Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo wa 14 amelalalamikia mizozo iliyotawaliwa na umwagaji damu inayoendelea duniani na kusema kuwa inahatarisha mustakabali wa ubinadamu.

Papa Leo ameeleza kuwa dunia inayumba kutokana na tamaa na kuchagua mambo yanayodidimiza haki na amani. Ameyasema hayo akiwa ziarani Uturuki ambako amekutana na kuzungumza na Rais Recep Tayyip Erdogan.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani pia ameitolea wito Uturuki kulifurahia jukumu lake kama msuluhishi wa mataifa  katika juhudi za kutafuta amani ya kudumu.

Kwa upande wake Rais Erdogan ameusifu msimamo wa Papa Leo kuhusu suala la Palestina baada ya mkutano wao. Erdogan amesema ana matumaini kuwa ziara hiyo ya kwanza ya Kimataifa ya Papa, itakuwa ya manufaa kwa utu wakati kukiwa na mivutano na hali ya mashaka ulimwenguni.