Tanzania imejaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na rasilimali lukuki za kila aina. Rasilimali hizi ni pamoja na wanyama, milima, ardhi nzuri, mito, watu, maziwa, ndege, bahari, samaki na madini ya aina mbalimbali.

Asilimia 63 ya Watanzania wanapata mahitaji yao kutokana na shughuli zinazotegemea mazingira. Asilimia 66 ya Pato la Taifa linatokana na shughuli zinazohusiana na mazingira, kikiwamo kilimo, uvuvi, ufugaji na usafirishaji.


Ziwa Victoria lililopo Kanda ya Ziwa ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya maendeleo ya nchi yetu, na hata nchi nyingine kama vile Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya na Misri inayopata huduma ya maji ya Mto Nile unaoanzia kwenye ziwa hili la kwanza kwa ukubwa barani Afrika na la pili kwa ukubwa duniani.


Licha ya haya yote, uchafuzi mkubwa wa mazingira unaosababishwa na shughuli za binadamu, umechangia kwa kiwango kikubwa kupungua kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria lenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya 68,100.


Kutokana na kukithiri kwa uchafuzi wa mazingira, utafiti wa kitaalamu unathibitisha kwamba samaki wamepungua kutoka kati ya tani 400,000 na 500,000 hadi tani 243,564 kwa mwaka 2010, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita.


Chanzo cha rasilimali hii kupungua katika Ziwa Victoria, linatajwa kuwa ni mojawapo ya uchafuzi mkubwa wa mazingira. Hii inatokana na ukweli kwamba asilimia 80 ya maji ya ziwa hili yanatokana na mvua.

Vijito vingi vidogo navyo vinachangia asilimia 20 katika kuingiza maji kwenye bonde hili. Mto mkubwa unaoingiza maji kwenye ziwa hili, ni mto Kagera unaotiririka kutoka upande wa magharibi mwa nchi.


Kimsingi, kuanza kupungua kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria lenye kina cha wastani wa mita 40 (futi 130), na mwambao wa urefu wa mita 4,828 (maili 3,000), kunatokana na Serikali ya Tanzania inayomiliki eneo kubwa la ziwa hili, kuonekana kuzembea katika kutoa elimu kwa raia wake kuhusu athari za uchafuzi wa mazingira.


Yawezekana kabisa Serikali imeshindwa kusimamia sheria zilizopo, hasa Sheria ya Mazingira Na 20 ya Mwaka 2004, na Sheria ya Rasilimali za Maji ya mwaka 2009 Na 11.


Serikali yetu kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilitunga na kupitisha Sheria Na 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira.


Pamoja na sheria hizi kuwa na vifungu vinavyotaka mchafuzi wa mazingira akamatwe na kutozwa faini ya Sh milioni moja, au kwenda jela mwaka mmoja, bado zinaonekana kupuuzwa. Hili ni tatizo kubwa kwa nchi yetu iliyoridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu utunzaji wa mazingira.


Kwa mantiki hiyo, iwapo Tanzania na mataifa mengine jirani ya Kenya na Uganda hayatachangamka kusimamia kikamilifu sheria kwa kudhibiti uchafuzi huu mkubwa wa mazingira, rasilimali za samaki na viumbe wengine adhimu ndani ya ziwa hili vitapotea. Naam, vitapotea na kubaki historia tu!


Ni dhahiri, kama imefikia kiwango cha kushuka kutoka kati ya tani 400,000 na 500,000 za samaki kufikia tani 243,564 mwaka 2010, tunakoelekea ni kubaya zaidi. Tutapoteza kabisa samaki ndani ya Ziwa Victoria iwapo Serikali yetu haitasimamia vema sheria zake.


Naungana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Christopher Sayi, ambaye ameweka wazi kwenye taarifa yake wakati alipozuru jijini Mwanza hivi karibuni kwamba, matumizi ya mazingira yasiyo endelevu yana madhara makubwa kwa jamii.


Mfano, ongezeko la idadi ya watu limekuwa na athari kubwa kwa mazingira ya nchi. Hii inatokana na maisha ya binadamu kutegemea mno rasilimali za asili ambazo haziongezeki.


Bila udhibiti madhubuti, ziwa hili linaweza kupungua maji yake kama ilivyowahi kutokea miaka ya 2000 na 2004, ambapo yalipungua kwa kiasi cha mita 1.9.


Serikali yetu imejizatiti kuanzisha miradi ya kijamii takribani 126, kupitia chombo chake cha Hifadhi ya Mazingira Ziwa Victoria (LVEMP II). Miradi hii isimamiwe kikamilifu. Watendaji watakaoonekana kuihujumu miradi hii wakamatwe na kushitakiwa mahakamani.


Lakini, miradi hiyo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), chini ya maridhiano ya utekelezaji wa MoU isimamiwe vizuri iweze kusaidia kuboresha maisha ya Watanzania. Tunahitaji kuona maendeleo na si porojo zisizo na maana kutoka kwa viongozi wa Serikali yetu.

 

Serikali ishirikiane na wananchi kutunza mazingira. Lazima tushirikiane kutunza ardhi oevu na kuhakikisha shughuli zote za kilimo na ufugaji zinatekelezwa kwa kufuata taratibu zilizopo ili kulinda bioanuwai.

Tushirikiane kuijenge Tanzania yetu.

0777 068270

By Jamhuri