17 Sep 1976, Dar es Salaam, Tanzania Julius K. Nyerere 

Mwanangu Julius, ualimu na siasa havipatani hata kidogo, fuata oni langu, uache kabisa mambo ya siasa na uzingatie kazi yako ya ualimu.” Kauli hii ilitamkwa na Padri Mkuu wa Shule ya St. Francis’ College, Mwakanga, Pugu (sasa ni Pugu Sekondari, Mkoa wa Dar es Salaam), kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, siku ya Jumapili,  Machi 22, 1955.

Padri Mkuu alitamka maneno haya baada ya siku moja tu Mwalimu Julius Nyerere kurejea nchini, Jumamosi, Machi 21, 1955 kutoka UNO (United Nations Organization), New York, Marekani, kwenye Baraza la Wadhamini la Umoja wa Mataifa katika kudai Uhuru wa Watanganyika. 

Katika mkutano wao, maneno haya ya padri mkuu wa shule yalipenya ndani ya mishipa ya fahamu na kutua ndani ya moyo wa Mwalimu Julius Nyerere na kujaza ujasiri, ushupavu na matumaini ya kutenda jambo lolote lenye uamuzi wa ndiyo au hapana.  

Baada ya mkutano, Mwalimu Nyerere alitoka nje na kwenda nyumbani kwake. Alipokuwa nyumbani alizidi kuyafikiri maneno haya na kujiuliza afanye nini. Aliambiwa achague kati ya sifa ya usalama wa kazi ya ualimu au kujitosa katika bahari ya siasa. Hakika ulikuwa mtihani mkubwa mbele yake. 

Katika kitambo kidogo, alipiga moyo konde na kumkabili padri mkuu wa shule, akampa barua ya kujiuzulu, kwa maana ya kuacha kazi ya ualimu na kwenda kupiga mbizi katika bahari ya siasa. Akazama na akaibuka na Uhuru wa Tanganyika, Desemba 9, 1961. Wananchi wote walifurahia. 

Katika kipindi cha uongozi wake kwenye vyama vya siasa na utawala serikalini tangu mwaka 1961 hadi mwaka 1985, Mwalimu Nyerere amefanya mambo mengi ya ukombozi wa Mtanganyika na Mtanzania katika utu wake, utamaduni wake, uungwana wake na uhodhi wa rasilimali zake. 

Mwalimu Nyerere amerejesha heshima na haki ya Mtanzania. Ameelimisha maarifa mbalimbali, ameonyesha matendo kadha wa kadha na amesuluhisha migongano na migogoro mingi kati ya Watanzania na hata Afrika na duniani. Mwananchi gani asiyeona wema huu? 

Mimi au wewe, laiti tungepewa nafasi ya kueleza na kuandika wasifu wake, ukweli tungehitaji maktaba nyingi za vitabu, magazeti na kanda za simulizi tele. Na wala isingekuwa kifu kusimulia na kusikiliza kwa sababu kauli na matendo yake hayasigani, ni mamoja. Hakika ni kiongozi wa mfano mzuri wa kuigwa. 

Tangu Oktoba Mosi, mwaka huu, kila pembe ya nchi yetu Watanzania wamo katika kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, baada ya kututoka duniani miaka 19 iliyopita (Oktoba 14, 1999 – Oktoba 14, 2018) Tuendelee kumwombea heri katika sala mbalimbali kwa Mungu. Amina! 

Tukiwa katika kumbukizi, yatupasa kukumbuka na kuzingatia ni kweli tunamuenzi katika kauli na matendo yake kwa dhati au tunafunika kombe ili mambo yapite? Hebu tukumbuke alivyopiga moyo wake konde kuacha kazi yenye manufaa kwake na kutafuta manufaa ya wananchi wote wa nchi yetu. 

Mwalimu Nyerere ameleta ukombozi wa kujitegemea kiuchumi, amerejesha utamaduni wetu na kutukumbusha kuwa kufanya kazi ni uungwana, si utwana. Vipi leo sisi tushindwe kudumisha uchumi wetu? Tunapozozana kiuchumi na kisiasa katika misingi ya kujitegemea ndiyo tunamuenzi Mwalimu Nyerere? 

Tunaponukuu kauli au maneno yake katika mazungumzo au katika mikutano ya ndani na ya nje ni uungwana na tunaonyesha pasipo shaka mahaba tuliyonayo kwake. 

Je, ndani ya miaka 19 bila Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tumeendeleza na kudumisha maendeleo yetu katika kujenga uchumi wetu, kutoa huduma bora kwa jamii, kulinda utamaduni wetu na kutumia ipasavyo falsafa yake? Kinyume cha haya, ukweli hatumuenzi Mwalimu Nyerere. 

Please follow and like us:
Pin Share