Kuna mtu mmoja aliniambia kuwa sasa hivi ukitaka kutukanwa tangaza kutoa rushwa kwa mtu yeyote, kuna watu waliokuwa wamezowea kupokea milungula kila siku na sasa hivi wanaogopa kama vile moto wa jehanam, hawataki kusikia kitu kiitwacho rushwa.

Sikutarajia hata siku moja kusikia nchi yetu inaweza kwenda bila kitu kiitwacho rushwa, kuna watu waligeuza rushwa kuwa sehemu ya haki yao, kimsingi kama hawawezi kupata malipo hayo waliona maisha hayawezi kwenda, rushwa iligeuka kuwa chachandu ya maisha.

Wakati nikikua, wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza, Rais Julius Nyerere aliwahi kusema rushwa ni adui wa haki, palipo na rushwa hakuna haki na haya sasa hivi tunaona jinsi yanavyodhihiri kila uchao katika sekta mbalimbali hapa nchini, inaonesha ni jinsi gani rushwa ilivyotutafuna.

Ukianza upande wa ardhi utaona jinsi watu wachache walivyoweza kumiliki maeneo makubwa isivyo halali, walimiliki maeneo ya umma kwa kupindisha sheria za ardhi na kuweza kuwakosesha walio wengi haki yao kwa uwezo wa rushwa.

Maeneo makubwa ya wazi ambayo yalitengwa kwa ajili ya huduma za jamii kama shule, masoko, zahanati maeneo ya kucheza watoto na yale ya wazi watu kupumzika, yaliuzwa kinyemela na kugeuzwa maeneo ya watu binafsi kwa matumizi binafsi kwa uwekezaji wao wa kuingiza kipato.

Ukija upande wa usalama barabarani, leseni zilitolewa kwa majina na watu kupelekewa majumbani huku wakiwa hawajui hata kuwasha gari, wapo ambao walipoteza maisha kwa ajali lakini pia wapo ambao waliuawa kwa ajali na wapo ambao walisababisha ulemavu kwa watu wasio na hatia kwa kosa dogo tu la kutumia rushwa kupata leseni.

Ukienda hospitali watu walizowea kuwa hakuna huduma ya afya  unayoweza kuipata bila kutoa chochote, kila mtu alikula katika meza yake, waliokosa fedha taslimu iliwabidi watafute mifugo na chochote ili waweze kupata huduma ya kutibiwa.

Ni kama vile nchi ilikuwa ikielekea Sodoma na Gomora kwa janga la rushwa, mahakamani ambapo haki ilitegemewa ipatikane ilikuwa ni shida, makarani walichanganya mafaili kuchelewesha kesi kwa sababu ya mlungula, makarani na mawakili wasiowaaminifu walikula njama za kupoteza ushahidi ili mtoa rushwa aweze kupata ushindi katika kesi.

Madereva waliendesha wanavyotaka bila kufuata sheria, usafiri ilikuwa ni nusu kifo lakini sasa tuna uhakika na safari yetu, tunaenda na tunafika salama, askari wanatimiza wajibu wao wa kusimamia usalama barabarani bila kupokea hongo, sasa tunajua haki yetu kwa kuwa rushwa haipokewi tena.

Rushwa ilitamalaki katika sekta ya elimu, kupata cheti lilikuwa ni suala la fedha tu na siyo maarifa yatokanayo na elimu, walimu walipoteza maadili yao ya kazi na kuweka mbele rushwa kama kigezo cha elimu, Taifa likaangamia kwa kuwa na vilaza wengi wenye kulididimiza Taifa badala ya kuliendeleza.

Rushwa ilitawala nchi na kufanya kila kitu kuwa ni fedha mbele, Taifa lilikosa mapato yake kutokana na rushwa na watu wachache walijineemesha kwa kupokea ama kutoa rushwa. Sekta zote ambazo ni muhimu kwa Taifa zilivamiwa na wahuni ambao ni wapokea rushwa na kulifanya Taifa kuwa katika wakati mgumu.

Mheshimiwa Rais aliposema hataki rushwa kwa siku moja tu mambo yalibadilika, kila mmoja alianza kuogopa kupokea rushwa na haki ikaanza kupatikana, tukaanza kufuatilia mambo ya nyuma ambayo yote yanaonesha dalili za rushwa.

Wazo langu; nadhani suala la rushwa liwe ni vita kubwa ya kumuunga mkono Rais na bila haya tumsaidie kupigana vita hii ili siku moja tuone rushwa ni adui wa haki na rushwa siyo sehemu ya maisha yetu, hapo ndipo tutakapoanza kuishi maisha halali. 

Utii huu ni mwanzo wa mkuu kuheshimu utawala wa sheria na sisi wengine tuseme yatosha katika suala la rushwa tutaona mabadiliko makubwa siku za jirani.

 

Wasaalamu,

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1008 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!