LeoBaada ya usiri wa muda mrefu juu ya familia ya Rais (mstaafu), Jakaya Kikwete, kuhusika na ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) uliotawaliwa na kiwingu, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebainika kuwa familia hiyo inahusika na ni sehemu ya umiliki wa kampuni ya Simon Group iliyonunua UDA.

Habari zisizotiliwa shaka zinazoambatana na vielelezo, zinathibitisha pasi shaka kuwa familia hiyo ilitumia nguvu kubwa kuhakikisha Simon Group inanunua UDA kwa bei ya kutupwa, kwa nia ya kufaidisha familia.

Nyaraka za ukaguzi wa kina uliofanywa na Kampuni ya Philip & Company yenye makao makuu katika Jengo la NIC Life House, Dar es Salaam mwezi Novemba 2009 kabla ya Simon Group kuuziwa hisa za UDA na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kinyume cha sheria inayosimamia ubinafsishaji, zinabainisha uhusika wa familia ya Kikwete katika Kampuni ya Simon Group.

“Mwaka 2008 hesabu za Kampuni ya Simon Group zilizochapishwa zilionesha ina wakurugenzi wawili ambao ni Bwana Robert Simon Kisena na Bwana Khalfan Mrisho,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya ukaguzi wa kina. Khalfan Mrisho ni mtoto wa Kikwete na ndiye anayemiliki hisa katika Kampuni ya Simon Group kwa niaba ya familia ya Kikwete.

Uwepo wa Khalfan katika umiliki wa Kampuni ya Simon Group ndiyo ulioelezwa kuipa nguvu za ajabu kampuni hiyo na kudiriki kununua mali za Serikali bila kufuata utaratibu wa kisheria. Hata waliohusika kupindisha sheria katika kuuza mali hizo za umma, hata pale walipofunguliwa mashitaka kama aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Iddi Simba, kesi yake ilifutwa na Mkurugenzi wa Mashitaka wa wakati huo, Eliezer Feleshi, ambaye baadaye Rais Kikwete alimteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu anakoendelea kutumikia wadhifa huo.

Ukaguzi ulibainisha kuwa Kampuni ya Simon Group haikuwa na uzoefu katika biashara ya kusafirisha abiria, hesabu zake zilikuwa na maswali mengi kuliko majibu na ilionesha kupata faida ya Sh bilioni moja baada ya kufanya kazi kwa mwezi mmoja, huku ikishangaza ulimwengu wa biashara kwa kuwa na hesabu za mwaka mzima wa 2007 wakati imesajiliwa Novemba, 2007.

Kampuni hiyo ilikosea misingi ya uhasibu kwa kuonesha kuwa mwaka 2008 ilipata faida ya Sh bilioni 1.7, mali za kampuni zilikua ghafla na kufikia sh bilioni 4.88 lakini kinyume na Viwango vya Kimataifa vya Taarifa za Fedha (IFRS), hesabu hizo hazikuonesha uchakavu wakati kuna vifaa kama magari, viti, kompyuta na vifaa vingine vingi vinavyoanza kuchakaa tangu siku ya kwanza.

Philip & Co wamebaini jinai ya kukwepa kodi, kwani katika faidi ya Sh bilioni 1.7 iliyotangaza kupata Kampuni ya Simon Group kwa mwaka huo wa fedha, ililipa kodi Sh 225,000 tu. Sheria ya Kodi inaitaka kampuni kulipa asilimia 30 ya faida iliyopata, hivyo kwa kupata faida ya Sh bilioni 1.7, Simon Group ilipaswa kulipa Sh milioni 510 kama kodi kwa mwaka 2008. Kodi hii haikulipwa.

Si hilo tu, kilichowashangaza wakaguzi kwa kampuni hii iliyojinasibu kuwa na uwezo mkubwa kifedha, hesabu ilizowasilisha kwao hazikuwa na muhuri wa TRA kuthibitisha kuwa zilikaguliwa na kuwasilishwa TRA, na kampuni hiyo ilionesha kupata mikopo ya Sh bilioni 2.7 na Sh milioni 250 katika mazingira yasiyo ya wazi. Walipofuatilia katika Bodi ya Ukaguzi na Uhasibu (NBAA), walikuta mkaguzi aliyetumiwa na Simon Group kuthibitisha hesabu zao, hayumo kwenye orodha ya wakaguzi wanaotambulika.

“Mpango wa kuthamanisha upya mali za kampuni, hata hizi zilizoingizwa katika mwaka [2008] inaonekana zilitengenezwa kuongeza thamani yao kwamba waonekane wana uwezo waweze kupata mikopo kwa ajili ya kununua mali za kiwanda cha Igogo,” wanahitimisha wakaguzi hao.

