·       Asema Mahakama haitosita kusimamia sheria dhidi ya waajiri wanaokiuka masharti ya sheria

·       Wafanyakazi nao wasisitizwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo bila kusukumwa na kuwa na ujasiri ili kutoa taarifa za ukiukwaji wa sheria za usalama mahala pa kazi na taarifa muhimu nyinginezo

Na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju amekemea vikali tabia ya baadhi ya Waajiri nchini kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii PSSSF na NSSF hali inayosababisha usumbufu kwa waajiriwa na kufunguliwa kwa mashauri mengi yanayotokana na migogoro ya kazi.

Akizungumza leo tarehe 25 Agosti, 2025 wakati akifungua Mkutano wa Tisa wa Kamati ya Utatu (Tripartite Users Committee) unaofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini Dar es Salaam, Mhe. Masaju amesema kuwa, ni muhimu kwa Waajiri kuthamini maslahi ya wafanyakazi na kuthamini ubinadamu wao badala ya kujikita katika kutaka kutengeneza faida pekee.

“Mifuko ya Hifadhi ya Jamii PSSSF na NSSF ipo kwa ajili ya kuwalinda wafanyakazi wanapofikia uzee au wanapopata majanga kama ulemavu, au hata kwa familia zao baada ya kifo hivyo inasikitisha kuona baadhi ya waajiri wanakata michango ya wafanyakazi lakini hawawasilishi kabisa au wanachelewesha kuwasilisha kwenye mifuko husika. Hili ni kosa la kisheria, na ni dhuluma kwa mfanyakazi. Kwa hiyo, waajiri wote: Lipeni madeni ya michango mara moja na wasilisheni kwa wakati michango ya kila mwezi” amesema Jaji Mkuu

Kadhalika, amewasihi baadhi ya Waajiri ambao bado hawajajisajili kwenye kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wajisajili kwa manufaa ya wafanyakazi.

“Waajiri endeleeni kujali maslahi ya ubinadamu wa wafanyakazi na sio faida tu mnazopata, nanyi Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) ongezeni bidii katika ukaguzi ili kulinda afya za wafanyakazi na waelimisheni watumishi kuhusu sheria ya OSHA, wafanyakazi wapewe mafunzo ya mara kwa mara,” amesema Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu amesema kuwa, hivi karibuni atarekebisha Kanuni za Uendeshaji wa Sheria ya Madai (Kanuni ya XXXV) ili madai ya NSSF yaweze kusikilizwa na kutolewa uamuzi wa haraka yaani summary proceedings / summary suit, njia ambayo haitumii mlolongo mrefu wa mashauri ya Madai.

Jaji Masaju vilevile ameishauri Mifuko ya Hifadhi kuwasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka kwani kutokulipa michango ya wafanyakazi kunakofanywa na Waajiri kunaweza vilevile katika mazingira fulani kutafsiriwa kukiuka aya ya 10 ya Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi [Sura ya 200 Marejeo ya 2023] ambayo inatengeneza kosa la kuisababishia mamlaka husika hasara.

Aidha, Jaji Mkuu ametoa rai pia kwa Wafanyakazi waliopo Serikalini na katika Sekta Binafsi kufanya kazi kwa bidii sambamba na kudumisha nidhamu kazini bila kulazimika kusimamiwa au kusukumwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Heshimuni Sheria ya Usalama kazini na tambueni haki zenu. Watu wa utawala msiwakandamize wafanyakazi bila kuwajulisha haki zao, Kwa wafanyakazi; tambueni haki zenu. ulizeni, fuatilieni, hakikisheni kuwa michango yenu inaenda mahali sahihi. Hifadhi ya jamii ni msingi wa utu. Tuendelee kuwa taifa la haki, linalothamini binadamu kabla ya faida,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Aidha, Mhe. Masaju ametoa rai kwa Waajiri kuhakikisha wanatekeleza viwango vya usalama kazini kulingana na sheria, kuwapa wafanyakazi mafunzo ya usalama mara kwa mara kuwasiliana, kuheshimu maelekezo ya usalama kazini na kutoa taarifa za ukiukwaji wa usalama kwa usiri na ujasiri na OSHA kwa ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini hatari mapema.

Kadhalika, Jaji Mkuu amempongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama mahala pa Kazi kwa kuingia mkataba na Mahakama wa kutoa mafunzo ya miaka miwili kwa Maafisa wa Mahakama na wadau wake kote nchini, jambo ambalo linadhihirisha dhamira ya dhati ya Mhhimili wa Mahakama na Serikali katika kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi.

Jaji Mkuu alimshauri Mtendaji Mkuu wa OSHA kuangalia namna nyingineyo ya kuisaidia Mahakama kwa kuwanunulia vyombo vya usafiri kama pikipiki Mahakimu walioko katika vituo vya mbali, kompyuta mpakato, au kuangalia vilevile kama wanaweza kujenga majengo ya Mahakama.

