Yah: Tunahitaji utashi, si lazima kuishi kama kenge

Kuna wakati huwa najiuliza maswali mengi ambayo kimsingi naona yanajibiwa na idadi kubwa ya shule za misingi, sekondari na vyuo vikuu vilivyopo. Najiuliza tuna wasomi wangapi?

Usomi ni vyeti au shahada aina zote ama kusaidia kutatua matatizo? Najiuliza dhana ya sheria ni msumeno ni kukata ama kutokunjika? Leo nimeona ni vyema niandike waraka wangu wa kutaka kuwauliza wenye mamlaka juu ya mambo ambayo kimsingi, huwa sielewi tuna maana gani ya kuwa na hao tunaowaita wahitimu ama tuliowapa madaraka kutokana na vyeti vyao vya elimu.

Kuna mambo ambayo ukitaka kujua ustaarabu wa mtu, ni pale anaposhindwa kuelewa sababu ya mkosaji kushindwa kuvumilia kosa lake na hata anapotoa sababu ya kujitetea anakuwa haeleweki kwa huyo tuliyempa madaraka.

Napenda sana kukubaliana na baadhi ya mahakimu na majaji ambao hutoa uamuzi unaokuwa tofauti na wengi walivyokusudia kutokana na utashi unaotumika. Nimeshuhudia baadhi ya mahakimu na majaji wakiwaachia watuhumiwa kutokana na sababu za kibinadamu zaidi kuliko sheria inavyosema.

Lengo langu kubwa leo katika waraka wangu huu ni askari wa usalama barabarani, ambao baadhi yao wamekuwa wakifanya kazi kama sheria haiwezi kuvunjwa kwa nia njema na kwa faida ya Taifa na watumiaji wa barabarani.

 

Mathalani, sioni sababu ya msingi askari kuzuia magari yasipite mahali kwa sababu tu kumetokea ajali, ambayo bado haijapimwa bila kuzingatia muda na hao abiria ndani ya magari hayo wana majukumu gani mbele.

Nilipata kushuhudia askari wa usalama barabarani kwa kutumia wadhifa wake, akikataa kupitisha gari ambalo alikuwa akilitumia daktari aliyeomba awahi kwenda hospitali kutoa matibabu, baada ya kuitwa na wasaidizi wake kwamba hali ya mgonjwa ni tete.

 

Askari yule alishindwa kutumia utashi wake na badala yake alitumia ubabe na kutaka kujionesha yeye ni nani katika nchi hii. Hivi sasa barabara nyingi zinatengenezwa katika mikoa mingi, watengenezaji hawatengi sehemu mbadala za kutosha na muhimu kwa wanaoendelea na safari, lakini katika gharama za ujenzi wa barabara yote hayo huzingatiwa na kupewa gharama zake. Inatokea mkandarasi anafunga njia muhimu kwa matumizi na kuwafanya watumiaji wa barabara kushindwa kutumia ipasavyo.

Inapotokea hivyo, watumiaji hutumia njia nyingine ambayo kimsingi ni kosa, lakini askari ambao tumewapa dhima hiyo ya barabara huanza kufikiria kosa badala ya chanzo na kuchukulia makosa hayo kama sehemu ya mapato yao. Tumeshuhudia wengi wakilipa faini kwa uonevu na baadhi kupelekwa mahakamani.

Uzoefu wa kisaikojia unaonesha kwamba mtu anayeonewa huwa mnyonge na kushindwa kuvumilia, na badala yake anaweza akawaonea wengine pia kwa kutenda makosa makubwa zaidi ya lile alilolifanya. Madereva ni moja ya watu wanaoonewa sana na hawa askari wa usalama barabarani, ambao baadhi yao wanashindwa kutumia utashi katika kutanzua masuala ya kibinadamu.

