Zavala ‘wasotea’ umeme miaka 7

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani, limesema wananchi wa Zavala, Kata ya Chanika wataanza kupelekewa huduma ya umeme wiki hii.

Meneja wa Tanesco Mkoa wa Pwani, Injinia Martin Madulu, ameithibitishia JAMHURI kuwa maandalizi yote kwa ajili ya kazi hiyo yameshakamilika.

Amewaomba wananchi wawe na subira kwa kuwa shirika linatambua umuhimu wa mradi huo ambao umeombwa miaka takribani saba sasa.

Kauli ya Madulu imetokana na malalamiko ya wananchi wa Zavala, ambao wamesema wameomba huduma hiyo kwa muda mrefu bila mafanikio.

Wakazi wengi wa Zavala ni wale ambao awali walikuwa wanaishi karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), lakini wakahamishwa ili kuruhusu upanuzi wa uwanja huo.

“Siyo kazi rahisi kuwafikishia wananchi wote umeme kwa siku moja. Lengo la Serikali ni kuhakikisha hadi mwaka 2030 wananchi wengi kadri inavyowezekana wanapata huduma ya umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA).

“Mradi unapoanza mkandarasi anakuwa sehemu moja, huwezi kumtoa hapo na kumpeleka kwingine ambako wananchi wangependa kuona mradi wao ukitekelezwa. Work force (nguvu kazi) ni hiyo hiyo, kwa hiyo inabidi amalize sehemu moja ndipo aende kwenye mradi mwingine.

“Wananchi wanataka umeme, kuna mwamko mkubwa na maombi mengi, lakini nina furaha kukueleza kuwa wananchi wa Zavala wasiwe na wasiwasi. Mkandarasi ameniambia yuko site (eneo la kazi) ili Februari 15 kazi ianze. Kazi itaanza na kukamilika ndani ya siku tatu. Jumanne au Jumatano (Februari 20) itakuwa imekamilika.

“Naomba Zavala wawe wavumilivu, shida tunayoipata ni kuwa kila mtu aliyeomba umeme anataka tuanze na yeye, lakini ni ukweli kuwa miradi haiwezi kuanza siku moja kwa kila mahali,” amesema Injinia Madulu.

Wakazi wa Zavala katika malalamiko yao, wanasema wamekuwa wakifuatilia kupata nishati hiyo kwa miaka saba bila mafanikio. Kimuundo, Tanesco Zavala ipo chini ya Meneja wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani.  

“Sisi ni wazalendo kwa Taifa letu, tulihama Airport ili kupisha upanuzi wa uwanja ambao unaingiza fedha nyingi kwa Taifa letu na kupewa viwanja katika eneo la Zavala huku tukiahidiwa kupata mahitaji yote muhimu kama vile umeme, maji, shule, soko na hospitali katika makazi mapya.

“Inasikitisha sana tangu mwaka 2008 tulipohamishwa tulichoambulia ni viwanja tu ambavyo tumejenga na tunaishi, lakini hakuna umeme,” anasema mmoja wa wakazi wa Zavala.

 Wananchi hao wanasema walishaambiwa na Tanesco kuwa mkandarasi amepatikana (Mradi wa Kigilagila) na siku yoyote angefikisha huduma hiyo Zavala.

“Jibu hilo tumekuwa tunapewa tangu mwaka 2010. Ni aibu na fedheha kwa wakazi wa Ilala, Dar es Salaam kukosa umeme wakati ukipita Tabata Liwiti na Ubungo Maziwa unakuta nguzo za umeme zimelala hapo.

“Huduma hii ikiletwa na sisi tunakuwa wateja ambao ni wanunuzi wa umeme na tunalipa service charges, hivyo tunaongeza mapato kwa Tanesco na Serikali kwa jumla. Tunashangaa kwa nini huduma hii icheleweshwe kwa muda wote huo!” wanasema wakazi hao.