Yah: Uzalendo uliondoka kama Ujamaa na Kujitegemea?

Wanangu, leo nimeamka nikiwa na siha njema kabisa na kufurahi kwamba sasa mmeanza kuyaona yale ambayo labda sisi watu tunaoonekana wazee, mnaweza kuyaangalia kwa kina na kuyatafutia ufumbuzi wa kina ili tuondoke hapa tulipo twende huko kulikokuwa kunatarajiwa na wengi.
Wanangu, naandika barua hii nikiwa bado na fikra za zamani ambazo leo hazina tija kabisa katika mfumo huu wa vyama vingi, lakini bado kwa mawazo yangu ya zamani naona kuna kila dalili za kuwa na tija kwa chama tawala kwa wakati wake.

Zamani, wanangu wakati tuko katika mfumo wa chama kimoja, tulikuwa tunaamini kwamba mawazo ya mwenyekiti wa chama ndiyo mawazo mazuri na tulikuwa tukiyaombea yadumu ili tuweze kusonga mbele. Na kwa bahati mbaya mwenyekiti huyo alikuwa mmoja tu hadi anang’atuka madarakani yaani Julius Kambarage Nyerere.

Wakati wetu tulipokuwa tukisema ‘zidumu fikra za mwenyekiti wa TANU’ tulikuwa tunamaanisha mawazo yake na ya wajumbe wa chama cha TANU. Tulikuwa tukiamini  yana lengo la kutukomboa kiuchumi na kuleta umoja katika awamu zetu za mtindo wa siasa tuliokuwa tunautumia kwa kipindi maalumu cha miaka michache.

Labda niwakumbushe suala la hivi karibuni wakati tukiingia katika vita ya kumtoa Idi Amin kule Kagera. Baadhi yenu mlikuwa wadogo hamkumbuki, lakini Julius alipotangaza vita pale Diamond Jubilee, jeshi letu lilikuwa dogo sana kiasi cha kuanza kuwatumia waliokuwapo wakati huo na wengine kuanza kuwafundisha mgambo sehemu mbalimbali za nchi hii.

Kutokana na moyo tuliokuwa nao kwa mwenyekiti wa chama chetu, imani tuliyokuwa nayo kwa mwenyekiti na mawazo yake tukiyaamini, watu walithubutu kwenda wao wenyewe katika ofisi za kijiji na kujiandikisha kwa ajili ya mafunzo ya mgambo ili waende mstari wa mbele kumtoa nduli.

Wazee na watoto waliobakia nyumbani walifanya kazi kwa bidii ili tuweze kupata chakula cha kuwalisha wapiganaji wetu, hali kadhalika walichanga kila kinachowezekana ili kipelekwe vitani. Wapo waliochanga ng’ombe, kondoo, mbuzi, kuku, mahindi, mchele na hata mayai. Huo wanangu ulikuwa ni moyo wa kujitolea kutokana na mfumo wetu wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Wakati haya yote yakifanyika, kamati za siasa na ulinzi za wilaya na mkoa zilikuwa zikijadili hotuba ya mwenyekiti na kuchukua uamuzi wa haraka katika kukabiliana na vita iliyo mbele yetu. Leo, nathubutu kusema kwamba vita ya Uganda ilikuja ghafla pasi na maandalizi, hivyo hatukuwa tumejiaanda kuingia vitani na ndiyo maana baada ya vita kwisha tuliamua kufunga mikanda kwa miezi kumi na minane ili tuweze kulipa madeni tuliyoingia kutokana na vita ile.

Lakini pia tukumbushane uzalendo tuliokuwa nao kutokana na kuamini fikra za mwenyekiti wa chama baada ya hotuba ile ya kututaka tufunge mikanda. Tulipiga ndulu na vigelegele kuashiria tumeelewa lengo kamili la mwenyekiti na tukaanza kilimo cha kufa na kupona, tukaamua kuuza nje tu badala ya kuagiza kutoka nje ili tuwe na akiba ya fedha za kigeni kuweza kununulia mahitaji muhimu tu.

Tuliishi hivyo kwa hali ngumu sana, tulikosa nguo, mafuta, huduma muhimu za kijamii kama dawa, sukari na hadi chumvi. Viatu tukavaa matairi ya magari (makata mbuga)kuanzia mwanakijiji hadi mkuu wa mkoa, tulifanya hivyo kwa moyo mmoja tukiamini kuwa tunajiletea maendeleo yetu wenyewe.

