Moja kati ya misingi ninayoamini mimi ni kwamba utumishi wa umma ni thamani na siyo utumishi wa moja kwa moja au kurithi. Mimi ni muumini wa demokrasia ya uongozi wa Taifa kwa maana ya kila mwenye uwezo apate nafasi alitumikie Taifa.

Bado kuna dhana ya utawala wa kichifu na bado kuna dhana ya akina fulani ndiyo wenye uwezo wa kuongoza, hili nalipinga kwa nguvu zangu zote na nitaendelea kulipinga hadi pale nitakapothibitishiwa kuwa utawala wa nchi hii ni wa kifalme na kidikteta, wenye kutawala watakuwa akina fulani na akina fulani watakuwa watawaliwa.

Watu wengi wamekuwa wakihoji uteuzi mbalimbali ambao unafanyika katika awamu hii, wana haki ya kuhoji lakini hawana haki ya kukataa uteuzi, mamlaka ya uteuzi ndiyo inayopaswa kuulizwa baada ya kuvurunda. Ni awamu hii ndiyo nayaona maswali mengi juu ya uteuzi, nadhani kuna siri ya watu wanaohoji.

Mimi ni mmoja wa watu wachache ambao najivunia rehema za Mwenyezi Mungu kunipa baraka ya kuzishuhudia awamu zote tano za uongozi wa nchi hii, niliiona awamu ya kwanza na sasa nashuhudia awamu ya tano, nayajua mageuzi ya kiuongozi na ninajua mwanzo wa tatizo ambalo leo linatukabili katika kuhoji uteuzi.

Moja kati ya siku za kufuturu yaliibuka maneno ya kudai kwamba hali ya fedha mitaani ni mbaya, sikumbuki na sijui ni nani alisema kwamba hali hii muda si mrefu itatengemaa kama tutafanya kazi kwa bidii kila mmoja mahala pake pa kazi, kwa ufupi kauli hii inamaanisha watu wengi tuliweza kumudu kuwa na fedha bila kufanya kazi.

Kama nilivyosema nilikuwapo awamu zote, maisha ya Mtanzania nayajua. Ana baraka ya kuwa na amani na ana baraka ya kusema chochote zaidi ya demokrasia inavyomruhusu, ana baraka ya uvivu, ana baraka ya kutoa mawazo hata kama ni ya uvunjifu wa amani, Mtanzania wa sasa ni dalali zaidi ya kufanya kazi.

Katika awamu hizi nchi yetu imebarikiwa kutoa fursa ya kazi nyingi sana kwa kizazi cha nguvukazi, kizazi kile cha kila mwenye miaka 18 kumiliki shamba la mazao ya chakula na shamba la mazao ya biashara. Sisi tulipata maadili hayo ya nguvukazi na kwamba ilikuwa bila kujali unaishi mjini au umeajiriwa.

Hivi karibuni, sera zilibadilika sana, kizazi cha nguvukazi kilibadilishiwa majukumu ikawa kumiliki ofisi za udalali, pikipiki, siasa na mambo mengine yasiyohusiana na kilimo, uvuvi, kazi za viwandani na kadhalika. Ni kizazi kilichofundishwa kupokea hela ukiwa umekaa kitako, ni kizazi cha kutumia rasilimali zetu kujipatia kipato kwa kuuza kila kitu tulichofanya enzi zile.

Hivi sasa lawama zinazotolewa katika uteuzi huu zinatokana na kufumua mfumo wa kujipatia riziki bila kufanya kazi, tulishuhudia watu wakiwa na fedha bila kufanya kazi, tuliona watu wakimiliki mali kwa njia za ujanjaujanja na kudharau watu wanaofanya kazi, kwa ufupi kulikuwa na mfumko wa matajiri katika nchi maskini.

Uteuzi huu unaolalamikiwa ni kwamba umekamata kona zote za mapato yasiyo rasmi, uteuzi unaonekana kuwa mwiba kwa wale waliozowea kupata fedha kwa njia za udanganyifu, mwiba kwa madalali, mwiba kwa familia nyingi zilizoona cheo siyo dhamana bali ni haki yao.

Uteuzi wa awamu ya tano ambao unaenda sanjari na kaulimbiu ya hapa kazi tu nauona unaweza kuturudisha kule kwenye heshima ya kazi. Watu walizowea kufanya kazi kwa mazowea, watu waliona vyeo na mali zao, watu walibweteka katika utumishi, vyeo vilikuwa vya familia na ndugu kwamba hata mke na mtoto walikuwa wakivaa joho la cheo cha baba.

Watu walinyanyasika na kugeuka kuwa watumwa kwa baadhi ya familia ambazo zilikuwa ‘mambo safi’, sasa sote turudi huku chini tufanye kazi kuleta mabadiliko, sisi tulioko huku hatuna tatizo ndiyo mazowea yetu, wanaolalamika ni wageni wetu walioshuka na ambao walikuwa madalali, sasa ni kazi tu.

Nitaendelea kuandika juu ya mabadiliko ya hapa kazi tu

 

Wasaalam,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri