*Ukristo ama Uislamu na serikali si tatizo katu
Naomba nichangie hapa kama Mtanzania -na si kama Mwislamu au Mkristo au mpagani. Mosi, ni kweli kwamba kitabu cha yule padri Mzungu, Dkt. John Sivalon kinaleta shida sana mawazoni mwa watu. Lakini turejee kwenye ukweli wa kisomi, kwamba huwezi kuhitimisha jambo zito kwa kutumia chanzo kimoja.
Hatuna maandiko mengine ya watu wasiokuwa na upande yanayothibitisha aliyosema padri huyu, kwamba nchini Tanzania kulikuwa ama kuna na upendeleo wa kielimu. Hakuna utafiti wowote unaothibitisha haya ila zipo tafiti nyingi zinaonyesha kwamba Tanzania iko nyuma mno kielimu.

Aidha, ni muhimu pia kuchunguza ili kujua kwamba Dkt. Sivalon alisema hivyo katika mazingira gani. Uongo unaweza kubadilishwa kuwa ukweli na ukweli kufanywa uongo. Je, tuna hakika na maneno ya huyu mwandishi padri? Kwani padri ni nani? Si ni binadamu tu? Najua ukitaka kuvutia upande mmoja itabidi aliyodai yapo lakini hali halisi inagoma. Nitaeleza. 

Pili, ingawa Mwalimu Julius Nyerere analaumiwa kwamba aliwabana Waislamu kielimu, lakini kiukweli kama si yeye, hali ya kielimu kwa Waislamu nchini ingekuwa mbaya zaidi. Tusisahau kuwa tulipopata Uhuru, serikali ya Mwingereza haikutuachia shule za kutosha kwa sababu ilikuwa serikali ya kiwizi tu. Wakristo na dini za waasia wakiwamo Mabohora, Waismailia na Wahindu walikuwa na shule, lakini Waislamu hawakuwa na shule. Nyerere alilazimika kukabiliana na ukweli huu.

Sasa tukumbuke pia kuwa wakoloni wa Ulaya walikuja Afrika Mashariki kwenye karne ya 19 wakati wakoloni wa Uarabuni walikuwapo tangu karne ya 13. Kwa miaka 600 Waarabu hawa hawakujenga shule hata moja; bali walijenga madrasa kwa ajili ya masomo ya dini, jambo lililokuwa heri lakini halikutosha. Shule za kwanza zilijengwa Tanganyika na Mjerumani zikiwa ni za darasa la kwanza hadi la nne kwa kutumia Kiswahili. Zanzibar zilijengwa sana sana na Mwingereza. Tafuta maana na historia ya maneno haya: (i) darasa/madarasa (ii) shule (iii) skuli. Jiulize yamekujaje?

Kimsingi, Nyerere ndiye aliyezitaifisha shule za wasiokuwa Waislamu ili na watoto wa Waislamu waende kusoma kwa sababu walikuwa wanakwepa kubadilishwa dini na ‘kulishwa’ nguruwe ingawa Wakristo wengine kama Wasabato hawali nguruwe hata kwa viboko.

Tatu, baada ya Uhuru, nchi yetu ikapiga hatua zaidi na tukaanza kujenga shule za msingi. Nyerere akajenga shule kwa juhudi kubwa zaidi kwenye mikoa iliyokuwa nyuma ambayo mingi ilikuwa ni ya pwani waliko Watanzania Waislamu wengi zaidi. Huko kwingine wananchi walifanya kazi kubwa kujijengea shule kwa bidii kubwa.  Haikutosha, Nyerere akaweka nafasi maalumu kwa makabila ambayo hayakuwa na watoto wengi shuleni. Ukweli ni kwamba waliofaidika zaidi ni makabila ya mikoa ya pwani (na kule Umasaini kwa kutaja machache tu), ambako shule ilikuwa kama kituo cha polisi kwao. Watanzania wengi tulikuwa washamba, tunakwepa shule.

Nyerere hakuishia hapo, bali akiwa anaongoza TANU na baadaye CCM, akajenga shule za ya Wazazi ya chama, nyingi kwenye mikoa ya pwani kama ile ya Bagamoyo na ya Vituka nje ya Dar es Salaam. Alipopata msaada kutoka Kuba, aliiachagua mikoa ya pwani pia kujengewa shule, na ndipo tukapata shule za sekondari kama Kibiti, Ruvu, n.k. Hata ile ya Waswiden ilijengwa Kibaha na ndiyo alikosoma kiongozi wetu wa sasa, Rais Jakaya Kikwete. Nyerere alifanya hivi kuwasaidia Watanzania wengi wakiwamo hao mnaowaita Waislamu ambao mimi nawaita Watanzania.