Nimetoa mfano huo wa vita ya Uganda nikiamini kuwa suala hilo ni moja ya vitu ambavyo vilitusukuma katika kufikiria maendeleo kwa wakati wetu, kwamba tulifika mahali tulikuwa tunaweza kujenga barabara zetu wenyewe, kusomesha pasi na gharama wenyewe na kutoa huduma za afya na elimu kwa uwezo wetu kabla hatujanyang’anywa na vita ile.

Wanangu, leo nawaandikia barua hii baada ya kuhakikisha kuwa hatuwezi tena kuingia vitani baada ya kumtoa Idi Amin ambaye ndiye aliyekuwa kikwazo kwetu kwa wakati huo na sasa tuna vita ya kujiletea maendeleo ambayo hayahusiani na uhai kama vita, bali akili ya watu wachache kututoa hapa tulipo na kumaliza vita ya umasikini.

Hawa watu wachache tusiotaka kuamini katika fikra za mwenyekiti peke yake tunatarajia zaidi watumie uwezo wao wa akili katika kupambana na vita hii. Kumbukeni kuwa nchi hii ikipata uhuru ilikuwa na mainjinia wawili na madaktari kumi na wawili tu.

Leo wasomi tunao wengi kupindukia na wengi wao ni wale  waliosoma bure kwa nguvu zetu za Ujamaa na Kujitegemea, wapo mainjinia zaidi ya 10,000, tunao madaktari yawezekana idadi hiyo hiyo, tunao wachumi, watabiri, wasomi wa elimu dunia, wanasayansi wa ukweli na teknolojia ya kisasa ambao ni jeshi kubwa na zuri kuingia vitani.

Wapo wanasiasa waliosoma katika nyanja mbalimbali na wamekuwa chachu ya maendeleo kama ambavyo tunashuhudia kutoka ‘mjengoni’, wakipambana na kutoa hoja za msingi katika kukabiliana na vita hii iliyopo mbele yetu.

Wanangu, wanasiasa hawa nisingependa warejee katika awamu yetu ya kuamini katika fikra za mwenyekiti wa chama, bali wamsaidie ili aweze kukabiliana na matatizo yanalolikabili taifa letu. Watumie fursa walizonazo katika kutoa ushauri bora na si bora ushauri ili kwa pamoja siku moja tuseme zidumu fikra zake.

Wanangu, sina hakika na msimamo wenu wa kizazi cha dot. com, lakini sisi wazee tungelipenda moyo wa uzalendo tuliokuwa nao enzi hizo hadi siku hizi za karibuni wakati tukipigana na nduli Idi Amin urudie ili tuweze kusonga mbele tuwafikie hata hao tuliowakomboa kutoka katika utawala dhalimu wa kidikteta.

Ningelipenda wasomi wafanye kazi ya kutukomboa kwa elimu zao na wanasiasa watoe ushauri mzuri kwa mwenyekiti ili tuweze kusonga mbele, badala ya wasomi kufikiria wajilimbikizie nini na wanasiasa wamshauri vibaya mwenyekiti ambaye tunaamini katika mawazo yake.

Tutumie fursa iliyopo ya wasomi na wanasiasa kupiga hatua katika maendeleo badala ya kurudi nyuma, wananchi hawa ambao ni maskini waamini kutoka rohoni kwa viongozi wao kama ilivyokuwa zamani, tusirudi tukiamini kuwa sasa suala la kutoamini fikra za mwenyekiti ni muhimu kutokana na mawazo ya wanaomzunguka.

Wanangu, turudishe uzalendo, tuwaamini viongozi wetu nao waaminike kwetu, tufanye kazi kama tuna vita na Uganda nao wafanye kazi kama tuko vitani. Sasa tunajeshi kubwa kwa kila sekta, tunachoshindwa ni nini?

Swali hili kila mtu ajiulize; moyo ule wa kutoa uko wapi? Moyo ule wa kuamini katika fira za mwenyekiti wa chama uko wapi? Moyo ule wa kuamini kuwa tutashinda vita uko wapi? Moyo ule wa kupiga ndulu na vigelegele kuyapokea matatizo uko wapi? Nini hatima ya taifa ambalo hatuaminiani?

Tunashindwa nini sasa Watanzania sisi kufunga mikanda kukabiliana na changamoto za elimu na madarasa, umeme, maji, afya, miundombinu mizuri, makazi, viwanda vilivyokufa, huduma za uzazi, madini, uzuiaji wa jangwa na mwisho ikibeba yote hayo; maisha bora kwa kila Mtanzania  iliyokuwa kauli ya mwenyekiti wa chama? 

Wasalaamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.