Ije Jubilee nyingine ya malkia tushibe

Si mapumziko hata kidogo, maana ni sikukuu lakini waliofanya kazi wametoka na vinono. Wengi wataendelea kumwombea Mtukufu Malkia Elizabeth II adumu na serikali iendelee kuridhia maadhimisho ya sherehe zake.
Basi tangu wiki iliyopita imekuwa mfululizo wa shangwe, nderemo, vifijo na kila aina ya bashasha hapa Uingereza wakati Mtukufu Malkia Elizabeth II alipoadhimisha miaka 60 tangu ashike hatamu za uongozi taifa hili na mengineyo kama Australia, New Zealand kwa kutaja machache.

Wameiita Diamond Jubilee na imeadhimishwa kila mahali, kuanzia kwenye Kasri ya Buckingham na Kasri ya Windsor anakokaa, kanisani, shuleni, mitaani na hata nyumbani.

Utawaambia nini watoto kwamba eti haiwahusu kwa vile sisi ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wameshiba vya kutosha kuhusu ufalme wa Uingereza na jinsi ilivyo na himaya nyingi? Utamwambia nini kijana wa Kitanzania aache kumpenda Malkia wakati ndiye aliyemwezesha mkono kwenda kinywani, kwa kuuza matunda yake kwa wingi kwa shule zilizokuwa zinaadhimisha Jubilee Ijumaa iliyopita?

Utambadilisha vipi mawazo mwanamama wa Kibongo aliyefanikiwa kupata tenda ya kuwasuka watoto wa shule bila kujali asili yao, mradi tu apachike rangi za kibuluu, nyeupe na nyekundu kwenye nywele zao?

Dada mmoja alipata tenda, bahati mbaya akawa mwenyewe na mdogo wake huku wanafunzi wakiwa wengi – jasho lilimtoka nakwambia, ikawa analifuta kwa khanga japokuwa ubaridi ulikuwa wa haja, akiangalia vichwa bado vingi vya kusuka, anacheka lakini vidole vinamuuma, basi anaendelea tu akijua mwenyewe alicholipwa.

Wikiendi hii ambayo wanaiita ‘bank holiday’, yaani wanapumzika Jumamosi hadi leo Jumanne wanakula vya Malkia, huyu dada aliniambia hafanyi kazi ya mtu.

Nikamuuliza kulikoni, akaniambia; “mgodi umetema!” Maana mwenyewe hakuamini alipojaza vocha na kuandikiwa hundi za mipauni kibao, akajiona kama vile anaiba, lakini ndiyo uthubutu na ujasiri aliokuwa akizungumzia mzee wa uwazi na ukweli jamani.

Jubilee hii haiendi tupu, ni mtu na akili zako kichwani tu; unabuni kitu cha kufanya kwenye jamii unayoishi au taasisi unayoijua, na wao wanakifikiria kitakavyoipamba Jubilee, halafu wanakukubalia – unaingiza paundi tu mwanangu! Nawajua vijana wenye ushirikiano wao, walioanzisha wazo wakiwa kijiweni tu kuhusu cha kufanya kwenye Jubilee hii.

Walitoka na wazo hili; kwamba Malkia Elizabeth II amekuwa kiongozi bora kwa Uingereza na ni wa kupigiwa mfano katika bara lote hili, hadi Amerika na Afrika. Kwa hiyo wakabuni aina ya nyimbo, nasema aina maana ni beti mbili tu, tena fupi, wameenda kuziimbisha kwenye shule mbalimbali jimboni Berkshire, wakubwa wamezikubali na kuona ni kudhihirisha utandawazi wa ‘Bibi’. Ngawira zimewatoka na vijana wetu wakashiba.

Watu wanaojituma wamefaidi siku hizi kubwa za Malkia Elizabeth II, maana hata kazini wamelipwa mara mbili mbili – yaani kama malipo yalikuwa paundi sita kwa saa, basi mtu analipwa paundi 12 kwa saa hiyo hiyo moja. Na hadithi hiyo ni ya siku nne – Jumamosi hadi Jumanne leo unavyosoma makala haya!

Wengine walianza Ijumaa, kwa sababu shule za msingi zilifungwa Ijumaa, ilibidi nao wafanye maadhimisho shuleni – ndiyo wengi walioimba zile nyimbo ‘zetu’ na kusukwa na dada ‘yetu’.

Hapakuwa na kuvaa sare shuleni Ijumaa. Wazazi tuliandikiwa barua kabisa kwamba tutafute nguo zenye rangi ya bendera ya Union Jack – nyeupe, nyekundu na kibuluu. Wapo wasichana waliovaa kama malkia na hadi krauni kichwani kabisa, rinda refu jeupe na kizibao cha buluu kilichochangayika na nyekundu.

Maduka makubwa yameshusha hata bei kwa ajili ya Jubilee ya Malkia, wanasema asilimia 20 au 25 hadi 50 inapunguzwa ili nguo ziishe zivaliwe kumpendeza Malkia, potelea mbali hata kama hawatapata faida! Na mitaa inafungwa ili watu washerehekee kwa kupeperusha bendera halafu wakae wale na kunywa sharubati.

Moja ya vyakula vikubwa hapa ni mikate, piga ua lazima, keki muhimu sana na pasta moto na mapaja au miguu ya kuku kabla ya kupeperusha tena bendera kwa heshima ya huyo ‘Bibi’.

Akili ya kuambiwa changanya na ya kwako na ukiwa Roma fanya kama Warumi wafanyavyo. Kwa hiyo walioitikia mwito wa kuzipamba siku hizi muhimu za Jubilee wamepata matunda yake, wanakula na watashiba. Alamsiki.

[email protected]