Ni kweli kwamba kwa wakati hakujenga sekondari nyingi, lakini kule kwingine kama Kilimanjaro waliamua kujenga shule za sekondari za binafsi kwa nguvu zao na ndiyo maana hadi leo wanazo nyingi. Serikali ya Nyerere ilitaifisha tu zilizokuwapo na ilipojenga, ilijenga kwenye mikoa yenye Waislamu wengi. Ndiyo ukweli huo ila watu hawataki kuutafuta. Rekodi zipo, tafuteni muone.

Nne, Serikali ya Tanzania haikuishia hapo. Wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, Waislamu walilalamika kuhusu suala la elimu. Zikafanyika juhudi nyingi ikiwamo kumweka Profesa Kighoma Ali Malima kwenye sehemu kama elimu. Juhudi hizi ziliifanya serikali kulifungia jarida maarufu la ‘Afrika’ lililokuwa likichapwa London, baada ya kueleza mambo kifitina.

Itakumbukwa kuwa Profesa Malima alianzisha awamu mbili za kwenda shule kwenye sekondari za serikali. Lengo lake likiwa kuongeza idadi ya watoto wanaokwenda sekondari wakiwamo wa Kiislamu na wa Kikristo pia. Wakati wa Malima pia Tanzania ikapata nafasi za masomo kwenye mataifa ya Kiislamu ya Misri, Algeria, Iran na Uturuki – maalumu kwa ajili ya Waislamu.

Marafiki zangu walikwenda huko na walinithibitishia kwamba hii ilikuwa maalumu kwa Waislamu tu. Hata hivyo, bado Waislamu waliendelea kwenda nchi nyingine zisizokuwa za Kiislamu bila tatizo. Huu ulikuwa msaada mkubwa na mkakati mzuri wa kuwasaidia Watanzania kupata elimu. Mmoja wa wahitimu hao leo ni mtaalamu wa kuheshimika nchini wa Teknohama akiwa kama mkurugenzi hapo alipo.

Tano, ikaja serikali ya Rais Benjamin Mkapa na yenyewe ikaweka rekodi ya kuwapa Waislamu majengo ya chuo kikuu. Leo hii kipo Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro kwa kutumia majengo ya serikali ya kilichokuwa Chuo cha Tanesco. Chuo hiki kinaongozwa na wasomi Waislamu Watanzania wanaoheshimika kama akina Profesa Juma Mikidadi aliyesomea udaktari wa falsafa kule alikosomea Nyerere, Edinburgh, Uskochi.

Serikali ya Rais Jakaya Kikwete pia imejenga shule nyingi za sekondari nchi nzima na sijasikia ubaguzi kwa upande wa mikoa yenye Waislamu wengi. JK pia amehakikisha Waislamu wanaongoza Wizara ya Elimu ili kuondoa malalamiko, na si kweli kwamba eti asiyekuwa Mwislamu akiwa waziri wa elimu, basi Waislamu wanashindwa kusoma. Hakuna ukweli hapa.

Najua kuna malalamiko mengi kuhusu shule na hata hospitali za misheni, lakini tuzitendee haki. Hizi ni za kuhudumia Watanzania wote, na ndiko binti mmoja wa rais wetu alikosomea pia (Kifungilo, Lushoto). Hata Mzee Yusuph Makamba hukiri kwamba alisomea kwenye shule za wamisheni na ndiyo maana anaimudu Biblia. Tuweni wakweli kwenye hili. Waislamu wanatibiwa kote huku, wanasoma kote, na ruzuku ndiyo mkombozi wa Mtanzania mnyonge anapohitaji huduma za afya.

WAISLAMU KWENYE VYEO NA ELIMU

Sita, labda, tuje kwenye hili moja: KWANINI HATUNA WAISLAMU WENGI KATIKA NAFASI ZA JUU SERIKALINI? Hili ni jambo la kweli, lakini inabidi tujiulize swali jingine zaidi: KWANINI KUNA MADAI KWAMBA WAISLAMU HAWAJASOMA?

