Hisia tupu hazitusaidii kuzikabili changamoto zenye uhalisia mwingi. Kiendeleacho Afrika Kusini ni matokeo ya muda mrefu wa kupandwa kwa saratani ya ubaguzi wa kijamii, kisiasa na kiuchumi.
 Haiyumkiniki ni kile kitarajiwacho baada ya jamii na tawala kujisahau, wakatokea kudunisha baadhi ya watu na kusimika unyonyaji, dhuluma iliyotopea na kusakafia ubeberu kinyume cha thamani kuu ya utu.


 Ninaamini bado wengi wa ndugu zetu wa Afrika Kusini hawajasahau machungu ya uonevu. Waafrika Kusini kamwe hawajasahau mchango wa ndugu zao na majirani zao waliokuwa bega kwa bega katika kipindi kile kibaya zaidi cha ubaguzi wa kila nyanja wa dhahiri shahiri.
Ndugu zao hao walitoa uhai wao na kuzitumia rasilimali zao chache wakijifunga mkaja kuhakikisha ukombozi wa mtu mweusi na wananchi wote wa kusini si tu unapatikana bali unaendelea kudumu daima.


Waafrika wenzao walihakikisha harakati za wanyonge hao zinazaa matunda na kuuzika ubaguzi wa rangi kinyume cha ubinadamu na kutokomeza uimla, hatimaye kufikia tamati mikononi mwa Nelson Mandela na kuliasisi taifa huru chini ya wazawa.
Leo hii baadhi ya Waafrika Kusini wanaweza kueleweka vibaya machoni mwa wenzao, kikubwa kwa kuhisiwa kuzisahau tunu za mtu huru, yote ni kwa sababu ya vijana siwezi kuwaita wachache, kuingia mitaani kuhanikiza vurugu, mapanga, mawe mikononi na ngumi juu tayari kuwakabili Waafrika wenzao na wanyonge wengine wahamiaji na hata wakimbizi kutoka Bara Asia.


Vijana hawa hawataki kukumbuka kuwa hao wanaowakabili ni wanyonge wenzao waliozikimbia nchi zao kutokana na vurugu, uasi na kikubwa zaidi sababu ya chumi dhaifu za nchi watokazo.
Hii ni sawasawa na kilichoshuhudiwa wiki hii cha wahuni watumiao mgongo wa dini kudhuru wengine, wakiwakamata raia wa Ethiopia nchini Libya na kuwatoa uhai hadharani. Hebu jaribu kufunga macho na kufikiria kuwa ni wewe uliyekamatwa ukijaribu kuikimbia nchi yako kuelekea mataifa yenye nafuu kiuchumi, unaangukia mikononi mwa binadamu hawa katili na duni kabisa kufikia kuhitimishwa uhai wako huku shingo yako ikiwa halali yao; inachusha, inauma, inahuzunisha na kusikitisha!


Tukirudi kwa vijana hawa wa Afrika Kusini utamaizi wengi wao ni wa umri wa kati ya miaka 20 na 30, wakiwa wachache wa elimu, malezi duni ya mitaani kutoka vitongoji maskini kabisa huku wakikosa kabisa ama kuwa na ajira chache.
Ukiwaangalia vema vijana hawa wanawaka hasira na chuki, vijana hawa hawana cha kupoteza hata kidogo, kifupi wamekata tamaa na wala hawana haja ya kuikumbuka thamani kuu ya utu na uhai wa mwanadamu.


Haya ndiyo matokeo hasi ya kupandwa kwa mbegu ya ubaguzi. Wafanya vurugu hawa wanaamini kwa dhati ya mioyo yao kuwa ukosefu wao wa ajira ni kutokana na kuwapo kwa wahamiaji na wakimbizi nchini mwao.
Vijana hawa hawataki kukubali sababu nyingine zozote za chanzo cha uduni wa maisha yao, pia hawataki kukumbuka kuwa kilichopandwa na makaburu kinaendelea kuchomoza wakati huu. Kwao wao wanaamini kuwa nafasi na fursa za kiuchumi zimehodhiwa na ndugu zao hao wanyonge kutoka nchi za Kiafrika na Bara Asia.


