Yatakayomkwamisha Rais Magufuli… (1)

Rais John Magufuli, ni Mwenyekiti wa tano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni Mwenyekiti mpya ndani ya chama kile kile. Ashakum, nadhani unaweza kusema ni mvinyo ule ule ndani ya chupa mpya. Upya wa chupa hauugeuzi mvinyo uwe mpya.

Dk. Magufuli ndiye Rais wetu wa tano hali hiyo ya kuwa kiongozi mkuu wa dola anayeongoza Serikali, haifanyi asijadiliwe kama kiongozi wa chama cha siasa kwa sababu ni Mwenyekiti wa CCM kama Freeman Mbowe alivyo Mwenyekiti wa CHADEMA, sawa na Anna Mghwira alivyo Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, akiitisha mkutano wa wenyeviti wa vyama vya siasa vya Tanzania, Mwenyekiti Dk. Magufuli asisite kuitika wala asione haya kuketi meza moja na wenyeviti wenzake akina James Mbatia wa NCCR- Mageuzi, Mghwira, Mbowe na wengineo kwa sababu Tanzania ilipoukubali mfumo wa vyama vingi Julai mosi, 1992 iliukubali ubatizo.

Rais Magufuli akiwa Mkristo anaelewa maana na umuhimu wa ubatizo, mwokozi wetu Yesu alijumuika kwenye foleni ya makahaba, watoza ushuru na wenye dhambi wengine akisubiria zamu yake ifike ili naye abatizwe na Yohana Mbatizaji.

Kwa asili yake Yesu alikuwa Mtakatifu, mwema na asiyekuwa na dhambi. Biblia inasema yeye ambaye hakuijua dhambi, bado alifunga safari kutoka mjini akaenda porini kwa Yohana ili abatizwe sawa na walivyobatizwa Wayahudi wengine. Kwa nini Yesu alibatizwa- hilo ni somo linalojitegemea, kinachotupasa ni kuuchukulia ubatizo wa Yesu kama funzo kwa wote wanaojiona ni wakubwa na waliotukuka.

Ilipofika zamu ya Yesu, Mungu aliwasiliana na Yohana kwa njia ya Roho akamwambia huyo ndiye Masihi, mara hiyo Yohana akapaza sauti yake akawaambia Waisraeli waliomsikiliza: “Huyu ndiye niliyesema habari zake huko nyuma kwamba ajaye nyuma yangu ni mkuu kuliko mimi hata sistahili kulegeza gidamu ya kiatu chake.”

Baada ya hapo yalifuata mabishano ya aina yake kati yao wawili, Yohana Mbatizaji alimhoji Yesu akisema: “Hata wewe unakuja kwangu? Mimi siko tayari kukubatiza.” Lakini Yesu alimkaribia na kumwambia: “Yohana tusibishane kubali hivi sasa kunibatiza kama unavyowabatiza Waisraeli wengine (wenye dhambi) kwa kuwa imetupasa sisi (tuliopewa uongozi na Mungu toka mbinguni) kuitimiza haki yote.” Hapa msisitizo ni wangu.

Kwa Mafarisayo na wakuu wengine wa jamii ya Kiyahudi waliojikweza na kuishi kwa haki za kujihesabia wao wenyewe badala ya kutumainia haki itokayo kwa Mungu, ubatizo kwao uligeuka kikwazo cha kuwakwamisha. Kwa sababu waliojikweza hawakuuona uhalali wa wao kujumuishwa kwenye kapu moja na makahaba na watoza ushuru waliowadharau wakidai ni wenye dhambi.

Siku moja wakuu hao walimhoji Yesu kuhusu aliyofanya kwamba alifanya kwa mamlaka ipi na kutoka kwa nani? Yesu akawajibu akisema naye atawauliza swali moja ambalo kama watamjibu kwa usahihi ndipo angewaambia aliyafanya hayo kwa mamlaka ipi, akawauliza ubatizo wa Yohana ulitoka wapi- mbinguni au duniani?

Nani aliyeasisi ubatizo- ni Mungu au binadamu? Wakahojiana wao kwa wao wakisema ikiwa wataukiri ukweli kwamba Mungu ndiye mwasisi wa ubatizo, Yesu atawauliza mbona hawakumwamini Yohana Mbatizaji ikiwa waliujua ukweli kuwa Mungu ndiye mwanzilishi wa ubatizo? Wakaona wakimpa jibu la kuukana ubatizo na kudai haukutoka mbinguni ila ulianzia duniani na uliasisiwa na binadamu, umma ungewapiga mawe kwa kuwa ulimwona Yohana ni mtu aliyetumwa na Mungu, kwa makusudi wakajifanya hamnazo wakadai hawajui ubatizo ulikotoka.

