Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM, Taifa na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe, Doto Mashaka Biteko amewahimiza wananchi wa Jimbo la Sumve, wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza kuwapigia kura wagombea wa CCM kwa kuwa Chama hicho kimefanya jitihada kubwa ya kuwaletea maendeleo.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 21, 2025 Mwanza wakati akimnadi mgombea Ubunge wa Jimbo la Sumve kwa tiketi ya CCM, Moses Bujaga ikiwa ni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Amesema Serikali ya CCM imeendelea na jitihada zake za kujenga Kituo cha Reli ya Kisasa ya SGR kwa ajili ya kupokea mizigo itakayosafirishwa kwenda maeneo mbalimbali pamoja na kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa jijini Mwanza ili kufungua uchumi wa mkoa huo kwa ujumla.
Aidha, imehakikisha wananchi wa vijiji vyote katika Jimbo hilo wanapata umeme ikiwa ni pamoja na usambazaji umeme katika vitongoji.
Dkt. Biteko ameendelea kusema Dkt. Samia Suluhu Hassan ni msikivu na mtu wa vitendo zaidi, ambapo katika Jimbo la Sumve pamoja na miradi mingine amejenga shule za msingi 75, vituo vya afya vitano pamoja na barabara za lami ili kusafirisha mazao kwa urahisi kufika sokoni.

“ Maendeleo haya hayasemwi tu yanaonekana na sisi tunataka kuleta maendeleo na katika kipindi cha miaka mitano ijayo Dkt. Samia anataka kutekekeza miradi mingi zaidi ya maendeleo. Nawaomba Sumve pigeni kura nyingi kwa wagombea wa CCM ili kuheshimisha chama chetu na mkimaliza kupiga kura mtudai maendeleo,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa zoezi la kupiga kura ni la uwekezaji wa maendeleo na kuwa uchaguzi wa mwaka huu una uhusiano wa moja kwa moja na maisha na maendeleo ya watu. Hivyo amewataka wananchi hao kumpigia kura mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akimnadi mgombea Ubunge wa Jimbo la Sumve kwa tiketi ya CCM, Moses Bujaga, Dkt. Biteko amemtaja kuwa ni mtu makini, mtulivu na msomi mwenye umahiri katika katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za wananchi hivyo ifikapo Oktoba 29, wajitokeze kumchagua kwa kura nyingi.

Naye, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Sumve, Moses Bujaga ameishukuru CCM kwa kumteua kugombea nafasi hiyo na atakapochaguliwa atafanya kazi kwa kushirikiana na wananchi ili kitimiza jukumu la kuleta maendeleo.
Naye mgombea Ubunge wa Jimbo la Kwimba, Cosmas Bulala amesema kuwa Kwimba ni kitovu cha maendeleo katika Mkoa wa Mwanza na kuwa ili kuendelea kupata maendeleo zaidi Oktoba 29 wananchi wawachague tena wagombea wa CCM.