MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amesema Spika Anne Makinda, asipodhibitiwa, ataiua nchini kutokana na uongozi wake wa kiimla.

Amesema Makinda ameligeuza Bunge na kuwa kibogoyo, huku akionekana wazi kuibeba Serikali; jambo ambalo amesema ni hatari kwa kustakabali wa nchi. Kauli ya Zitto imekuja baada ya Spika huyo kuivunja Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na mwanasiasa huyo kijana.


“Kwa vyovyote vile Spika wa Bunge amedhihirisha namna ambavyo anafanya uamuzi bila kuzingatia masilahi ya nchi wala kuzingatia historia ya uwajibikaji katika nchi.


“Namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna anavyofanya uamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya uwajibikaji wa nchi.


“Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia.”


Zitto ameendelea kusema, “Katika Mkutano wa Kumi wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Spika wa Bunge ndugu Anne Makinda alitangaza mabadiliko kadhaa ya muundo wa Bunge katika Kamati mbalimbali za Bunge. Moja ya uamuzi wa Spika ulikuwa ni kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ambayo inajulikana kifupi kama POAC. Uamuzi huu umeleta sintofahamu kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala ya Bunge na Uwajibikaji katika nchi yetu.


“Ni muhimu tufahamu uundwaji wa POAC ulitokana na misingi gani na kwamba uamuzi wa Spika unarudisha nyuma maendeleo makubwa ya kujenga Bunge imara na lenye meno. Uamuzi wa Spika ni kinyume cha Kanuni za Bunge, Sheria ya Ukaguzi na Katiba ya nchi. Uamuzi wa Spika unavuruga Bunge, ni ya hovyo na unapaswa kupingwa na kila mdau wa uwajibikaji nchini.


“Baada ya Tanzania kuingia kwenye ubinafsishaji, mashirika mengi ya umma yaliuzwa na mengine kufa kabisa. Wakati huo kulikuwa na chombo kinaitwa SCOPO (Standing Committee on Parastatal Organisations) kwa madhumuni ya kusimamia uendeshaji wa mashirika ya umma. Bunge lilikuwa na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na kamati hiyo ilifutwa mwaka 1997 kutokana na hatua za ubanifsishaji na ukweli kwamba mashirika ya umma hayatakuwapo na hivyo hapakuwa na haja ya kuwapo kwa kamati hiyo. Mwenyekiti wa mwisho wa Kamati hiyo alikuwa ni Mzee William Shellukindo wakati huo akiwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga.


“Mwaka 2007, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya mkutano wa Uwajibikaji na kueleza Taifa kuwa kimsingi mashirika ya umma bado yapo na hesabu zao, kwa kuwa haziangaliwi, ni mabaya sana na fedha za umma zinapotea. Pia alieleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 143(5) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kutoa taarifa za Ukaguzi za Mashirika ya Umma (Public Authorities and Other Bodies).


“Hivyo aliomba Bunge liunde Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma ili liweze kupokea, kujadili na kutoa maelekezo kuhusu hesabu za mashirika ya umma na kusimamia ufanisi wa mashirika hayo. Vile vile alishauri Kamati hiyo isimamie Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma. Spika wa Bunge wa wakati huo, kupitia Kamati aliyoiunda chini ya Job Ndugai (wajumbe wengine walikuwa Dk. Wilbrod Slaa, Beatrice Shelukindo, Hamad Rashid Mohammed na Nimrod Mkono) wakaunda Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kanuni za Bunge za Mwaka 2007.


“Kamati ya POAC iliundwa rasmi mwaka 2008 mwezi Februari. Nilipewa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati hii. Sababu za kuanzishwa kwa Kamati ya POAC bado zipo na kimsingi sababu hizo ni za maana sana sasa kuliko ilivyokuwa kabla.


“Majukumu ya POAC yaliainishwa na sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007, kanuni ya 115 (13) (a-e). Majukumu hayo ni pamoja na kushughulikia hesabu zilizokaguliwa za mashirika ya umma, kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma, kutathimini ufanisi wa mashirika ya umma na kufuatilia utekelezwaji wa sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma.


