Na: OWM–TAMISEMI, Mbeya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameelekeza kuundwa kwa timu itakayozunguka Jiji la Mbeya kufanya tathmini ya maeneo watakayotumia madereva wa bajaji, njia watakazotumia, njia za daladala pamoja na kupendekeza njia za usafiri zitakazowawezesha abiria kufika katika eneo la uwanja wa ndege wa zamani, ambako soko la Wamachinga litajengwa.

Prof. Shemdoe amesema uundaji wa timu hiyo ni hatua ya kutatua mgogoro baina ya madereva wa bajaji na daladala uliopelekea kuibuka kwa mgomo wa madereva hao na kusababisha kusimama kwa huduma za usafiri jijini Mbeya, na kuongeza kuwa mgomo huo ulitokana na uongozi wa mkoa kutowashirikisha kikamilifu madereva wa bajaji katika kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha usalama wa madereva hao.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo, Oktoba 22, 2026, jijini Mbeya kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Jumanne Sagini, ya kuunda timu hiyo baada ya kufanya kikao na makundi husika. Amemtaka timu hiyo iwe na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, LATRA, Halmashauri ya Jiji, wamachinga, madereva wa bodaboda, bajaji na daladala, na kuwasilisha taarifa ndani ya siku 14 ili kuwezesha kutatuliwa kwa changamoto iliyojitokeza jijini Mbeya.

“Timu hiyo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, uiandalie hadidu za rejea, lakini miongoni mwa kazi zinazotakiwa kufanywa ni kuzunguka mji wote wa Mbeya ili kuangalia bajaji zitakaa wapi, daladala zitapita wapi, pamoja na kuandaa njia za usafiri za kuja hapa katika eneo ambalo soko la wamachinga litajengwa,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Kutokana na hatua hiyo, Prof. Shemdoe na wawakilishi wa madereva wa bajaji wamekubaliana kuwa madereva hao warejee kazini na kuwa tayari kwa utaratibu utakaowekwa na Serikali ili waendelee kutoa huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Jiji la Mbeya.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Madereva wa Bajaji, Bw. Damas Mwakalinga, amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kusikiliza hoja zao na kusema kuwa wako tayari kushirikiana na Serikali ili kumuunga mkono Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Mkoa wa Mbeya unakuwa salama na unaendelea kudumisha amani.