Uchunguzi wa JAMHURI unaonesha kuwa kwa nguvu ya Khalfan Mrisho Kikwete, Simon Group ambayo haikuwa na ujuzi wowote katika uendeshaji wa biashara ya UDA, iliiwezesha kununua mali za Serikali kinyume cha sheria. UDA ilipoanzishwa mwaka 1974, Serikali iliamua hisa za UDA ziwe 15,000,000.

Wanahisa walipewa fursa ya kununua hisa zilizogawiwa katika thamani ya Sh 100 kila hisa na mwaka huo zilitolewa hisa 7,119,697, ambapo Jiji la Dar es Salaam lililipia asilimia 51 ya hisa hizo sawa na Sh 363,104,600, huku Msajili wa Hazina kwa niaba ya Serikali akilipia hisa asilimia 49 sawa na Sh 348,865,100.

Wataalamu wa masuala ya fedha wanasema thamani ya hisa ya Sh 100 mwaka 1974 (NPV) ni kubwa kuliko Sh 100 ya mwaka 2008. Awali, mwaka 1992 Sheria ya Mashirika ya Umma ilipotungwa, ilikuwa imebainisha kuwa shirika linatambulika kuwa la umma pale Serikali inapokuwa na asilimia 50 ya hisa. Kwa mantiki hiyo, kwa Serikali kumiliki asilimia 49, UDA ilipoteza sifa za kuwa Shirika la Umma, bali Serikali ilibaki kuwa mbia.

Sheria hii ndiyo iliyowapa fursa aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, aliyeshindwa ubunge Jimbo la Ubungo mwaka jana, Dk. Didas Masaburi, ambaye kwa kushirikiana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya UDA wakati huo, Iddi Simba, waliiuza UDA kwa Simon Group bila kuishirikisha Serikali. 

Simba aliwekewa Sh milioni 320 kwenye akaunti yake binafsi katika tawi la benki lililoko Makambako, Mkoa wa Njombe, kutoka kwa mnunuzi wa UDA ambaye ni kampuni ya Simon Group. Kisena alikiri kumpatia Simba fedha hizo akisema zilikuwa “gharama ya ushauri uliomwezesha kuinunua UDA.”

Ikumbukwe awali Iddi Simba mwaka 2001 alijiuzulu kutoka Serikali ya Rais Benjamin Mkapa, baada ya kukumbwa na kashfa ya kutoa vibali vya sukari kinyemela kwa waagizaji nje ya nchi. Kimakosa wiki iliyopita gazeti hili liliandika kuwa Iddi Simba alijiuzulu kwa ajili ya kashfa ya minofu ya samaki, lakini uhalisia ni kashfa ya vibali vya sukari.

Wakati Kisena katika barua yake kwenda kwa  Katibu Mkuu wa Usafirishaji (Miundombinu) isiyo na namba ya kumbukumbu ya Mei 24, 2011 akimjulisha kuwa yeye hadi wakati huo ndiye aliyekuwa mmiliki mkuu wa UDA, baada ya kununua hisa 7,880,303 sawa na asilimia 52.35 ya hisa zote za UDA kati ya hisa 15,000,000 za awali kwa gharama ya Sh milioni 285, uchunguzi unaonesha kinyume.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, aliliambia Bunge mwaka jana kuwa hisa za Serikali ndani ya UDA hazijauzwa. Malima alisema Serikali haitambui mauziano yoyote yaliyofanyika na hakuna nyaraka za kuonesha uuzwaji huo.

Barua nyingi za mawasiliano kati ya Simon Group, UDA na wizara mbalimbali za Serikali zinaonesha kuwa Msajili wa Hazina, ambaye ni mdhibiti wa mali za Serikali, hakushirikishwa katika vikao vingi – hakuwa akihudhuria. Badala yake, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Masaburi, ndiye aliyekuwa akitia saini nyaraka nyingi za kuidhinisha mauzo au kuvunjwa kwa Bodi ya UDA.

UDA ni shirika ambalo lilitengwa kwa ajili ya ubinafsishaji (specified) chini ya usimamizi wa Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) ambalo lilikuwa na jukumu la kuyaunda upya mashirika ya aina hiyo.

Kwa mantiki hiyo, CHC kwa niaba ya Msajili wa Hazina ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kuidhinisha uuzaji wa hisa za UDA na siyo Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kama ilivyofanyika, ingawa hoja hii waliipiga kumbo kwa kutumia Sheria ya Mashirika ya Umma ya Mwaka 1992 inayoitaka Serikali kumiliki asilimia 50 ya hisa kwa shirika kutambulika kama shirika la umma.

Julai, 2010, CHC iliishauri Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kupata idhini ya Serikali kabla ya kuendelea na uuzaji wa hisa za UDA. Imethibitika kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa UDA iliendelea na uuzaji wa hisa hizo bila kupata kibali cha Serikali.

Shirika Hodhi la Mali za Serikali lilitoa ushauri kwa Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kuwa njia ya wazi itumike kulingana na Sheria ya Ununuzi wa Umma kumpata mwekezaji bora katika Shirika la UDA. Bodi ilikiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004 inavyotaka.