Nianze na historia yetu. Waarabu walipokuja kwenye karne ya 13 walileta vitu kadhaa vikuu vikiwa viwili – dini nzuri ya Kiislamu na utamaduni wao wa kishenzi. Ndiyo, sijateleza ulimi wala mkono. Waarabu walileta utamaduni wa kishenzi. Utamaduni wa Kiarabu si dini ya Kiislamu na dini ya Kiislamu si utamaduni wa Kiarabu.  

Watanzania wengi wanachanganya haya mawili kwa kutokuwa na upeo. Tuulizeni tuliosafiri duniani, kuna Wazungu na Wachina Waislamu na kuna Waarabu Wakristo kama Wakoptiki wa Misri. Uislamu si Uarabu na Uarabu si Uislamu na kwa hakika Uislamu ndiyo uliopunguza ushenzi wa Waarabu (ujahiliya), na kuwapa utu na ustaarabu.

Tukumbuke pia, Uislamu ndiyo ulioongoza elimu duniani kwenye karne ya sita, saba na nane na hata vyuo vikuu vya kwanza duniani vilikuwa vya Waislamu, na haya majoho ya mahafali za leo yalianzishwa na Waislamu na si wazungu.

Nirejee kwenye rekodi. Taasisi ya kwanza ya kielimu kwa Waarabu duniani ilikuwa Ez-Zitouna ya Tunisia iliyoanzishwa mwaka 737, lakini kinachokubalika kama Chuo Kikuu cha kwanza duniani ni Al-Karaouine cha Moroko cha mwaka 859. Chuo Kikuu cha pili duniani kilikuwa Al-Azhar cha Misri mwaka 970 na cha tatu kilikuwa Nizamiyya cha Iraki mwaka 1065. Wazungu pamoja na kelele zao zote, chuo kikuu chao kwa kwanza ni Bologna cha Italia mwaka 1088 na baadaye mwaka 1096 kile cha Paris. Hakuna ubishi, Waislamu ndiyo waanzilishi wa vyuo vikuu duniani.

Saba, lakini si Waislamu wote hupenda elimu, kama ilivyo kwa dini nyingine pia. Ukienda kwenye nchi za Maghrebu (Afrika Kaskazini) kama Moroko, Algeria, Tunisia na Misri na zile za Mashariki ya Kati kuanzia na Uturuki, Syria, Irak, Lebanoni, na Yodani kidogo, hadi Iran kuna Waislamu wengi wenye elimu kubwa.

Hapa Marekani Waislamu wa mataifa haya wanaheshimika, mathalani, wahandisi na wataalamu mahiri wa teknohama hutoka Uturuki, Pakistan na India wakati madaktari mahiri hutoka Iran. Mataifa ya Pakistan na Iran ndiyo pekee yaliyomudu kuwa na wataalamu wake wenyewe wa nyuklia bila kusaidiwa na mataifa ya Ulaya na Marekani na wote walikuwa Waislamu, akiwamo Abdul Qadeer Khan wa Pakistani.

Aidha, mwanasayansi aliyesimamia urushaji wa satelaiti ya India ya kwanza mwaka 1980 ni Mwislamu Avul Abdul Kalam baadaye aliyekuwa Rais wa India mwaka 2002 hadi 2007. Ninachotaka kusema ni kwamba ukiondoa Waislamu walioko kwenye Ghuba ya Uarabuni, wengine wote ni wasomi wa uhakika. Sababu ni moja tu: UTAMADUNI.

Nane, hali ni tofauti sana kule Ghuba kwenye nchi za Saudia Arabia, Yemen, Kuwait, Oman, Qatar, Falme za Kiarabu na Baharein. Huko Ghuba watu hawataki shule. Tusiwasitiri sana na kuficha ukweli: Ghuba hawataki shule. Hawa watu wa Ghuba ndiyo walioleta utamaduni wao huu Afrika Mashariki kuanzia kule Somalia, shuka hadi Lamu, Malindi na Mombasa nchini Kenya, Njoo kwetu Tanzania anzia na Pangani hadi Kilwa na Mafia, teremka hadi Pemba iliyoko kaskazini mwa Msumbiji – kote huku kuna watu wenye utamaduni wa Ghuba wa kukataa shule. 

