“Tanzania sawa na Hamaphrodite anayeona aibu kujitangaza”

Nakiri kutoka moyoni kwamba simtakii mabaya Rais Magufuli wala simtabirii kushindwa, sitafurahi akikwama kuifanyia nchi yetu jema lolote alilodhamiria.Nayaweka wazi mazingira yanayoweza kumkwamisha ili akiweza ajiepushe.

La kwanza linaloweza kumkwamisha ni kuthubutu kuurudisha mfumo wa chama kimoja kupitia mlango wa nyuma, hapo lazima nchi itakwama kwasababu mfumo huo ulikwishaanguka,ndio uliosababisha dola za Ulaya mashariki zisambaratike, mfumo ulioanguka hauwezi kutumika kufufua viwanda au kujenga viwanda vipya, kujenga Reli wala kutoa elimu bure.

Narudia niliyoyaandika kwenye kitabu cha hii ndiyo Tanzania tunayoitaka ambapo nimeifananisha Tanzania na “Hamaphrodite”wa kisiasa na kiuchumi. “Hamaphrodite” ni neno la Kiyunani linalomaanisha binaadamu aliyezaliwa na jinsia zote mbili ya kike na ya kiume.

Wayunani wa kale waliamini kuna Mungu mume waliyemwita “Hamas” na Mungu mke waliyemwita “Flora” pia waliamini wanadamu wanapokutana kuzaa miungu nayo ilikutana kuumba.Wayunani waliamini inapotokea “Hamas” kumzidi nguvu “Phlora”alizaliwa mtoto wa kiume na“Phlora” alipomzidi nguvu “Hamas” alizaliwa mtoto wa kike. Ilipotokea nguvu za miungu hao kuwa sawa ndipo wazazi walimzaa mtoto mwenye jinsia zote mbili ya “Hamas” na ya “Phlora” wakamwita “Hamaphrodite.”

Mtu anayejikuta amezaliwa akiwa na jinsia zote mbili anapokuwa hatua za utotoni hapati tatizo la kujumuika na watoto wenzake. Lakini matatizo humkuta ukubwani kwakuwa kadri anavyozidi kukua ndivyo anavyolazimika kujitambulisha na kundi mojawapo, aidha kundi la wavulana ama kundi la wasichana.

Tatizo lingine la “Hamaphrodite” huwa ni mfumo wake wa ndani ya mwili, maana ingawaje mwonekano wa nje huthibitisha kwamba anazo jinsia mbili, lakini kwa ndani huwa na mfumo mmoja aidha wa kike ama mfumo wa kiume hawezi kuwa na mifumo yote miwili naye hutambulika hapo anapopevuka.

Ikitokea alipokuwa mtoto wazazi wake walimwaminisha kwamba ni msichana wakampa jina la kike, waliomzunguka wakamwelewa hivyo,lakini anapopevuka akijigundua kwamba ni mwanaume hupata ugumu wa kujitangaza kwamba kuanzia leo mimi sio tena fulani msichana bali ni mvulana ninayeitwa fulani.

Huko nyuma mkoani Morogoro ilitokea mwanafunzi msichana aliyekuwa akisoma sekondari alipata ujauzito akafukuzwa shule. Msichana alipofika nyumbani kwao wazazi wake walim’bana aeleze mwanamume aliyempa ujauzito, msichana akamtaja mwalimu wake ambaye jumuia ya shule ilimfahamu kuwa ni mwalimu wa kike. Hapo siri ikafichuka kwamba kumbe mwalimu alikuwa “Hamaphrodite” ingawa nje alionekana mwanamke,kiuhalisia mfumo wake kwa ndani ulikuwa wa kiume.

Mzizimo ukawapata wazazi wa msichana aliyepewa mimba kwamba itakuwaje binti yao atakapowaletea mjukuu ambaye baba yake ni mwanamke na mwenye jina la kike?

Mazingira ya kisiasa ya Tanzania yanafanana na hali hiyo kwasababu kihistoria tulikoloniwa na wazungu kwa miaka 75, katika kipindi hicho wazungu walifanya kazi ya kututoa kutoka kwenye Uafrika wetu wakitutamadunisha upya hadi wakatufikisha kwenye “uzungu.”

Wazungu walituanzishia mifumo mipya na kusababisha tuendeshe maisha yetu ndani ya mifumo ya kigeni, kwa maana hiyonasi “tuligenishwa” (foregnised) ndani ya nchi yetu wenyewe.

Tulipopata uhuru hatukuondokana na madhila yote ya ukoloni bali tulibaki na nusu uhuru na nusu ukoloni, kwa nje tulionekana tuko huru tusiotawaliwa tena na Mwingereza. Lakini mfumo wa utawala na uendeshaji wanchi ulibaki kama ulivyoanzishwa na mkoloni, mfumo wa uchumi ulibaki ule ule alioasisi mkoloni  na ulitimiza malengo ya kikoloni yakunyonya na kuhamishia faida nje ya nchi.