Hisa za Shirika la UDA zilithaminishwa na kuwa Sh 744.79 kwa kila hisa Oktoba, 2009. Novemba, 2010 thamani ya kila hisa ikawa Sh 656.15. Hata hivyo, katika uuzaji huo, Bodi ya Wakurugenzi ya UDA ilitoa punguzo la asilimia 60 kwa kila hisa kwa mwekezaji huyo (kwa tathmini ya bei ya hisa ya Oktoba, 2009), bila kuwapo sababu za kufanya hivyo.

Kwa hiyo, kila hisa ilitakiwa kuuzwa kwa Sh 298 kutoka Sh 744.79 kwa hisa moja ambayo ilithaminishwa Oktoba 2009. Hatua hiyo iliifanya UDA ipate hasara ya Sh bilioni 1.559.

Vilevile. imebainika kuwa Bodi ya UDA iliingia mkataba wa kumuuzia mwekezaji hisa 7,880,303 ambazo hazikugawiwa kwa bei ya Sh 145 kwa jumla ya Sh bilioni 1.142 badala ya Sh 744.79 kwa hisa kulingana na ripoti ya mshauri ambako hisa hizo zingekuwa na thamani ya Sh bilioni 5.869. Hatua hiyo ililisababishia shirika hasara ya Sh bilioni 4.727.

Kwa kutumia bei ya hisa ya Sh 298 na 145 badala ya Sh 744.79 kwa hisa moja iliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 6.285 (Sh 1,558,694,380 + Sh 4,726,526,936).

 JAMHURI imeambiwa kuwa mnunuzi (mwekezaji) alilipa Sh 145 kwa hisa moja na kulipa jumla ya Sh milioni 285 kinyume cha thamani ya hisa ya Sh 744.79 au 656.15 kwa hisa moja.

 Mwaka 2011, Waziri Mkuu alimuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalum juu ya taratibu zilizotumika wakati wa uuzwaji wa hisa za UDA kwa mnunuzi wa hisa hizo na pia kufanya ukaguzi maalumu wa Menejimenti ya UDA.

Ukaguzi ulifanyika kutokana na maswali yaliyoibuka kwenye kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julai, 2011 kuhusiana na uuzwaji wa hisa za Serikali zilizokuwa katika UDA na uuzwaji wa hisa ambazo zilikuwa bado hazijatengwa kwa mwekezaji.

JAMHURI imewasiliana na Robert Kisena ambaye anasema kuwa yeye binafsi hamfahamu Khalfan Mrisho na kwamba UDA inamilikiwa kwa asilimia mia moja na familia yake.  Anaeleza kuwa umiliki wake ulianza tangu mwaka 2006 mkoani Mwanza na amekuwa akifanya kazi na wanafamilia katika kampuni hiyo ambao ni pamoja na mtoto wake, Gloria, na mke wake.

Aidha, anasema hata jina hilo la Simon limetokana na jina la baba yake mzazi ambaye ndiye mwenye jina hilo, hivyo suala la kampuni hiyo kuwa nje ya familia yake linamshangaza.

Aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi, kwa upande wake anasema kuwa mkataba wa uuzwaji wa UDA upo wazi na yeye binafsi hakuhusika na uuzwaji wake bali uongozi uliomtangulia ndiyo uliohusika.

Masaburi anasema Bodi ya Wakurugenzi ndiyo iliyouza UDA, hivyo anashangazwa kuhusishwa na uuzaji wa shirika hilo.

Akizungumzia taarifa kuwa hivi karibuni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inaandaa utaratibu wa kumhoji kuhusiana na sakata hilo, anasema anawakaribisha na atashukuru iwapo atahojiwa kuhusu sakata hilo.

“PCCB wakija nitashukuru sana ili niweze kueleza ninachokijua, ila wakija hao wanafiki wengine nitawafukuza maana mimi sipendi unafiki, nataka wakweli waje tu mimi nipo,” anasema Masaburi.

Juhudi za JAMHURI za kumpata Khalfani Mrisho Kikwete ziligonga mwamba na pamoja na kupitia kwa wapambe wake wa karibu inaonesha bado anayo nguvu ya aina yake katika kuhakikisha hafikiwi.

UDA sasa imeanzisha kampuni tanzu ya Mabasi Yaendayo Kasi (DART) jijini Dar es Salaam, ambayo mradi huo nao una mizengwe na inatajwa kudaiwa kodi katika mabasi yaliyonunuliwa.

Habari za uhakika kutoka Wizara ya Sheria na Katiba zinasema Serikali sasa inaendesha uchunguzi wa kina dhidi ya Simon Group na Iddi simba ambao pamoja na kesi yake kufutwa katika mazingira ya kutatanisha chini ya utawala uliopita, huenda wakati wowote kuanzia sasa kesi hiyo ikarejeshwa mahakamani.

4183 Total Views 2 Views Today
||||| 7 I Like It! |||||
Sambaza!