Moja ya makala zilizobeba uzito katika toleo hili, ni ile inayohusu tuhuma za kituo cha watoto yatima kugeuzwa mradi wa biashara ya mtu binafsi. Kituo kinachotajwa katika makala hiyo ni kile kinachojulikana kama ‘City of Hope’ kilichopo katika Kijiji cha Ntagacha, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Baadhi ya wanakijiji waliozungumza na mwandishi wa makala hayo wanamtuhumu Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. John Chacha, anayeishi Marekani kwamba amekigeuza kuwa biashara yake binafsi. Kwamba badala ya kutekeleza madhumuni yake ya kuhudumia watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi, miradi ya shule na zahanati ya kituo hicho imegeuzwa kuwa vitegauchumi vya Dk. Chacha, ingawa bado mwandishi anaendelea kumtafuta azungumzie tuhuma hizo.

 

Tuhuma nyingine ni kwamba alitumia kivuli cha huruma ya watoto yatima kurubuni wanakijiji, wakampatia ardhi kubwa ya kujenga kituo hicho. Na inaelezwa kwamba wanakijiji walijitolea pia kuchangia nguvukazi ya ujenzi wa zahanati ya kituo hicho, baada ya kuahidiwa neema ya kupata huduma za matibabu kwa gharama nafuu. Hata hivyo, baada ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho, Dk. Chacha anadaiwa kuwageuka wanakijiji kwa kuwalipisha gharama kubwa za matibabu kinyume cha makubaliano yao.

 

Shule iliyojengwa kituoni hapo kwa madhumuni ya kusomesha watoto yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi, inadaiwa kuendeshwa kibiashara zaidi kwa kutoa kipaumbele kwa watoto wa matajiri kutoka maeneo mbalimbali wanaolipiwa ada nono.

 

Kimsingi JAMHURI hatuwezi kumhukumu Dk. Chacha moja kwa moja kufuatia tuhuma zinazoelekezwa kwake, lakini tunadhani kuna haja ya Serikali kuingilia kati suala hilo ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na wananchi wenye hasira. Mamlaka husika za Serikali zichukue hatua ya kufuatilia tuhuma hizo na kutafuta ufumbuzi haraka iwezekanavyo, badala ya kuendelea kukaa kimya huku zikiwa zimeshapata malalamiko hayo.

 

Serikali inapaswa kuwa makini kwa kuhakikisha watu wenye uchu wa kupata utajiri wa harakaharaka, hawapewi nafasi ya kutumia migongo ya makundi yasiyojiweza kama watoto yatima kujineemesha kilaini. Uchunguzi wa hivi karibuni, umebaini kuwa baadhi ya wasomi wanaongeza kasi ya kujikita katika kutumia kivuli cha makundi yasiyojiweza na watu wenye matatizo kama njia ya kujifutia umaskini.

 

Ndiyo maana sisi JAMHURI tunasema hatutaki kusikia wala kuona watoto yatima na makundi mengine yasiyojiweza katika jamii, yanageuzwa migongo ya watu wachache kujineemesha.

By Jamhuri