seifWakati Zanzibar ikikumbwa na mzozo wa kisiasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kwa madai ya kuwepo kwa dosari mbalimbali, hali ya mambo imekuwa sintofahamu.

Kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi visiwani humo kunaelezwa kuwa ni agizo la viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makao Makuu. Hali hiyo inatokana na chama hicho kuona kimeshindwa katika uchaguzi mwaka. Hayo ni madai yanayojadiliwa kwenye vyombo vya habari na sehemu nyinginezo.

CCM kimekuwa kikijiita chama dola. Kwa kuwa kina uwezo wa kuongoza kwa namna yoyote ile. Iwe kwa njia yoyote.

Kuhusu Zanzibar walishindwa kuweka nguvu kubwa kukabiliana na CUF. Wakaelekeza nguvu zao zote bara kutokana na ushindani mkali wa kisiasa uliochochewa na makada wake maarufu kukihama chama hicho akiwemo Edward Lowassa aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema.

Kinachowatesa sasa ni kushindwa kutumia mbinu kama zilizotumika bara kujihakikishia kutawala kama wapendavyo. Hawako tayari kuiachia Zanzibar mikononi mwa Wazanzibar wenyewe na kuheshimu uamuzi wa wananchi kwa njia ya kidemokrasia.

Wanaosema uchaguzi urudiwe. Bila shaka wana ajenda yao ya siri. Hawataki Wazanzibar waamue mambo yao na kuwachagua viongozi wawatakao kwa njia ya kidemokrasia.

Uamuzi wa Jecha, kufuta matokeo unafunua siri iliyofichika kwa wananchi wengi kwamba Zanzibar ni koloni la Tanganyika na CCM hilo wanalielewa. Hii ndio sababu iliyofanya waamuru matokeo yafutwe kwa kuwa CUF ilikuwa inaongoza.

Ukweli lazima usemwe. Kama Watanzania tutafikia mahali kujenga matabaka ya kisiasa kwamba kiongozi fulani hafai kuongoza kwa sababu anatoka nje ya chama kilichoko mamlakani huu ni “ulevi wa madaraka na ndio ukaburu” aliouelezea Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Suala hili limeanza kuzua vita vya maneno kwa pande mbili CCM na CUF. Wakati upande mmoja unataka matokeo yatangazwe na mshindi apewe nafasi ya kuongoza serikali na mwingine unataka uchaguzi urudiwe na kwamba kinachosubiriwa ni tarehe ya kufanyika upya kwa uchaguzi huo.

Licha ya mzozo huo bado mazungumzo yanaendelea kati ya waliokuwa wagombea urais wa uchaguzi huo Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM na Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF ambayo yanawahusisha na marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.

Pamoja na mvutano uliopo sasa hakuna taarifa kamili zilizowahi kutolewa kuhusu nini kinazungumzwa kwenye mazungumzo hayo ya vyama hivyo ingawa vimekuwa vikitoa kauli ambazo zimekuwa zikiacha maswali kuhusu mazungumzo hayo.

Kitendo kinachofanywa na CCM kinaweza kuleta vurugu kubwa za kisiasa Zanzibar kutokana na makada wake kung’ang’ania uchaguzi huo urudiwe. Hili linaweza kulazimishwa tu. Sio kama watakavyo Wazanzibar walio wengi. Mashinikizo ya kibabe mara nyingi hayavumiliki na ndio chanzo cha kuvurugika kwa amani.

Katika hili CCM wanajua wanachokifanya. Wanacheza na maisha ya Watanzania kwa kujihakikishia kutawala watakavyo. Hii ni hofu inayotokana na watawala. Wakati wote watawala wetu wanapaswa kuelewa kuwa kuna kuungwa mkono na vile vile kupingwa.

Ni aibu kubwa tuliyoipata watanzania baada ya uchaguzi mkuu na kupoteza sifa ya kuaminiwa na mataifa mengine kama watatuzi wazuri wa mizozo katika inayoibuka kwa majirani zetu. Viongozi wetu hawana ujasiri wa kusuluhisha mzozo wa kisiasa Burundi na kwingineko kwa kuwa wanafanana kwa tabia na vitendo vyao.

Wameonekana kulazimisha matokeo ya chaguzi zetu ili CCM ipate ushindi tu. Kwa ujinga wanaoufanya Zanzibar kwa kutaka uchaguzi urudiwe. Je wakishinda CCM, nani atamlazimisha Jecha kutangaza uchaguzi ni batili. Haya yote yanaletwa na tume zinazoundwa kwa maslahi ya vyama vinavyokuwa mamlakani. 

ZEC ilipingwa na wadau mbalimbali kikiwamo Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) kilichosema kwamba Jecha hakuwa na mamlaka ya kufuta uchaguzi.

ZLS inaeleza kwamba Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Sheria ya Uchaguzi Namba 11 ya 1984 Ibara ya 119 (1) Tume ni Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine sita kama walivyoainishwa na ibara hiyo na uamuzi wowote wa tume lazima uungwe mkono na wajumbe waliowengi lakini uamuzi wa kufuta matokeo hayo ulitangazwa na mwenyekiti tu.

Suala la Zanzibar lisiendeshwe kibabe na kama CCM itazidi kushupaza shingo amani inaweza kutoweka. Uongozi unahitaji zaidi busara.

1699 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!