Waendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda jijini Dar es Salaam wamesema wananyanyasika kupita kiasi kutokana na kukamatwa hovyo na askari na watu wasiofahamu ni kina nani, hivyo wanaomba Rais John Magufuli aingilie kati kuwaokoa.

Wakizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki, wadereva hao wa pikipiki wamesema tofauti na ahadi ya Rais Magufuli kuwa wasibugudhiwe, mateso na manyanyaso yameongezeka asilimia 100 baada ya yeye kuingia madarakani.

“Tatizo ni kwamba tunakamatwa na askari, tunakamatwa na watu wasio na sare na ukikamatwa lazima utoe faini Sh 120,000 na ukikamatwa maeneo ya Posta unatozwa hadi 450,000 la ajabu hupewi risiti,” amesema Bilali Bakari Lukwello kwa masikitiko.

Lukwello aliyeambatana na Method Simon Ng’imba na Timothy Dede, walisema wakiwa katika eneo lao la kazi karibu na chuo cha ufundi stadi (VETA), karibu na ICD ya Masi Chang’ombe mara kadhaa wamewasikia askari na watu wanaowakamata wakikejeli kauli ya Rais Magufuli.

“Wanasema kutukamata na kutuondoa barabarani ndiyo maana ya ‘hapa kazi tu’. Kutokana na kamakamata ndiyo maana wengi wanapita ‘no entry’ kukwepa foleni kwani wanapokukuta kwenye foleni hata kama una vibali unakamatwa. Wakikukamata wanakupeleka yadi ya TAMESA, unatozwa 60,000 hadi 110,000 na ukipewa risiti ukifika mlangoni wanakunyang’anya hiyo risiti unarudishiwa pikipiki yako,” amesema Ng’imba na kuongeza kuwa hata risiti za elektroniki ukipewa baada ya nusu saa inafutika.

“Tunataka kauli ya Mheshimiwa Rais juu ya kamata kamata ya madereva wa pikipiki (bodaboda). Tuna wasiwasi na hawa wanaokamata hizi pikipiki (bodaboda) na hizo leseni za kukamata pikipiki anawapa nani. Je, na hizo pesa ambazo anatoa dereva wa bodaboda zinakwenda fungu gani? Je, na Serikali Kuu inatambua haya? Tunataka tupewe ufafanuzi juu ya haya maswala,” amesema Dede.

Naye Lukwello, aliendelea kusema: “Katika hotuba yako Mheshimiwa Rais ulizungumzia jambo la mama Lishe, Machinga na Bodaboda na tangu wakati huo sasa ni miezi miwili na nusu. Mheshimiwa hujazungumza jambo lolote tunazidi kuteseka tena imekuwa mara mbili ya mwanzo na watu wanakejeli kauli yako ya hapa kazi tu. Kwa nini hutoi tamko mara moja juu ya hawa watu wanaokamata au ndio mfumo wa Serikali?”

Amehoji ukamataji wa pikipiki ni “jipu la namna gani na kama ni la kawaida kwa nini linashindikana kutumbuliwa. Hili jipi ni la kampuni gani kwa maana haijulikani kwamba ni nani mwenye mamalaka halisi ya kulitumbua hili jipu.”

Dede kwa upande wake, akasema: “Na je, askari wa mabomu ya machozi wanahusika na nini kuhusu kamatakamata ya pikipiki? Je, na mheshimiwa Rais analitambua hilo askari wa mabomu anahusishwa na ukamataji wa pikipiki tena ni vinara wa rushwa?

“Je, na hizi notification tunazoandikiwa za 2007-2009 na za 2011, hizi ziko upande gani ni halali au tunaibiwa wananchi? Kuna ‘difenda’ ziko tatu na namba zao tunazo na madereva wake majina tunayo zile ‘difenda’ zinazunguka ndani ya city centre kwa ajili ya kukamata pikipiki tu

“Hawajihusishi na mambo ya kukamata vibaka wao kazi yao ni kukamata pikipiki na vibaka wanakwapua mali za raia pochi, simu, lakini ile ‘difenda’ inazunguka na kuwasha taa na huku inatembea.

“Hii gari haisaki wahalifu bali inawapita na kukimbizana na pikipiki na hata kama imeegeshwa pembeni pikipiki inakamatwa. Pia hawatumii ukamataji salama wanakusukuma tu na imechangia watu kuvunjika miguu na wengine kufa.”

Waendesha Bodaboda hao waliosema wamejitokeza kuwasemea wenzao juu ya mateso wanayopata na kuomba kukutana na Rais Magufuli wameleze kilio chao, wameomba namba na majina yao yachapishwe kurahisisha mawasiliano kwa kiongozi mwenye nia ya kuwasaidia kwani wao wako tayari kueleza manyanyaso wanayopewa. “Pie ieleweke, tuko tayari kufuata sheria tukiwekewa utaratibu wa wazi badala ya kuviziwa kama ilivyo sasa,” amesema Lukwello.

Majina ya waendesha bodaboda hao na namba zao kwenye mabano ni Timotheo E. Dede (0757-398847), Ramadhan  Issa  Juma (0714- 373836), Bilali  B. Lukwello (0684- 639423), Method  S. Mgimba (0679- 391335) na Jimi K. Omary  (0657- 088559). Wanaomba viongozi wawasaidie kuweka utaratibu wa uendeshaji wa pikipiki Dar es Salaam.

By Jamhuri