani kwa kizazi kijacho kama kilivyokuwa chetu?

 

Ningelipenda kila mtu ajiulize watoto wake wanajua michezo gani na wanajua nini kwa faida na umri wao. Kila mtu ajiulize watoto wanasikiliza nini na watajua nini kutokana na kile wanachosikia? Tujiulize, wanaona nini ambacho ni fundisho zuri kwao?


Ikiwezekana tuigeukie Serikali yetu na kuiuliza wanaandaa Taifa gani kwa kuacha kufundisha michezo yenye maadili mazuri shuleni na kuacha kufundisha masomo ya maadili mema kama ya kilimo, ufundi, upishi, ushonaji, ukerezaji na mengine; badala ya kuiachia jamii iliyoparaganyika kutoa mafunzo hayo huko uchochoroni?


Kama ningekuwa bado nina nguvu ya kuwa kiongozi, ningelazimisha wanenu waache michezo ya kisasa kwa vile haitufundishi jambo lolote kwa utamaduni wetu. Ningeanzisha utaratibu wa kufuatilia sehemu wanazocheza watoto kama sehemu zao za starehe na kadhalika.


Wanangu, naomba kila mmoja wenu mwenye mtoto ajiulize mwanawe anajifunza na anacheza michezo gani kwa faida ya maisha yake baadaye. Mimi miaka yangu imeisha, sijui nini kitatokea miaka ijayo kwa kizazi chenu na michezo na starehe zilizopo, lakini wazazi kama mpo liangalieni hilo.


Wasalaam,

Mzee Zuzu,

Kipatimo

0784 232768

By Jamhuri