Sikusudii kusema sheria zivunjwe, la hasha, tuangalie mazingira ya mkosaji kabla ya kuchukua hatua za kisheria bila kujua na kuhoji uhalali wa mkosaji kufanya kosa. Tukiamua kutoa hukumu bila kusikiliza upande wa pili ni sawasawa na hakimu kupelekewa kesi na akasikiliza maelezo ya mshitaki na kutoa hukumu.

Tumeshuhudia baadhi ya  askari wetu wakishindwa kutoa hoja, na badala yake wanatumia mabavu kutekeleza azma yao ya kumtuhumu dereva na kumpeleka mahakamani ambako hakimu hutumia muda mfupi kutanzua kosa hilo kwa kutumia utashi wa kibinadamu.

Baadhi yetu hatujui madhara ya kutumia vibaya sheria bila kuzingatia utashi wa mambo yanayotuzunguka. Mathalani kiuchumi ni makosa kutumia mafuta mengi kuzunguka umbali mrefu kumpeleka mgonjwa hospitali, lakini pia ni hatari kuchukua muda mrefu kumfikisha mgonjwa hospitalini kwa sababu ya kuzunguka njia ndefu. Hapo ndipo tunapokuwa kama kenge kwamba usomi wetu hautusaidii kutanzua mambo ya msingi badala yake tunakwenda kama reli.

Mifano ipo mingi katika suala hili la kutumia nguvu ya kisheria hasa kwa upande wa usalama wa barabarani. Kuna ujenzi wa barabara jijini Dar es Salaam, kila mtu anaweza akawa shuhuda wa jinsi mkandarasi huyu alivyoshindwa kutoa njia mbadala kutokana na kuziba njia za msingi.

 

Askari wetu badala ya kuhoji na kuwasaidia wananchi wanaotumia njia hiyo, wao wanakaa mahala ambapo wanadhani watumiaji watapita kuwahi majukumu yao, na hapo ndipo hutumia wadhifa na madaraka yao kuwakomoa madereva badala ya kuhoji makosa ya mkandarasi.

 

Wachumi wanajaribu kufikiria kupunguza matumizi ya mafuta ambayo si malighafi yetu, tunatumia fedha nyingi za kigeni ambazo tungeweza kununua dawa, vitendea kazi na kadhalika, lakini tunashindwa kudhibiti matumizi ya mafuta kutokana na makosa ambayo tunashindwa kuyatanzua, kisa sheria iliyoandikwa na kushindwa kutumia utashi wa kawaida.

Wafanyakazi wa aina zote — walimu, waganga, wahasibu na kadhalika — wanajaribu kufikiria muda wanaopoteza barabarani kwa sababu kuna mtu yupo kama msumeno, hataki kusikia na kuelewa jambo dogo la kibinadamu mbele yao.

Askari anatafuta makosa badala ya kuyaona yaliyopo mbele yake, anaona magari mabovu yakitiririsha moshi na uchakavu wa bodi, lakini anagombana na mtu ambaye hajafunga mkanda katika gari jipya pembeni. Ni aibu kwa mtumishi wa aina hiyo.

Madereva wengi sasa wanawaona askari hawa kama maadui badala ya kuwa marafiki katika uwanja wao, ndiyo maana askari wa usalama wa raia walipoona wametengwa na wananchi walianzisha ulinzi shirikishi na polisi rafiki wamepata matokeo mazuri.

Alipo askari ndipo salama zaidi, si mahali pa kupakimbia. Tunatakiwa kutumia saikolojia ndogo ya kujua makosa na jinsi ya kuyadhibiti. Kuwa askari hakumaanishi uwe kama sanamu usiyesikia na kutumia utashi, hali kadhalika vyombo vingine pia maofisa walioko katika ofisi za Serikali tumieni pia utashi, walinzi, masekretari na kadhalika.

 

Haya ni mawazo yangu. Tuwe na ubinadamu, sheria tumezitunga sisi na tunaweza kuzifanyia marekebisho, tusiwe kama kenge kwamba njia ni moja tu hatuwezi kuepa. Tutakuwa tunachekwa!

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu 
Kipatimo.