Nimetoa mfano wa Yesu, Mafarisayo na ubatizo kwa makusudi maalumu. Nchi yetu Tanzania ina Rais, CCM na vyama vya upinzani. Rais aliye kiongozi wa dola pia ndiye Mwenyekiti wa CCM. Je, ni wakati gani anaposema kama kiongozi wa Serikali na wakati gani anasema kama kiongozi wa chama? Hili bado halijawekwa wazi wala hakuna ufundi wa kulitenganisha.

Lakini suala hili litaisumbua Serikali, litaisumbua CCM, litamsumbua Rais Magufuli, pia litatusumbua Watanzania katika ujumla wetu. Rais anaongoza Serikali ambayo kimsingi haipaswi iwe na mpinzani kwa kuwa haitakiwi ipingwe na yeyote. Vyama vya siasa ni wapinzani wa CCM, siyo wapinzani wa Serikali- wakati gani wanapaswa kuipinga CCM pasipo kuigusa Serikali; hili halijawekwa wazi, nalo litawasumbua wapinzani, litaisumbua Serikali pia litatusumbua wananchi. Nani atatuondolea usumbufu?

Suala lilianza mwaka 1992 Tanzania ilipoukubali ‘ubatizo’ wa kutoka kwenye mfumo wa chama kimoja kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa. Neno kubatiza katika lugha ya Kiyunani linatamkwa kama “bapto” inayomaanisha kuzamisha.

Kwa hiyo uhalisia ni kwamba Tanzania ilizamishwa kwenye mfumo mpya wa vyama vingi. Kama ingekubali kuitimiza haki yote ingebidi iibuke ikiwa Tanzania mpya yenye utamaduni mpya. Kwa sababu hao waliokubali kuzamishwa na Yohana Mbatizaji kwenye maji ya Mto Yordani kwanza waliungama dhambi zao hadharani, ndipo wakazamishwa majini walipoibuka ilikuwa ishara kwamba wamezaliwa tena wakiwa watu wapya na walianza maisha mapya wakimhofu Mungu.

Tanzania ilipotoka kwenye chama kimoja kuingia kwenye vyama vingi vya siasa ilibidi ianze maisha mapya ya kisiasa tofauti na mazoea ya enzi za mfumo wa chama kimoja. Ilihitaji ujasiri kutoka nje ya mazoea kwani mfumo wa vyama vingi uliilazimisha CCM kufunga matawi yake kwenye ofisi za Serikali, viwandani na kwenye mashirika ya umma. CCM ilifunga matawi yake jeshini ambako enzi za mfumo wa chama kimoja tulikuwa na Mkoa wa Majeshi na Mwenyekiti wake alichukuliwa sawa na wenyeviti wa mikoa 17 iliyokuwako wakati huo.

CCM isingeweza kupingana na upepo wa mabadiliko yaani mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yaliyoanzia Ulaya Mashariki. Kila nchi iliyothubutu kupingana na upepo wa mabadiliko ilitikiswa hadi mfumo wake wa utawala, siasa na uchumi vikasambaratika.

Dola kuu ya USSR muungano wake ulitikiswa hatimaye ukasambaratika. Kuna sababu kuu tatu ama “factors” zilizosababisha mageuzi. Mambo hayo matatu ni Uhuru, Demokrasia na Haki za Binaadamu, kwenye nchi zote zilizoongozwa na mfumo wa chama kimoja bila kujali mfumo wa kisiasa kama ni ukomunisti, usoshalisti au ubepari, zilikuwa na mambo yaliyofanana.

Wananchi ndani ya nchi hizo walikosa uhuru, walibaki na uhuru wa nchi uliokuwa uhuru wa jumla kwamba nchi yao ilipata uhuru tarehe, mwezi na mwaka fulani. Lakini wananchi wakiwa kama watu binafsi hawakuwa huru. Walikosa uhuru wa kusema na kuwa na maoni tofauti na maoni ya watawala, walitakiwa kusema yale ambayo watawala walitaka kuyasika.

Vyombo vya habari havikuwa huru, viliandika na kutangaza habari ambazo serikali ilizihakiki na iliridhia zitangazwe hata kama hazikuwa na ukweli. Ukweli ulifichwa, ulipuuzwa au ulipindishwa; lengo likiwa kuwafurahisha watawala. Matokeo yake wananchi walikosa imani na viongozi wao ila walificha wakaishi kama bubu hawakusema walichoamini.

Mfumo ulizifanya nchi zikose uongozi zibaki na utawala tu. Hali hiyo iliwafanya viongozi walimbikize matatizo wasiyoyatolea suluhisho. Kukosekana uhuru kuliwafanya watu ndani ya chama kimoja wakose utamaduni wa kuelezana ukweli. Hawakukosoana wala hawakuwakosoa wakubwa na kuwaonesha makosa yao. Matokeo yakawa mabaya kwani matatizo mengi yalirundikana kwa muda mrefu pasipo kupatiwa ufumbuzi.