Tusifichane ukweli, maeneo haya watu hawataki shule. Hili liko wazi. Kwa kuwa Waarabu wa Ghuba ndiyo walioleta pia Uislamu, basi watu hujumuisha kwa pamoja tatizo la kukosa elimu na hii dini nzuri ya Uislamu. Narudia, utamaduni wa kukataa shule ni wa Waarabu wa Ghuba si Waislamu hapa duniani. Tatizo letu Tanzania ni kwamba Waislamu wengi (si wote) wamechukua utamaduni wa kimwinyi-mwinyi wa Ghuba wa kuzikimbia shule kana kwamba ndiyo ujanja. Hiki ndiyo chanzo cha malalamiko yote haya – hakuna cha uonevu wala nini.

Saudia watu ni vilaza watupu kiasi kwamba kuna Wamisri milioni moja na zaidi wanaofanya kazi za kitaalamu. Kila taifa la Ghuba isipokuwa Yemen na Oman, lina wageni wengi zaidi nchini mwake kuliko wenyeji kwa sababu wananchi wao ni vilaza; hawataki shule. Yemen na Oman hawana mafuta wala gesi asilia, yaani ni masikini na ndiyo maana hakuna wageni wengi. Hata hivyo, ukienda Oman kuna Watanzania sana (hasa wenyeji wa Zanzibar), laki sita na ushei na wao pia shule hamna kitu; wanaiga uvivu wa wenyeji wao.

Tisa, hivyo basi, Waislamu wa pwani ya Tanzania kama wenzao wote wa Somalia, Lamu, Malindi, Mombasa, Pemba, Unguja, Mafia, Kilwa, Lindi na Pemba ya Msumbiji, wana utamaduni wa Waarabu wa Ghuba wa kugomea shule, tofauti na Waislamu wa Tanzania walioko Machame na Usangi mkoani Kilimanjaro, au Usukumani, au kule Bukoba, na hata wale wa Uganda (kabila la Baganda), wao wanapenda shule.

Maeneo yote waliyokaa Waarabu kuanzia Bagamoyo, halafu fuata ile barabara ya watumwa hadi Kondoa, nenda hadi Tabora, fika hadi Ujiji, ingia Kongo mashariki, kote huko shule si mali kitu. Tatizo hapa si Uislamu bali ni utamaduni wa Uarabu wa Ghuba. Anayebisha hongera zake.

Kumi, tafiti tatu ninazozijua, moja ya Ilana Kessler wa Chuo Kikuu cha Georgetown cha Marekani ya mwaka 2005, na ile ya Erasmus Kaijage wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ya mwaka 1999, zinaonyesha kwamba wanafunzi wa shahada ya kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliokuwa Waislamu ni kati ya asilimia 14 na 15 tu ya wanafunzi wote.

Aidha, Baraza la Udhamini la Waislamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUMT), liliwahi kutoa taarifa yake kwamba kati ya mwaka 1986 na 1990, kwa wanafunzi walioingia chuoni hapo kusoma shahada ya kwanza, Waislamu walikuwa asilimia 13 tu. Hiki ni kiasi kidogo mno lakini ni kidogo cha kiasi gani cha Waislamu nchini? Lazima tujue hili nalo pia, hata kwa makadirio tu.

Kumi na Moja, sasa turudi kwenye jingine. Nyerere aliamua tuachane na sensa ya kupekua dini za watu kwa sababu nzuri kabisa – alitaka Watanzania tusitambuane kwa dini zetu (na makabila pia). Hivyo, ili kuweka usawa tukaanzisha msemo huu: Tanzania sisi nusu ni Waislamu na nusu ni Wakristo. Huu ni msemo tu na hauna usahihi. Aidha, hata kama sensa ya zamani ilionyesha kwamba Waislamu ama Wakristo au wapagani ndiyo wengi, haina maana yoyote leo wakati taifa letu lina watu milioni 45 hivi. Tulipata uhuru tukiwa milioni 12 na baadaye Zanzibar ikaongeza laki tatu. Watanzania hatukuwa na kelele za asilimia ngapi ni dini hii na ile. Leo zimerudi. Inakera sana!

Kwa mujibu wa taarifa kadhaa za kitafiti (si mimi), Waislamu nchini Tanzania ni theluthi moja ya wananchi wote. Aidha, kwa bahati ama kwa mpangilio, rais wetu wa sasa, Mheshimiwa Kikwete alipoteua mawaziri Novemba 2010 aliweka theluthi moja Waislamu, na hivyo hivyo kwa manaibu. Wote tunajua. Hali kadhalika, alipoteua mawaziri na manaibu wao hii juzi, aliweka theluthi moja Waislamu kwenye uwaziri na pia kwenye unaibu.  

