Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MKAZI wa Jiji la Tanga, Fahad Soud, ameibuka mshindi wa pili wa gari jipya aina ya IST kupitia kampeni ya Benki ya CRDB inayolenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijitali, hususan SimBanking.
Hafla ya makabidhiano ya zawadi hiyo ilifanyika jana katika Viwanja vya Dar Village, Mikocheni jijini Dar es Salaam ambapo ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa benki hiyo na wadau mbalimbali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa CRDB, Stephen Adili, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa wateja wanaotumia huduma za kidijitali za benki hiyo.
“Mbali na magari aina ya IST yanayotolewa kila mwezi, zawadi nyingine mbalimbali kama fedha taslimu pia zinapatikana. Ili kushiriki, mteja anatakiwa kuwa na akaunti ya CRDB na amejiunga na SimBanking. Kila muamala unakupa nafasi ya kushinda, iwe ni kununua umeme, kulipia bili au kukata tiketi za SGR,” alisema Adili.
Kwa mujibu wa CRDB, droo hiyo itaendelea hadi mwezi Disemba ambapo mshindi wa mwisho atajinyakulia gari aina ya Harrier Anaconda, huku wateja wengine wakiendelea kujipatia zawadi mbalimbali kila mwezi.

Adili alisisitiza kuwa huduma ya SimBanking ni jumuishi na haina mipaka kwa kundi maalumu la wateja, kwani inawahusu wanafunzi, wafanyabiashara, watumishi wa umma na hata wafanyakazi binafsi.
Kwa upande wake, mshindi wa zawadi hiyo, Fahad Soud, aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuendesha kampeni hiyo na kuwataka wateja wengine kujitokeza kwa wingi kutumia SimBanking.
“Nimefurahi sana kushinda gari kupitia huduma hii. Naomba Watanzania waamini kwamba kampeni hii ni ya kweli na washiriki kwa kufanya miamala kupitia SimBanking ili nao waweze kushinda kama mimi,” alisema Fahad.



