Majuzi tulikuwa tunakumbuka kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tulikuwa na kumbukizi ya mambo mengi sana juu ya nchi yetu na falsafa yake ya ujamaa na kujitegemea, falsafa ya uhuru ni kazi na haki ya kila raia katika nchi hii, lakini ni wachache walioongelea kuhusu demokrasia na uhuru ni kazi.

Kuna mengi unaweza ukamkumbuka Mwalimu, wapo watakaomkumbuka kwa mchezo wa bao, wapo watakaomkumbuka kwa utani wake, wapo watakaomkumbuka kwa ukweli unaouma, ambao alikuwa hajui kuuonea haya, wapo watakaomkumbuka kwa Kiingereza chake kizuri na wapo watakaomkumbuka kwa Kiswahili chake mwanana, lakini wapo watakaomkumbuka kama Mzanaki tu na si Mkara. 

 

Wiki jana tumeadhimisha  miongo hii miwili bila Nyerere, si jambo dogo kukaa bila Mwalimu kwa kipindi chote hicho nchi ikiwa katika amani na utulivu mpaka leo. Nakumbuka kauli ya rais wetu wa awamu ile ya kifo cha Mwalimu Nyerere alipokuwa anatoa taarifa ya kifo chake na kututaka tuwe watulivu kipindi kile, na ninaona mwangwi wa sauti yake ikiendelea kutulinda kama taifa katika kipindi kigumu cha mapito na majaribu ya wenye uchu.

Hii ndiyo Tanzania ambayo Mwalimu Nyerere aliijenga usiku na mchana, Tanzania ya watu kulala kwa amani na kuamka kwa amani, taifa lenye kuheshimu sheria na utawala bora, taifa lenye msimamo wa uzalendo na kila mtu kuwa huru juu ya ardhi ya taifa hili, ni Mwalimu aliyewalea vijana wa zamani ambao baadhi yao ni viongozi leo.

 

 Tumefanya kumbukizi nyingi sana lakini kwetu wazee ambao tunaweza kumkumbuka Mwalimu tunaona kama tuko katika usingizi mzito wenye njozi za kutisha na kuchekesha, tunaona dhamira kwa taifa hili na tunaona safari ilivyokuwa ngumu. 

Ni katika kipindi hiki ambacho uwepo wake ni wa kiroho zaidi ndipo tunapoona baadhi ya mambo ambayo tunaweza tukahoji kwanini alitwaliwa mapema ili asiwepo na kudhibiti mambo haya? Unajiuliza, ni Tanzania hii ambayo yeye aliiasisi kwa kujinasibu kwamba nchi yetu kilimo ndio utu wa mgongo?

 

Ni Tanzania hii hii ambayo alipiga vita rushwa kwa moyo wote lakini siku chache tu baada ya kifo chake watu walijichukulia mlungula kwenye mifuko ya sandarusi?

Naona ni usiku wa giza totoro na kama kuna jinamizi limenikaba lakini pia nina ndoto nzito, naota Watanzania wanamuangalia Mtanzania mwenzao akifanyiwa unyama lakini Watanzania hawa wako ‘busy’ na harakati za kutafuta fedha, namuona Mwalimu anapotukanya juu ya thamani ya utu kwa kulinganisha na fedha. 

 

Ndoto ni mbaya sana, nasikia kauli ya Mwalimu juu ya uhakika wa maisha ya Mtanzania, lakini kwa mbali nawaona watu wakiwa wamenyoosha mikono, ni kama wametekwa na wanapelekwa porini, nawaona askari wakirushiana risasi na Watanzania wachache walioamua kujiundia mamlaka yao ndani ya mamlaka halisi, hii ndoto inanitisha. 

Najitahidi kuamka lakini jinamizi linanishika vibaya, nasikia kauli za wanademokrasia wa ajabu ajabu juu ya kila kitu hata yale ambayo ni ya msingi kwa taifa letu, naona gari la mitihani likisimamishwa na mitihani kufunguliwa ili wapewe watahiniwa kabla ya mtihani, na kwa mbali nakiona kizazi cha wajinga wenye vyeti vizuri. 

 

Nawaona viongozi wanavyopingana na ukweli wa maisha ya Mtanzania halisi, huyu anasema hivi na yule anampinga, ninashuhudia mabishano lakini hakuna kazi na siku inakwisha, naona maghala ya chakula yakiwa na mizoga ya panya waliokufa kwa njaa, najiuliza ni lini tutaanza kuthamini akiba ya chakula?

Na baada ya kuthamini chakula ni lini wakulima watakuwa na thamani katika nchi ya kusadikika ya kilimo kuwa uti wa mgongo? 

 

Nawaona watoto wadogo wakiwa kwenye hatari ya kutekwa na wenye uchu wa utajiri wa harakaharaka bila kufanya kazi, imani za kishirikina zikiwa zimepewa kipaumbele na kila mwananchi, nayasikia matangazo katika redio na televisheni zetu, nayaona matangazo katika kuta mbalimbali za matangazo rasmi, mwisho najiuliza kuna watu katika ofisi au wapo likizo? 

Namkumbuka Nyerere kwa mengi, lakini ndoto inakata ghafla ninaposikia kelele nje kwamba kuna mtu ametekwa kweli, najiuliza niliyokuwa nikiota ni kweli yanasadifu uhalisia? Najiuliza, hii ndiyo Tanzania ya Nyerere? Tutafika kweli? Tunamuenzi vipi?

 

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.  

By Jamhuri