Naweza kumpenda au kumchukia sana Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, lakini hata iweje sitajizuia kumuunga mkono mtu yeyote akifanya jambo jema au lenye tija kwa taifa.

 

Siku chache zilizopita, Lowassa aliongoza harambee iliyokusanya Sh. milioni 530 kutoka kwa wadau wa maendeleo ya elimu – fedha ambazo Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho yeye mwenyewe ni mwanachama wake, kilichangia Sh. milioni 20.

 

Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Kipawa, Ilala Dar es Salaam, Bonnah Kaluwa (CCM), Lowassa binafsi alichangia Sh. milioni 10 huku watu wengine na taasisi mbalimbali zikijitokeza ili kumuunga mkono.

 

 

Sisemi kuwa viongozi wengine wa kisiasa hawafanyi chochote kushughulikia maendeleo ya elimu nchini, lakini hakuna ubishi kwamba Lowassa amekuwa mstari wa mbele kufanya hivyo.

 

Inawezekana kwamba hatimaye taasisi mbalimbali zinapotafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za ibada, madarasa ya shule za msingi, sekondari na vyuo nchini, zimekuwa zikimualika mara nyingi zaidi ikilinganishwa na viongozi wengine, lakini hazifanyi hivyo kwa bahati mbaya ila kwa sababu zinatambua mwitikio wake anapoombwa kusimamia harambee zake.

 

Ndiyo maana amekwenda Mwanza, Kigoma, Singida, Morogoro, Dar es Salaam na mikoa mingine huku ikielezwa kuwa ratiba yake siku zote huwa imejaa kwa miezi mingi mbele kutokana na mialiko anayopewa kutoka maeneo tofauti nchini.

 

Mahitaji ya elimu kwa dunia ya sasa ni makubwa kuliko ilivyokuwa miaka yote iliyopita. Pia idadi ya wanaohitaji kusoma kuanzia shule za chekechea, msingi, sekondari, vyuo vya kati hadi taasisi za elimu ya juu inaongezeka kwa kasi kila mwaka.

 

Najua, kwa mfano kuwa wakati Lowassa alipokuwa mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika miaka ya 1970 na hata alipokwenda kusoma Shahada ya Juu ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Bath nchini Uingereza mwanzoni mwa miaka ya 1980, mwamko wa elimu nchini ulikuwa chini.

 

Baadhi ya makabila kutoka pwani hadi bara yalikuwa hayasomeshi kabisa watoto wa kike. Yalikuwa yakidai kwamba kuwasomesha hakuna faida yoyote, badala yake yaliwachukulia kuwa mitaji ya kuingizia fedha kupitia mahari wanapofikia umri wa kuposwa na kuolewa.

 

Hata wavulana walipohitimu elimu ya msingi ilikuwa ikielezwa kuwa “amemaliza shule”, hivyo kuingia kidato cha kwanza haikuonekana muhimu, bali ilikuwa ni kupunguza nguvukazi nyumbani. Ndiyo maana kuna wazazi, hasa maeneo ya vijijini walikuwa wakiziuza nafasi za watoto wao wanapofaulu kwenda sekondari kwa “watu wa mijini”.

 

Kusoma katika kipindi hicho kulichukuliwa kama anasa, kupoteza muda kwa jambo lisilokuwa muhimu na wazazi wengine walikosana na watoto wao waliotaka kuendelea na masomo.

 

Shule za kulipia (private schools) katika ngazi hiyo ya elimu zilikuwa chache kiasi cha mtu kuweza hata kuzihesabu. Shule za serikali zilifahamika idadi yake huku baadhi ya mikoa kadhaa ikiwa na sekondari moja.

 

Waliofika au kuishi katika mikoa hiyo wanajua Rukwa ilikuwa na Kantalamba Sekondari, Kigoma (Kigoma Sekondari) na Shinyanga ikiwa na Shinyanga Sekondari, lakini leo kuna shule angalau moja ya sekondari kwa kila kata kuanzia mijini hadi vijijini.