Mhe George Masaju vilevile alizungumzia kuhusu nguzo tatu za Dira ya Maendeleo ya Taifa ambapo alisema nguzo ya kwanza ya Dira hiyo inagusia kuhusu uchumi imara jumuishi na shindani na kusisitiza kuwa, kwa vile tunataka kuwa na uchumi jumuishi ni lazima vilevile kujiuliza walemavu wanawasaidiaje kwenye uchumi huo jumuishi kama Dira ya Taifa ya Maendeleo inavyotaka.

“Ushirikiano huu ni utekelezaji wa Nguzo ya Tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya mwaka 2020/2021 – 2024/2025, inayolenga kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama pamoja na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama. Nimefurahi zaidi kuona mpango huu wa mafunzo unahusisha Watumishi wenye ulemavu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na Mahakama,” ameeleza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF kwa kuendelea kushirikiana kikamilifu na Mahakama ya Kazi ambapo amesema, “natambua ushirikiano wenu katika mambo mbalimbali ikiwa pamoja na mafunzo kwa watumishi wa Mahakama.”

Kwa upande mwingine, Jaji Mkuu amesema Utatu ni nguzo muhimu katika kutekeleza, kusimamia na kutafsiri sheria za kazi hivyo, ushirikiano wa wadau wa utatu ni wa msingi katika kuongeza ufanisi na tija ya Mahakama za Kazi.

Akizungumzia kuhusu Kaulimbiu ya Mkutano huo isemayo: “Mchango wa Wadau wa Haki Kazi katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050”, Jaji Mkuu amesema kuwa, ili Taifa liweze kufikia malengo ya Dira hiyo ni muhimu kutambua kwamba kazi ni uti wa mgongo wa maendeleo ya mtu mmoja  na taifa kwa ujumla, hivyo Wadau wa Haki wanapaswa kujituma kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia sayansi na teknolojia katika kuboresha utendaji kazi katika sekta mbalimbali ikiwemo  kilimo, viwanda, biashara, afya, elimu  na sekta muhimu katika utoaji wa huduma ikiwemo wadau wa haki kazi ili kutengeneza Uchumi jumuishi na shindani.

“Tuitumie vyema fursa hii kutoa maoni na ushauri ili kuisaidia Serikali na wadau wengine kuimarisha utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Dira ya 2050,” amesisitiza Mhe. Masaju.

Ameongeza kuwa, anaamini  mkutano huo ni wakati mzuri wa kuangalia namna ya kutengeneza ajira nyingi na bora zaidi haswa kwa vijana, kupanua wigo wa huduma za Hifadhi ya Jamii, na kukuza vyama vyenye nguvu na uwakilishi wa waajiri na wafanyakazi.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amelishukuru Shirika la Kazi Duniani kwa kufadhili mafunzo mbalimbali kwa Majaji yakiwemo ya hivi karibuni yaliyowahusisha Majaji Wafawidhi wote jijini Arusha.

Katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo Jaji Mkuu amezindua Juzuu mbili za maamuzi ya Mahakama Kuu kuhusu migogoro ya kazi nchini. Ya kwanza ikiwa ni ya kipindi cha 2010 hadi 2022, na ya pili ikihusu miaka ya 2023 hadi 2024.

“Natambua pia ILO wamekuwa wakifadhili uaandaaji na uchapishaji wa High Court Labour Law Compendium. Tangu mwaka 2023 ILO kwa kushirikiana na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi mnaandaa Juzuu. Mlianza na ile ya Mahakama ya rufani, na sasa za Mahakama Kuu. Hakika Uongozi mahiri wa ILO unaacha alama kubwa kwa Mahakama ya Tanzania.

Ameongeza kuwa, anatarajia zitachapishwa nakala za kutosha kila Jaji nchini na wadau wa haki kazi kupata nakala ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Kamishna wa Kazi, Shule ya Sheria, Vyuo Vikuu vinavyofundisha sheria nchini, IJA, Maktaba ya Taifa, Government printers, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali na wengineo.

Katika hafla hiyo ya ufunguzi wa Mkutano huo, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju amekabidhiwa Tuzo Maalum ya kutambua mchango wake na ushirikiano wake katika kukuza mazungumzo ya kijamii na kukuza Haki ya Kazi nchini.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju akifungua Mkutano wa Tisa wa Kamati ya Utatu (Tripartite Users Committee) leo tarehe 25 Agosti, 2025 kwenye Ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini Dar es Salaam.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (kushoto) akipokea tuzo maalum aliyopatiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika sekta ya haki.