Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, Mheshimiwa Misana Majura, mnamo Septemba 4, 2025, alitoa hukumu katika shauri la jinai namba 4719/2025, ambapo Jamhuri ilimshtaki Bw. Jafari Hamisi Fadhili kwa makosa mawili ya kuomba na kupokea rushwa kinyume na Kifungu cha 15 (1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, marejeo ya mwaka 2024.
Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa na Waendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Bw. Amrani Buyege na Bi. Mwasiti Mshana, mshtakiwa akiwa Afisa Mtendaji wa kujitolea katika Kijiji cha Mgambazi, Wilaya ya Uvinza, alionekana kuomba rushwa ya shilingi milioni 3 kutoka kwa Bw. Pascal Donald Lala ili kumrudishia hati ya shamba lake.
Aidha, ilibainika kuwa Januari 5, 2025, mshtakiwa alipokea sehemu ya fedha hizo, kiasi cha shilingi 500,000, ambazo zilikuwa fedha ya mtego kutoka kwa mlalamikaji.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mahakama ilimtia hatiani Bw. Fadhili na kumhukumu kulipa faini ya shilingi 500,000 kwa kila kosa, au kutumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa. Hata hivyo, mshtakiwa alilipa faini jumla ya shilingi milioni 1 kama mbadala wa kifungo.