 

Katika kipindi hicho pia, Jiji la Dar es Salaam lenye idadi kubwa zaidi ya wanafunzi kuliko mikoa mingine, lilikuwa na shule nane za sekondari za serikali ambazo ni Kibasila, Pugu, Azania, Jangwani, Zanaki, Tambaza, Kisutu na Forodhani.

 

Tofauti na wakati huo, mahitaji ya shule za sekondari za serikali hivi leo ni makubwa mno, lakini zilizopo katika ujumla wake zote hazitoshi, hivyo kuongeza kwa kiwango kikubwa zaidi mahitaji yake kutoka kwa watu binafsi, taasisi za umma, mashirika au madhehebu ya dini na kadhalika.

 

Ingawa pia zinaongezeka kwa kasi kila mwaka, lakini bado hazitoshi kwa sababu wanafunzi wanaohitimu darasa la saba nao wanakadiriwa kuongezeka kwa wastani wa angalau asilimia tano hadi 10, hivyo hata iweje haziwezi kuwatosheleza.

 

Kinachofanyika ni kuzidi kuongeza mikondo kuanzia shule za msingi hadi sekondari na kuingia darasani kwa kupishana, halafu madarasa ya vyuo au taasisi za elimu ya juu nayo yakizidi kujaa.

 

Nimesema kwamba Lowassa alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika miaka ya 1970, kipindi ambacho mbali na kuwapo shule chache mno za sekondari, lakini hata hicho nacho kilikuwa pekee cha ngazi hiyo ya elimu nchini, halafu wanafunzi wake walikuwa wachache.

 

Katika msingi huo, juhudi zinazofanywa kwa nguvu kubwa na Waziri Mkuu huyo wa zamani za kuhamasisha au kuongoza harambee za kuchangia maendeleo ya elimu, hazina budi sasa ziungwe mkono kwa namna zote na kila Mtanzania.

 

Naamini kwamba wote wanaomwalika kuwaongozea harambee zao za kuchangia maendeleo ya elimu, naye akiitikia mialiko yao bila kulalamika, akasafiri kila mahali kuifanya kazi hiyo; hakutokani na sababu zozote za kisiasa, kumjenga kwa namna moja au nyingine wala hawalengi kumpandisha chati ili afikie malengo yake ya kisiasa.

 

 

Hawafanyi hivyo ili awatumie kuwa mbeleko yake kwa ajili ya jambo lolote. Ndiyo maana hawatoki eneo moja wala wenye mwelekeo wa aina moja, badala yake wanamwalika kwa sababu wameridhika naye kwamba akiongoza hafla za kukusanya michango ya elimu, malengo yaliyokusudiwa mara nyingi hufikiwa.

 

Wanamwalika kama wanashindana kwa vile wamegundua kwamba hana ubaguzi wa kikanda, kidini au kikabila, isipokuwa ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa ambaye akitumika anaweza kuingiza fedha nyingi.

 

Wamegundua kuwa hata akialikwa mara nyingi halalamiki, hakwepi wala hatumi mwakilishi. Yeye mwenyewe huibeba kazi hiyo wakati wowote na mahali popote iwe kanisani asubuhi, ukumbini usiku wa manane na mahali pengine.

 

Nimekuwa nikifuatilia kwa muda mrefu harambee mbalimbali za kuchangia elimu nchini na kugundua kwamba Lowassa amekuwa akialikwa mara nyingi zaidi. Anaalikwa hivyo kwa vile hana “longolongo”.

 

Nimesema kuwa inawezekana nampenda mno mbunge huyo wa Monduli, na pia ninaweza kumchukia kupindukia kwa sababu hakuna binadamu anayependwa na watu wote duniani, lakini kwa juhudi anazofanya katika kuhangaikia elimu nchini, hakika siwezi kumkasirikia hata iweje.

 

Ndiyo maana naomba kila Mtanzania popote alipo atumie akili yake yote, nafasi zake zote na uwezo wote alionao kimapato, kitaaluma na hata vinginevyo ili kuziunga mkono juhudi zinazofanywa na Lowassa, aliyeonyesha wazi kwamba anaihangaikia Tanzania kielimu kwa sababu anaitakia kheri.

 

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0762 633 244

1124 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!