Na Cresensia Kapinga, Jamuhuri,Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linawashikilia watu 15 kwa tuhuma za mauaji ya Watu watano na wengine watatu kujeruhiwa katika tukio la mapigano ya wakulima na Jamii ya wafugaji.
Watuhumiwa waliokamatwa majina yao yamehifadhiwa ambao wanaendelea kuhojiwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo ambapo amewataja waliouawa ni Mfaume Machaka Ally (68), Imani Said Kosa(50),Abdallah Ally Biashara (37),Mipango Mwituta(54) na Hamis Shaibu(13) walikutwa maeneo tofauti tofauti wakiwa wameuwawa kwa kukatwa na kuchomwa na vitu vyenye ncha Kali sehemu mbalimbali za miili yao.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya alisema kuwa tukio hilo limetokea Oktoba 1 mwaka huu majira ya saa 7 usiku huko katika kitongoji cha Likologo,kijiji cha Wenje kata ya Nalasi Magharibi wilayani Tunduru.
Alifafanua zaidi kuwa inadaiwa chanzo cha tukio ni kwamba tarehe 30 Septemba 2025 majira ya saa 11 joini mwananchi mmoja Hassan Mponda Moshi mkazi wa Kijiji cha Nakapunda akiwa shambani kwake alishambuliwa na mfugaji ambaye jina lake halijafahamika, ambapo kufuatia tukio hilo ndipo Oktoba 1 mwaka huu majira ya saa 7 usiku wananchi wa kijiji cha Mkapunda na Wenje wapatao 100 waliwafuata wafugaji kwenye makazi yao huko katika kitongoji cha Likologo,kijiji cha Wenje ambapo waliwakuta wafugaji lakini walikimbia na kuacha mifugo yao ndipo wananchi hao waliwafungulia Ng’ombe wote zizini kisha kuanza kuwakatakata kwa mapanga, ngozi na kuchukuwa mnyama.
Alieleza zaidi kuwa wakati wananchi hao wakiwa wanarudi nyumbani na mizigo ya nyama ghafla walijikuta wakiwa wamezingirwa na wafugaji kisha kuanza kushambuliwa kwa siraha za jadi mikuki,mapanga na kupelekea vifo vya watu watano na kusababisha majeruhi kwa wakulima watatu ambao ni Jana Said Athumani (46),Alifa Salum Mbahu(49) na Mahala Rajabu Mahala (56)mbao wamelazwa katika katika hospitali ya Mission Mbesa ambako wanaendelea kupatiwa matibabu na miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Kufuatia tukio hilo polisi inaendelea kufanya upelelezi wa kina pamoja na msako wa kuwasaka wale wote ambao wamehusika na tukio hilo na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