Alipoteua Tume ya Kupitia Katiba, kwa wajumbe wa Bara aliweka pia theluthi moja yake Waislamu. Iko wazi. Rais Kikwete, nijuavyo mimi, anajaribu kwa kila hali kuliangalia hili suala la kelele za udini ili asiiharibu nchi yetu. Hatopenda kukumbwa na malalamiko akishaondoka kwani na yeye ni binadamu kama sisi. Anakuwa mwangalifu sana hata kama kuna wakati anateleza kibinadamu. Je, hesabu zake zina maana gani? Nina hakika anajua anachokifanya na kamwe hawezi kuwaonea Waislamu ambao ni Watanzania kama sisi wote. Hawezi kufanya uonevu.

Sasa, zifuatazo ni taarifa zinazoonyesha idadi ya waumini wa Kiislamu nchini Tanzania:

(a) Taasisi ya Kiislamu ya Asoon ya Iran ambayo inatunza rekodi za idadi ya Waislamu katika nchi zote duniani inadai Waislamu nchini Tanzania ni asilimia 35 ya wakazi wote;

(b) Taasisi ya utafiti iitwayo Pew Research Centre ya Marekani iliyofanya utafiti wa idadi ya Waislamu duniani, inadai kuwa nchini Waislamu ni kati ya asilimia 30 ya wakazi wote;

(c) Ofisi ya Demokrasia, Haki za Binadamu na Uhuru ya Serikali ya Marekani inasema katika utafiti wake, asilimia 35 ya wakazi wa Tanzania ni Waislamu.

Hizi si takwimu pekee na sijaweka za Wakristo kwa sababu sitafuti ushindani na siamini kama idadi ina maana yoyote Tanzania, na hizi kelele za idadi hazitufai; ni ujinga lakini anayezitaka aanzie na hizo hapo juu.

Aidha, mnamo Aprili 2011, mwanazuoni mmoja wa Tanzania, Mohamed Said, alialikwa kuhudhuria warsha ya Mustakabali wa Demokrasia Afrika Mashariki iliyofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Iowa, nchini Marekani. Akadai kwamba Waislamu ni asilimia 70 ya Watanzania wote, lakini akashindwa kujibu maswali ya ni wapi wanakaa Watanzania hao kiasi kwamba hawaonekani kwa wingi huo.

Mwaka 1994 pia kwenye jarida la kitaaluma la Nordic Journal of African Studies, mwanazuoni mwingine aliyekuwa Chuo Kikuu cha Uppsala cha Uswidi, Abdulaziz Lodhi, alidai katika makala yake ya “Waislamu Afrika Mashariki: Zamani na Leo,” kwamba Waislamu nchini Tanzania ni asilimia 60. Hakueleza wako wapi. Nirudie: kelele za idadi ya waumini ndani ya Tanzania ni ujinga. Lodhi alidokeza pia kuwa Waislamu nchini Kenya ni asilimia 25 ya wakazi wote; Uganda ni 45 na Msumbiji ni asilimia 40. Takwimu hizi zinapingana na nyingine zote zilizopo duniani zikiwamo za taasisi za Kiislamu.

Kumi na Mbili, kwa nini idadi inakuwa muhimu hapa achilia mbali kelele ninazozipinga? Ni kwa sababu tunataka kuielewa hii asilimia ndogo ya wasomi wa Kiislamu hapa Tanzania imekaaje? Je, leo hali ni nzuri zaidi kwa sababu tuna chuo kikuu cha Kiislamu na vyuo vikuu ni vingi zaidi? Tunahitaji utafiti ili tujue Waislamu wengine wameishia wapi. Lakini ile nadharia yangu ya UTAMADUNI WA WAARABU WA GHUBA si ya kusahau.

Kiukweli, hakuna mfumo wa kumfanyizia Mtanzania Mwislamu. Hakuna ushahidi wala nia. Mimi nimekulia na kusomea Dar es Salaam kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita, na JKT kabisa. Waislamu wote marafiki zangu waliokuwa wakali darasani waliendelea na elimu ya juu. Kwenye shule ya msingi yetu tulikuwa watoto wanne machachari, mimi, Waziri, Salum na Izihaki, na wote tulifaulu.

