Siku zote nawaambia kwamba miye umri ulinitupa mkono lakini kila siku napenda kuenzi kazi za mikono na thamani ya watu muhimu waliolitendea mema Taifa hili, thamani yao itazidi kuwa na maana kama sisi tuliopo tutaenzi na kuthamini kwa maana ya kuweka kumbukumbu zao vizuri kwa faida ya vizazi vijavyo.
Watu wachache sana wanaomsikia na kumsoma Shaaban Robert, huyu ni nguli wa fasihi ya lugha yetu, ni mwalimu na ameacha hazina isiyoweza kufutika kwa wanataaluma. Ikitokea siku moja wanataaluma wakaacha kumzungumzia katika matamasha mbalimbali ni dhahiri kuwa kizazi cha akina ‘dotcom’ kitaibuka na msanii wao ambaye hajaitendea haki jamii yetu na kumzika kwa mara ya pili Shaaban Robert na kazi zake muhimu kwa jamii yetu.

Watu wachache wanaweza kumzungumzia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa hali ilivyo sasa, tumegubikwa na siasa za maji taka na umaarufu wa kujitafutia kwa nguvu na sifa za kijinga. Ikumbukwe kuwa Nyerere ndiye aliyeasisi umoja wetu kama Taifa lilivyo leo, alipigania haki ya Mtanganyika na kujitoa mhanga kwa niaba ya wapiganaji wengine.
Mwalimu Nyerere alihukumiwa kwenda jela kwa kosa la kutaka usawa, bila kuwa na faini ya Sh. 12 ni dhahiri kuwa angekaa jela na kummaliza nguvu ya kisiasa. Nani anajua faini aliilipa nani?
Mambo mengi naona tunayatupa mkono kutokana na namna ya maisha ambayo tunaishi leo, tunachukulia mambo rahisi kuwa mazito, tunatunza rekodi ambazo kamwe hazina tija kwa Taifa letu na vizazi vijavyo, tunawatafuta watu waliojipa umaarufu hata kama ni kwa utapeli.

Taifa linapofikia kuwasujudu na kuweka kumbukumbu za wezi, matapeli, wajinga na wapumbavu ni dhahiri kuwa tunataka kuwa Taifa mfu kwa kukosa busara.
Tuna maeneo ambayo kwetu yalipaswa kuwa sehemu za kujivunia na kutengeneza kumbukumbu nzuri kwa ajili ya utalii na maendeleo ya Taifa, mathalani ukombozi wa Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara yalifanywa kisiasa zaidi na vyombo vya habari, matangazo yao yalirushwa kutokea External jijini Dar es Salaam.
Pamoja na hayo eneo hilo hadi sasa halina thamani ambayo naamini nchi zote ambazo zilitumia kituo hicho kufanya siasa ya ukombozi wangeelezwa kuja kutembelea na kuona fahari ya uhuru wao, nani asiyejua marais wengi wa nchi hizo waliishi Tanzania maeneo mbalimbali?

Nahofia uwekezaji unaopoteza sehemu muhimu za kumbukumbu, iwapi hoteli ambayo Nyerere alikunywa chai na akashitakiwa? Nataka kujua tu iko wapi hoteli ambayo mwakilishi wa mtawala wa Uingereza alifikia na kuondoka wakati tukiachiwa uhuru? Iko wapi ofisi ya urafiki wa mataifa ya Afrika, hivi tumeshindwa kutunza nyumba ya umbeya wa uhuru tuliyopewa na Mwafrika mwenzetu?
Tunasherehekea Sikukuu ya Mashujaa hivi sasa, nani anayemkumbuka Mtanzania aliyepanda Mlima Kilimanjaro mwaka 1961 na kusimika Bendera ya Taifa alfajiri ya siku hiyo, mnajua kulikuwa na ubaridi kiasi gani.

Aidha, Mwenge wa Uhuru aliwashwaje alifajiri hiyo, maandiko yake yako wapi na kumbukumbu yake iko wapi, hivi shujaa wetu ni yupi  katika orodha ya mashujaa, nani anamkumbuka mkuu wa majeshi wa kwanza aliyezima mapinduzi yaliyotaka kufanyika?
Ni vizuri tukawa na kumbukumbu kama Taifa ili kesho tujifunze kutoka kwao na siyo mambo ya majitaka tunayapa kipaumbele kama mambo muhimu kwa Taifa, hivi wale mashujaa wetu walioanguka na ndege za kivita siku ya mashujaa na baada ya kumaliza vita ya juzi tu hapa, walijengewa wapi mnara wa kumbukumbu? Sitashangaa kuona eneo hilo la ajali kuwa ni baa hivi leo, abishaye aende hapo Temeke nje tu ya Uwanja wa Uhuru anipe taarifa kuna nini kimeendelezwa kwa manufaa ya kumbukumbu ili nijue.

Kuna Watanzania wamepata nishani za juu sana kimataifa kwa kazi nzuri, nani anawakumbuka na taarifa zao ziko wapi, nani anamkumbuka wakili wa kwanza Mtanzania, nani anamkumbuka jaji wa kwanza Mtanzania, nani anamkumbuka aliyeongoza Vita ya Uganda, aliyechora Nembo ya Taifa, aliyeishi na sokwe Kigoma kwa muda mrefu.
Nimeamua kuwachokoza kizazi cha ‘dotcom’ lakini najua majibu yapo mengi na labda hakuna umuhimu wa kujua hayo leo. Wekeni msisitizo wa kuwatambua wasanii wa filamu na muziki wa kizazi chenu halafu akina Juma Kilaza na Mbaraka Mwinshehe waliopigania tasnia ya muziki muwaweke kando, vivyo hivyo Mzee Kawawa na filamu yake mwacheni kama alivyo.

Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo. 

920 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!