Utawala ulikuwa kitendawili, kwasababu Tanganyika ilitawaliwa na Gavana ambaye aliteuliwa na Malkia na aliwajibika kwa Malkia peke yake. Madaraka yake hayakuwa na ukomo wa kisheria wala kikatiba kwakuwa Gavana hakuitawala Tanganyika kwa kutumia katiba.

Kwahiyo Gavana wa kikoloni hakuwa chini ya sheria, alikuwa hapingwi, haulizwi wala hahojiwi na Mtanganyika yeyote, sijui kama alishauriwa.Mtanganyika mzawa hakuthubutu kubishana na lolote aliloamua Gavana liwe sahihi ama lisiwe sahihi.

Tanganyika ilipokaribia kupata uhuru mkoloni aliandika katiba ya uhuru pasipo kuwashirikisha wananchi, Watanganyika wengi hawakuelewa. Kutokana na hali yao ya kukosa elimu na uelewa hawakutilia maanani suala la katiba, wao walichokiona muhimu ni wazungu waondoke warudi kwao Ulaya ili Waafrika wajitawale.

Siku ya sherehe za uhuru walipokabidhiana madaraka pale Mnazi mmoja, wakoloni walimpa Mwalimu Nyerere nakala moja ya katiba naye akawakabidhi bendera yao ya “Union Jack.”

Waingereza ndio walioandika katiba ya Tanganyika huru na ndio waliobuni cheo cha “Chief Minister” awe mkuu wa dola, kiuhalisia madaraka aliyokuwa nayo Gavana wa kikoloni yalihamishiwa kwa “Chief Minister” ambaye sisi tulimwitaWaziri mkuu.

Nyerere alikaa kwenye Uwaziri mkuu siku 42 tu akajiuzulu, sababu za kujiuzulu haziwekwi wazi, lakini yaelekea mambo mawili yalimshinikiza Nyerere kujiuzulu. Kwanza aligundua madaraka aliyopewa kikatiba hayakumwezesha kuishi kama mkuu wa dola huru, bado aliendelea kuwajibika kwa Malkia akaamua kudai Jamhuri, Tanganyika ikawa Jamhuri tarehe 09 Desemba, 1962.

Sababu ya pili lilitokea fukuto la maasi ambayo yalihatarisha kuibua kwa mgogoro kama uliokuwa umetokea Congo kwa Lumumba.

Nyerere aliamua kwenda makao makuu ya TANU akajikita kwa mwaka ili kuzimisha na kukomesha mbegu ya uasi kwa hao waliokuwa hawamkubali, nimeyaeleza kwa kina kitabuni kwenye somo la Urais kiti cha moto.

Nyerere aliporudi madarakani kwa mara ya pili alikuwa Rais mtendaji, Tanganyika iliiga mfumo wa Marekani, hata hivyo chimbuko la madaraka ya Rais mtendaji bado yalitokana na Gavana wa kikoloni, aliyekuwa haulizwi, hapingwi, hahojiwi, maamuzi yake hayajadiliwi na lolote alilotakaalilifanya bila pingamizi, waliokuwa chini yake walitakiwa kutii na si vinginevyo.

Hapa ndipo chimbuko la mgogoro wanchi kuwa na Urais wa kifalme ambao ulikuwa ghali kuliko hata ufalme wenyewe. Rais wa Tanganyika huru hakuwajibika tena kwa Malkia wala hakuwajibika kwa Bunge kama alivyoRais wa Marekani, bali Rais wetu akawa juu ya kila kitu.

Rais pia aliendelea kuitawala nchi akitumia sheria za kikoloni, akitumia vyombo vya dola vya kikoloni na watendaji walioelimishwa na mkoloni.Hayo yalikuwa mazingira mapya ya uhuru ndani ya ukoloni yaliyokuwa mbaya kuuzidi ukoloni wenyewe.

Nchi iliendeshwa ikiwa kwenye hali ya mpito “transitional” kutoka ukoloni kuelekea uhuru, yakatokeamashinikizo yaliyomsukuma Nyerere ayakubali mabadiliko, maasi ya Jeshi kuu Tanganyika Rifles mwaka 1964 na jaribio la Shirikisho la Wafanya kazi kutaka kumwondoa madarakani.

Mwezi Novemba mwaka 1966 Nyerere akatikiswa tena na maandamano ya wasomi, ingawa yanaelezwa kwamba wanafunzi walipinga sera ya JKT, lakini nilipotafiti nikajua walidai mengi mojawapo walipinga tabaka la wanasiasa walioanza kujigeuza wanyonyaji wa umma wakitumia madaraka.