“Kuanzia mwaka 2008 Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa taarifa za hesabu za mashirika kama Katiba ya nchi inavyomtaka na Sheria ya Ukaguzi ya mwaka 2008. Sheria hii imeitaja Kamati ya POAC kama moja ya kamati zenye majukumu ya kuwasilisha bungeni taarifa ya mwaka ya hesabu za mashirika ya umma.


“Katika kipindi cha miaka mitano POAC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa umahiri na kwa kweli kwa uwazi sana kuliko Kamati nyingine zote za Bunge. Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge iliyowasilishwa katika Mkutano wa Saba wa Bunge, Aprili mwaka 2012 iliwezesha kutolewa kwa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo ilisababisha mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.


“Hatua hii ilikuwa ni hatua muhimu sana katika kuweka mizizi ya utamaduni wa uwajibikaji nchini kwetu. Wakati Kamati inajiandaa na taarifa yake ya Mwaka 2012 kwenye Mkutano wa Kumi na Moja, Spika ameivunja.


“Ikumbukwe maagizo ya mwisho ya Kamati ya POAC yalikuwa ni kuzuia mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa mikopo kwa Serikali bila ya kuwapo kwa mikataba. Hivi sasa Serikali imekopa shilingi zaidi ya trilioni 1.2 kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii kwa ajili ya miradi mbalimbali, mikopo hiyo ya fedha za wafanyakazi haina mikataba yoyote; na POAC iliona hatari ya fedha za wafanyakazi kupotea na kuleta madhara makubwa kwa wastaafu nchini.


“Katika maelezo yake, Spika amesema nchi nyingine duniani hazina Kamati kama ya POAC. Nadhani waliomshauri Spika waliamua kumdanganya na yeye akadanganyika. Nchi zote za Afrika Mashariki zina kamati ya kusimamia mashirika ya umma.


Kenya inaitwa Public Investments Committee, Uganda inaitwa State Corporations Committee na hata nchi nyingine kama India ambazo zinafuata utamaduni wa kibunge kama wetu wanayo na wanaita Public Undertakings Committee. Nchini Afrika Kusini sio tu kuna Kamati ya Mashirika ya Umma, bali pia kuna wizara inayosimamia mashirika ya umma (Ministry of Public Enterprises).


“Kimsingi Kamati ya POAC ilipaswa kuongezewa nguvu zaidi ili kufikia uwezekaji wa Serikali kwenye kampuni binafsi badala ya kuifuta. Uwezekaji wa Serikali kwenye kampuni kama BP, AirTel, Kilombero Sugar, SonGas nk. hauna uangalizi wowote.


“Uamuzi wa Spika wa Bunge kuifuta Kamati ya POAC ni uamuzi unaorudisha nyuma juhudi za nchi kujenga asasi za uwajibikaji, ni kinyume cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma inayotaja Kamati tatu za Bunge za kusimamia fedha za umma na ni kinyume cha Katiba ya nchi. Spika wa Bunge anasema kazi za Kamati ya POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania ina jumla ya mashirika ya umma 258 yenye thamani ya Sh trilioni 10.2 mpaka Juni mwaka 2012. Hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi kushughulikia mashirika yote ya umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje kusimamia wizara za Serikali, mikoa na wakala za Serikali na wakati huo huo mashirika ya umma 258?


“Kwa vyovyote vile Taifa linarudi miaka ya kabla ya 2008 ambako mashirika ya umma yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za umma. Hivi karibuni Kamati ya POAC iligundua mtindo wa wizara za Serikali kupeleka fedha za Serikali kwenye mashirika na kuzitumia kifisadi ili kukwepa ukaguzi kwenye wizara (Wizara ya Maliasili na Utalii ilipeleka zaidi ya Sh milioni 600 Bodi ya Utalii mwaka 2010/2011). Ikumbukwe pia wizi wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji holela wa baadhi ya mali za Serikali kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati ambazo Bunge halina kamati inayosimamia mashirika ya umma.


“Kwa vyovyote vile Spika wa Bunge amedhihirisha namna ambavyo anafanya uamuzi bila kuzingatia masilahi ya nchi wala kuzingatia historia ya uwajibikaji katika nchi. Namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna anavyofanya uamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya uwajibikaji wa nchi.


“Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia.”


By Jamhuri