Julius Malema alipata kuwakebehi baadhi ya viongozi wenye fikra za kibubusa kwa kusema kuwa ataendelea kuuona mchango na kumshukuru sana Nelson Mandela kwa kuwafikisha hapo walipo, ila anahitaji kuwaona kina Nelson Mandela wengi wapya ili kuulinda uhuru wao na kuuboresha zaidi kivitendo.
Hakika inajulikana Afrika iko matatizoni katika kuulinda vyema uhuru, kuuboresha zaidi na kuutafsiri kwa vitendo ili uwe na tija isiyo na mawaa. Afrika inaendelea kuwahitaji viongozi adhimu wenye maono makuu, wanademokrasia kindakindaki, viongozi wanaume kwa wanawake wenye kufanya uamuzi mgumu wenye usahihi mwingi wa dhati ya kuyaharakisha maendeleo ya kweli.


Nimetangulia kusema kuwa inahitajika utulivu wa hali ya juu kuwatafsiri vijana hawa, pamoja na upungufu wao niliyoyabainisha vijana hawa wamevizwa fikra na kupigana na adui asiyehusika!
Ukimsikiliza Mfalme Goodwill Zwelithini naye yuko katika hamaniko, changamoto ni nyingi zimemzidi kufikia kuonekana anawaungana mkono wafanya vurugu hawa mitaani. Ninaamini tamko la kiongozi huyu wa Kwa Zulu Natal halikuhusisha dhidi ya wahamiaji wote, labda wale waishio bila ya kibali na kinyume cha sheria.


Jiji la Durban na miji mengine hakika lina maendeleo makubwa ya vitu na ya watu wachache, watu ndani ya vikundi vilevile vikiiendeleza enzi, vikundi hivyo vya watu na familia chache vyenye meno makali ya chuma vinavyofaidika zaidi na uchumi wa nchi kipekee zaidi, vikiwa na ada ya kung’oa meno ya asili ya wasakatonge na kuwabakiza vibogoyo na kuwaacha wengine na meno ya plastiki, ndiyo moja ya vyanzo vya matatizo haya yanayoonekana sasa.
Ni hivi majuzi Waafrika Kusini wakiungana na viongozi wa serikali, kiroho na asasi za kiraia kupinga vurugu na ubaguzi huu uliotopea, kikatokea kioja cha mwaka. Wale vijana wanaofanya vurugu hawakutaka hata kusubiri maandamano hayo ya mshikamano na amani, waliingia barabarani na kuwashambulia wahamiaji na hata wenzao wanaoandamana.


Hapa ndipo unapotanabahi ukubwa wa tatizo na ndiko wanadamu tunapojisahau kuwa upandapo mbegu ya chuki huchukua muda mrefu kumea pengine hata isikuathiri binafsi bali vizazi. Inapopandwa mbegu ya ubaguzi wa aina yoyote na yeyote, mfano wa haya yaendeleayo Afrika Kusini huwa ni sahali.


 Tanzania, Taifa la kipekee, hatuna budi kujifunza na kuwa wanafunzi bora kutokana na makosa ya ndugu zetu wa Afrika Kusini, tukiwa Taifa linaloongezeka sana kwa idadi hususani majiji makuu ni lazima twende mbele zaidi na kuendelea kuziishi fikra adhimu za uhuru wa kweli kwa wote na kila mmoja wetu; uhuru ulio na ukweli mtupu dhidi ya wale maadui ujinga, umaskini na maradhi.


 Ni lazima tena tuvipambanue vyema vipaumbele vyetu viendane na uhalisia bila ukakasi, tukiendelea kuichonga barabara ya maendeleo kwa kasi ili leo na miaka mia mbele yasitokee makundi mithili ya wenzetu kufikia kutupa maneno ya kuwalaumu, ilhali tunaangalia tulipoangukia na si pale tulipojikwaa.


Mwisho nimalizie kwa kukumbusha zile imani adhimu, imani zilizo rahisi kutamka na nzito na ngumu kivitendo kwa watu  wenye kupenda majibu rahisi kwa maswali magumu. Hakika, binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

2157 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!