Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahamoud Thabit Kombo amewasili nchini Singapore kwa ziara ya kikazi inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 25 -29 Agosti 2025.
Akiwa katika ziara hiyo Waziri Kombo atashiriki katika matukio mbalimbali ya kimkakati ikiwemo; Mkutano wa 5 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Singapore (5th Singapore-Africa Ministerial Exchange Visit – SAMEV); Kongamano la 8 la Biashara kati ya Afrika na Singapore (8th Africa Singapore Business Forum -ASBF), kushiriki kongamano la Wafanyabiashara wa Tanzania na Singapore na kufanya mazungumzo ya uwili na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu Serikali ya Singapore na sekta binafsi.
Waziri Kombo katika ziara hiyo ambayo imebeba dhima ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ameambatana na ujumbe wa Wafanyabiashara, ikikusudia kuongeza wigo wa fursa za kiuchumi huku ikitilia mkazo zaidi katika nyanja za biashara na uwekezaji, uchumi wa bluu, teknolojia, nishati jadidifu, utalii na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia.
Aidha, Waziri Kombo atatumia mkutano huo kunadi nafasi ya Tanzania ikiwa kama lango la biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nchini Singapore. Mawaziri kutoka nchi 16 wanashiriki mkutano huo.
Tanzania na Singapore zimekuwa na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia na kiuchumi ambapo Tanzania imekuwa ikiuza nchini humo bidhaa mbalimbali ikiwemo mazao ya mbogamboga na matunda, kahawa, karafuu, madini na samaki. Vilevile Singapore imekuwa ikiiuzia Tanzania bidhaa mbalimbali ikiwemo za kielektroniki, magari, vifaa vya matibabu na madawa, vipuli vya magari na mitambo ya kuendesha viwanda.
Takwimu kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) zinaeleza kuwa kuanzia mwaka 1997 hadi Julai 2025, jumla ya miradi 36 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 535.13 imesajiliwa hapa nchini kutoka Singapore, ikikadiriwa kutengeneza ajira 3,228. Sehemu kubwa ya uwekezaji huo umejikita katika sekta ya viwanda, ikiwa na jumla ya miradi 21 kati ya 36.
Mhe. Waziri Kombo amepokelewa na Balozi Macocha Tembele, Balozi anayeiwakilisha Tanzania nchini Singapore ambaye ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Said Shaib Mussa, Wafanyabiara na Maafisa Waandamizi.