Wananchi walinyimwa haki ya kukusanyika pamoja nje ya mikusanyiko rasmi iliyoridhiwa (iliyotambuliwa) na dola. Hapo ndipo viongozi wabovu waliposifiwa na kutukuzwa kupita kiasi huku ubovu wao ukifunikwa na kuendelea kuiathiri nchi.

Ulipofika wakati wa uchaguzi mkuu wananchi walinyimwa haki ya kuchagua. Mfumo wa upigaji kura za ‘ndiyo’ au ‘hapana’ haukuwezesha wananchi kuchagua, bali watu walipigishwa kura ili kuwaidhinisha waliogombea.

Wananchi hawakuweza kubadilisha uongozi dhaifu kupitia sanduku la kura, hawakuwezeshwa kuwaondoa uongozi usiowafaa ili kuweka viongozi wengine kwa njia halali. Mbaya zaidi, wananchi wasingeweza kuubadilisha uongozi wa nchi yao kwa kuushawishi ufanye mambo mengine yaliyo mazuri nje ya hayo waliyowaza, waliyopenda na kuyapanga wao waliotawala.

Kiuhalisi utawala ulifunga milango, njia na uwezekano wa mema kutoka nje yasipenye wala yasiingizwe kwenye mfumo.

Kukosekana uhuru, haki na demokrasia kuliwalazimisha wananchi kuongozwa na viongozi wabovu kwa kuwa hazikuwako njia mbadala za kubadilisha viongozi na kuwaondoa madarakani wabovu waliochokwa.

Wananchi walilazimika kutekeleza mipango mibovu ya watawala ambao hawakuruhusu mawazo mapya yaingie kwa kuwa mfumo ulizuia. Wakasababisha kasi ya maendeleo iwe ndogo.

Wakati ulifika wananchi wakaona linahitajika jukwaa lingine linalowawezesha kuishi wakiwa huru kwenye nchi yao. Wakati ulifika ulipohitajika mfumo mwingine unaoruhusu wananchi kubadilisha mambo kwa kuondoa yote yaliyowakera ili kuleta mapya. Bahati mbaya mabadiliko yaliyotakiwa na umma yalitishia kuwang’oa madarakani watawala wa zamani ili kupata watawala wapya. CCM ilipoyatazama yaliyotokea nchi za Ulaya Mashariki ilitishika, ikaamua kujihami kwa njia zote. Badala ya kuangalia “factors” zilizosababisha mageuzi, CCM iliamua kuyadhibiti mageuzi ili isiondoke madarakani.

Ilifanikiwa kujibakiza madarani, lakini haikufanikiwa kuugeuza umma usihitaji mabadiliko. Watanzania waliendelea kuwa wenye kiu ya mabadiliko kwa sababu walichoshwa na ufisadi, walichoshwa na hali ngumu ya maisha, huku wengi wakiwa wamekata tamaa. Umma ulikuwa unatafuta jawabu, siyo majibu mepesi wala ahadi mpya zisizotekelezeka. Umma ulitaka jawabu au suluhisho la matatizo sugu yaliyorundikana kwa muda mrefu bila ufumbuzi na yaliyolisumbua Taifa.

Kwenye siasa za ushindani chini ya demokrasia ya kweli inayowezesha watu kuchaguana kwa uhuru kuna aina mbili za ushindi- kuna ushindi wa mgombea dhidi ya mwenzake waliyeshindana, pili kuna ushindi wa mpiga kura.

Wapiga kura hawawezi kuushangilia ushindi wa mgombea unaotokana na kura zao kwa sababu kwao hauna manufaa.

Ushindi wa mpiga kura ni pale matatizo yanayokera yanapopatiwa ufumbuzi.

Rais Magufuli angeyapatia ufumbuzi yanayoukera umma, angeibuka mshindi kila siku, kila wiki, kila mwezi, kila mwaka wala asingeingia kwenye mtego wa kupingana au kupigana na wananchi wake.

Ushindi wa mpiga kura ungemtengenezea Rais Magufuli mazingira mazuri ya kushinda uchaguzi ujao kutokana na uhalali unaojengwa katika miaka mitano ya utawala kwake. Lakini yaelekea “factors” zimefichwa (zimefunikwa) na kilichofunuliwa kwake ni mapambano dhidi ya CHADEMA upande wa Bara, na CUF upande wa Visiwani.

Rais Magufuli anafukuzana na vivuli vya aliowashinda. Anawajenga badala ya kuwabomoa. Kwenye mikutano yake kila atakapolitaja jina la Lowasa atamwandika kwenye kumbukumbu za hao walioanza kumsahau, hatimaye wananchi watajiuliza Rais wao anapoendelea kushindana na huyo aliyemshinda anatarajia kupata nini?

 

Mwinjilisti Kamala Kusupa anapatikana kupitia namba 0786 311 422.