Na Issa Mwadangala- Jeshi la Polisi
Wananchi, wachimbaji wa madini na wafanyabiashara Wilaya ya Songwe wametakiwa kuhakikisha wanalinda amani ikiwa ni pamoja na kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 29, 2025 kwa amani, utulivu na kuzingatia sheria za nchi.
Rai hiyo imetolewa Agosti 07, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Saza Wilaya na Mkoa wa Songwe na kuwasisitiza wananchi hao kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo kila mwananchi ana jukumu la kuilinda hasa katika kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu.
Aidha, katika mkutano Kamanda Senga aliwataka wananchi hao kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu wahalifu na vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali zao, huku akibainisha kuwa ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha uhalifu unatokomezwa na jamii inaendelea kuwa salama kwa ustawi wa maendeleo ya taifa letu.

“Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda raia na mali zao, ili kufanikisha hilo tunaomba ushirikiano wa karibu na wananchi kwani taarifa ni muhimu sana katika kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema Kamanda Senga.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya Mkoa huo, hasa kuelekea kipindi cha kampeni na uchaguzi mkuu, kwa kuhakikisha wananchi wanatekeleza haki zao za kidemokrasia katika mazingira ya utulivu na amani.