Nyerere alipozingatia ukweli wao bada ya siku 40 aliibuka na Azimio la Arusha ambalo lilimwongezea uhalali wa kutawala kwakuwa wananchi walio wengi walilikubali. Nchi yetu ikaingia kwenye mpito mwingine wa kutoka kwenye ubepari kuelekea kwenye Ujamaa, hata hivyo uhalisia wake ni kwamba kwa miaka 20 tuliendesha shughuli za kijamaa ndani ya mfumo wa kibepari, hilo lilikuwa na athari zake.

Inajulikana kwamba mnamo 1985 Nyerere aling’atuka (alistaafu), utawala wa Alhaji Alli Hassan Mwinyi uliofuatia (1985- 1995) haukuwa na mfumo rasmi wa kueleweka kwani ulegezaji wa masharti ya biashara haukuwa mfumo bali zilikuwa hatua za dharula baadaye zikazoeleka.

Viwanda vyetu vilizalisha chini ya kiasi kilichohitajika likawepo tatizo la upungufu wa bidhaa madukani, ndipo utawala wa Mwinyi ukaamua kulegeza masharti ya biashara ili kuwaruhusu walioweza waingize bidhaa kutoka nje waondoe nakishi au “deficit” iliyokuwako.

Matokeo yakawa tofauti na Mwinyi alivyodhamiria ndio maana namtahadharisha Magufuli kuhusiana na hatua zake kwamba sio lazima zitoe matokeo anayodhania, zinaweza kumpa matokeo mengine asiyotarajia. Kwasababu katika maisha ya kawaida moja na moja ni mbili, lakini katika siasa moja ya kisiasa na moja nyingine siyo lazima ziwe mbili, inaweza kuja sifuri au zaidi ya mbili.

Chini ya utaratibu wa OGL Benki kuu ilifungua “Open General License” wenye fedha waliingiza bidhaa kutoka nje kwenye nchi zilizoendelea kwa tekinolojia ya viwanda, bidhaa za nje zilizokuwa bora ziliuzwa kwa bei ya chini kwakuwa waingizaji wengi walikwepa kodi na ushuru.

Watu wakazielekea bidhaa za nje ambazo viwanda vyetu visingeweza kuhimili ushindani kwa ubora na bei, taratibu viwanda vyetu vikaanza kutetereka hatimaye vikafa kifo cha mende,kwasababu wahusika hawakudhibiti “importation” ikaua viwanda vyetu, ingawa wizi, uzembe na menejimenti mbovu navyo vilichangia.

Waingizaji walipoona viwanda vyetu vimekufa wakaanza kuingiza bidhaa hafifu mwisho wakaigeuza Tanzania “dampo” la kupokea bidhaa zinazostahili kutupwa au kuchomwa moto, tatizo la kuingia kwa bidhaa bandia sasa limekuwa sugu.

Kufikia 1990 Ulaya mashariki ilikumbwa na upepo wa mabadiliko ulioiathiri Afrika, Tanzania ikayakubali mageuzi kwa nje lakini kwa ndani ni kama iliyakataa. Badala ya kuukubali mfumo wa vyama vingi, watawala wetu waliokuwako wakati huo waliudhibiti wakayahujumu mabadiliko.

Badala ya kutunga katiba mpya waliamua kunyofoa kwenye katiba ya nchi kifungu kilichokataza vyama vingi wakajifanya kuviruhusu.Lakini mfumo mzima ukabaki ule ule wa chama kimoja, matokeo Tanzania ikawana vyama vingi vinavyojiendesha ndani ya mfumo wa chama kimoja, huu “uhamaphrodite” wa pili umekuwa mbaya kuliko wote uliotokea huko nyuma.

Baadhi ya matatizo yanatukuta kwasababu ya kung’ang’ania mfumo wa kale uliokwisha kupitwa na wakati, tuchukulie mfano hai wa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM kuendelea na kofia mbili “Uenyekiti” na “Urais.”

Je, ni wakati gani Dk Magufuli anaweza kusema kama mwenyekiti wa chama anayestahili kujibiwa, kujadiliwa ama hata kupingwa na wanasiasa au wenyeviti wenzake wa vyama vya upinzani?

Je, ni wakati gani Dk Magufuli anaweza kuuweka kando uenyekiti wake wa CCM akasema kama Rais wa nchi asiyestahili kupingwa na mwananchi yeyote? Ukweli ni kwamba hakuna ufundi wa kumtenganisha mtu mmoja kiasi kwamba tukawa na Magufuli wawili yaani Magufuli mwanasiasa anayeweza kukosolewa ama kupingwa na magufuli mtawala asiyestahili kupingwa na yeyote.

Haiwezekani serikali ikaendeshwa “kisiasa” wala chama cha siasa kikaendeshwa “kiserikali” ikitokea “vice versa” chama tawala “kikaserikalishwa” na serikali ya chama “ikasiasaishwa” lazima Tanzania itakwama na kudidimia.

 

Mwinjilisti Kamara Kusupa – 

0786 311 422

By Jamhuri