Nilipokwenda Azania mwaka mmoja nyuma yetu palikuwa na kijana Mwislamu wa Pemba aliyeongoza Tanzania nzima mwaka wao na akafanya hivyo tena alipokuwa Tambaza kidato cha sita. Baadaye alikwenda Ulaya kusomea uhandisi kwa nafasi iliyotoka serikalini; hakunyimwa nafasi yoyote. Hao wanaonyimwa wako wapi? Tulipomaliza kidato cha sita aliyeongoza Tanzania nzima alikuwa Mwislamu, Karim, na alikwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Uchache wa Waislamu kwenye vyeo unaweza ukachangiwa na idadi ya kweli ya Waislamu nchini, pamoja na idadi ya wanaofika kwenye elimu ya juu kulinganisha na wasiokuwa Waislamu. Tanzania, tukiri, kwamba tumeathirika na utamaduni wa Waarabu wa Ghuba, hasa huku pwani ambako kwa bahati ndiko kwenye Watanzania wengi Waislamu. Hakuna cha kushangaa bali huu ndiyo ukweli. Mambo ya vyeo ni matokeo tu lakini tuna uwezo wa kuleta mabadiliko.

HITIMISHO NA OMBI

Tufanye juhudi kuwakomboa wale wote walio nyuma kielimu Tanzania. Wako wengi – kwa dini na makabila mengi tu – lakini wote ni Watanzania. Walio nyuma wasiseme eti kuna uonevu, bali waondoe kilichowakwamisha. Sasa Wakurya waliokuwa wanakimbilia jeshi wanaacha shule nao wamlaumu nani hivi leo?  

Hatuwezi kulinganisha utamaduni wa elimu wa watu wote nchini, mathalani, watu wa Kilwa, Mafia, Rufiji na Pangani na watu wa Moshi, Kyela, au mkoani Kagera. Sijasema kwamba hakuna wasomi huko, la hasha wapo, ila ni wachache kulinganisha na wenzao na tafiti zipo. Mathalani, watoto waliopata “A” kwenye somo la dini ya Kiislamu kwenye mtihani wa kidato cha sita uliopita ni Rahma A. Mushi na Mabina M. Mabina. Kwa nini? Ukweli unauma, lakini ukweli ni dawa ya matatizo; huwezi kutibu malaria kwa dawa ya kichocho.

Watanzania tuweni wakweli. Mwenyezi Mungu hapendi waongo. Kwa nini shule za binafsi hazina pia Waislamu wengi? Nani anawazuia Waislamu kujenga shule Tanzania hivi leo? Je, kama kweli unataka mtoto wako apate elimu safi, na amekosa nafasi ya shule ya serikali, utampeleka wapi? Pale Kinondoni Muslim ambako wanafunzi huanguka mitihani? Tuseme ukweli.

Naamini tunao uwezo wa kuyatatua matatizo yetu ya kihistoria na kitamaduni na si kukaa chini kupanga vurugu kwa madai ya kuonewa. Waislamu wa Saudi Arabia hawajasoma licha ya utajiri wao. Je, hao nao waziri wao wa elimu na baraza la mitihani wametoka Tanzania? Mbona Waislamu wa Uturuki, India, Pakistan, Tunisia, Moroko, Misri, Senegal na Afrika Magharibi yote wana elimu?

Tutafute chanzo cha kweli cha tatizo, halafu wote tushirikiane kulitatua; wote kabisa. Rais Mwinyi husema kila siku: Waislamu pelekeni watoto shule, acheni kulalamika. Waislamu wa kwingineko duniani ni wasomi na walioko Tanzania wanaweza kuwa wasomi kama watakavyo. Tukumbuke pia, kama taifa, bado tuko nyuma mno kielimu na tunahitaji kuruka na ungo wakati wenzetu wanatambaa!

Wabillahi Tawfyq

Mwandishi wa makala haya, Mobhare Matinyi, aliwahi kuwa mhariri mkuu hapa Tanzania lakini kwa sasa ni mkufunzi kwenye Taasisi ya Mambo ya Nje ya Marekani, jijini Washington DC. Ana shahada tatu za uzamili (Masters) katika mawasiliano ya kisiasa, masuala ya mikakati (strategic studies), na uhusiano wa kimataifa. Anapatikana matinyi@hotmail.com.

3147 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!