Yanga Princes waitazame Simba Queens

NA MWANDISHI WETU 

Jumamosi ya wiki iliyopita Timu ya Yanga Princes ilicheza mechi yao ya saba dhidi ya mtani wao Simba Queens. Kilichobadilika ni idadi ya mabao waliyofungwa katika ‘derby’ zilizopita ukiachana na ile ya Desemba 12, 2020 katika Uwanja wa Mo Arena waliyopata sare tasa. Jumamosi hiyo walifungwa mabao 4-1.

Yanga Princes wanapotea katika vitu vingi dhidi ya mtani wao. Lakini kubwa ni uwekezaji. Tofauti yao imeanzia hapa. Simba Queens wamewekeza kweli katika mpira wa akina mama. Yanga Princes wamewekeza kidogo.

Si kitu kibaya kuiga kitu kizuri unachokiona kwa mwenzako. Simba Queens wamewekeza kwa kufanya usajili wa wachezaji nyota wa ndani ya nchi na nje kwa baadhi ya nchi.

Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’ ambaye hivi sasa yupo Morocco. Mawete na Ruth Kipoyi wote wametimkia Uturuki na walikuwa nyota wa Simba Queens.

Njia pekee ya kuifanya Yanga Princess kuwa washindani wa kweli dhidi ya watani wao ni kufanya wanachokifanya wenzao sokoni. 

Uwekezaji uliofanywa katika timu kubwa ya wanaume ulitakiwa kufanyika angalau kwa asilimia 50 katika timu ya akina mama.

Kuna ‘gape’ kubwa baina ya Yanga ya wanaume na Yanga ya wanawake. Timu moja zinazotumia jina na jezi moja, lakini nje na ndani ya uwanja ni timu mbili tofauti zinazoishi katika mazingira tofauti.

Ni wakati wa Mhandisi Hersi Said kuanza kuitazama timu hii kwa jicho la karibu. Yanga Princes wana mwalimu mwenye mvuto mkubwa katika soka la wanawake hapa nchini, Edna Lema, lakini anaangushwa na vitendea kazi kazini. 

Kama Yanga Princes wanataka kufika waliko watani wao, ni lazima watie nguvu kwa maana ya uongozi. Yanga Princes itabidi wawatazame watani wao nguvu na uongozi walionao.

Simba Queens wametengeneza uongozi unaofanya kazi ya kupigania haki za mabinti wao. Fatema Dewji (mdogo wake Mohamed Dewji ‘MO’) ndiye mlezi mkuu wa timu hiyo.

Fatema pamoja na kamati yake wamekuwa bega kwa bega na timu. Hata baadhi ya mechi za Simba Queens wamekuwa wakija viongozi wakubwa wa Simba kutazama. Maisha haya ni tofauti na siku ikiwa inacheza Yanga Princes.

Viongozi wanaoonekana kuwa bega kwa bega na timu ni Thabit Kandoro na Kibwana Matokeo – utawaona uwanjani katika mechi nyingi za Yanga Princes.

Licha ya uchanga wa ligi ya wanawake hapa nchini, lakini Simba wamejitahidi kuwekeza katika klabu yao ya wanawake. Viongozi wametengeneza mazingira mazuri kwa wachezaji na kupunguza baadhi ya changamoto zao ndogo ndogo.

Wakati Simba Queens ipo katika harakati za kupanda daraja, kambi yao ilikuwa Ilala Bungoni. Kambi ile ilikuwa ya kawaida na haikustahili kuitwa kambi ya wachezaji wa Simba.

Lakini baada ya kupanda, kambi ile ikahamishiwa Bunju Arena sehemu ambayo kuna mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Yanga Princes wao wameingia kambini siku tatu kabla ya kukutana na Simba Queens. Nafahamu kuna marekebisho yanayoendelea pale Jangwani – makao makuu ambako ndiko kuna kambi ya Yanga Princes kwa muda mrefu sasa.

Lakini bado timu ingeweza kuweka kambi sehemu nyingine ili kupata muda mzuri wa kujiandaa kwa ajili ya  mechi za ligi. Sitaki kuamini siku zote tangu ligi itangazwe kuanza Desemba 23, mwaka jana bado Yanga Princess walikuwa hawajui watakaa wapi. Hili siliamini.

Mwisho, Yanga Princes inahitaji kuungwa mkono katika hali zote. Mara nyingi wachezaji wa Yanga Princes mnatakiwa kukaa nyuma yao. Sijui, lakini naamini ndani ya uvungu wa mioyo yao hawafurahi kuona jinsi wachezaji wa timu ya wanaume wanavyofanyiwa huku wao wakiachwa tu. 

Kipindi cha Sikukuu za mwishoni mwa mwaka tuliiona timu ya wanaume wakipewa vocha za kufanya ‘shopping’ katika maduka ya mdhamini wao GSM, lakini ofa hiyo hatukuiona kwa timu ya wanawake.

Ndiyo. Kiwango kinaweza kisilingane ila kuwafanyia hivyo mnawapa moyo na kuwaambia kwamba mpo nyuma yao.