▪️Waziri Mavunde aweka jiwe la Msingi wa Ujenzi wa Maabara ya kisasa

▪️Ni maabara kubwa ya uchunguzi wa sampuli za madini Afrika Mashariki

▪️Kugharimu Tsh Bilioni 14.3

▪️Rais Samia atajwa kinara wa mageuzi sekta ya madini

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Tanzania imeanza ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini ambayo itakuwa ni kubwa kuliko zote kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati na ambayo itatoa huduma ya kimaabara kwa ubora na kwa uharaka kwa wadau wa sekta ya madini nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini katika eneo la Kizota,Jijini Dodoma.

“Tunamshukuru Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuwa kinara wa mageuzi makubwa ya sekta ya madini na kwa kuandika historia ya ujenzi wa maabara hii ya kisasa miaka 100 baadaye tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini(GST) mwaka 1925.

Leo tunaandika historia kuanza kwa ujenzi wa maabara kubwa ambayo itafungwa mitambo na vifaa vya kisasa katika kutoa huduma za kimaabara ndani na nje ya nchi.

Huu ni ukombozi mkubwa kwa wadau wa sekta ya madini katika kupata taarifa sahihi za kimaabara kwa wakati na zenye ubora wa hali ya juu.

Ni imani yangu maabara hii itachochea ukuaji na maendeleo ya sekta ya madini”Alisema Mavunde.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini(GST) Dkt. Notka Huruma Batenze amesema Maabara hiyo ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini utaleta tija kwa wadau wa sekta ya madini na kurahisisha upatikanaji wa huduma hii muhimu kwa maendeleo ya sekta ya madini.

Gharama za ujenzi wa maabara hii unatarajiwa kuwa Tsh Bilioni 14.3 na muda wa ujenzi wa kukamilika maabara ni siku 690.