Na Kulwa Karedia, Jamhuri Media,Kibaha
Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan atapa kura zisizokuwa na mfano katika mkoa wa Pwani.
Kikwete ametoa kauli hiyo leo Septemba 28 alipopewa nafasi ya kuwasiliana maelefu ya wananchi wa mkoa huo wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu mjini Kibaha.
“Nakuhakikishia mkoa wa Pwani utakuchagua Kwa kura nyingi zisizokuwa na mfano, wabunge wameeleza vizuri na kwa ufasaha kuhusu mambo yaliyofanyika ,”amesema.

Amesema Rais Samia amezikabili vizuri changamoto kwa mafanikio makubwa, kwa ufanisi, ujasiri na umakini wa hali ya juu..
“Umetenda mema na mazuri mengi mno, nasi tutalipa kwa mema uliyoptutendea,tutajaza mpaka kura zifurike kwenye boksi la Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania.
“Tunatambua umuhimu wa kupata wabunge na madiwani wa CCM, hapa kwetu utapata wabunge wetu na hata Bunge lijalo naamini litakuwa la CCM.
“Sisi hatuko tayari kuchanganya pumba na mchele tunajua madhara yake Oktoba tunakwenda kutiki,”amesema.

Amesema ana mpole na hongera kwa kampeni kutokana na kuchanja mbuga tangu Agosti 27 alipozindua Kawe,Dar es Salaaam.
“Kinachofurahisha unaonekana una afya njema, naamini utamaliza salama na utapata ushindi mkubwa ili Watanzania waendelee kunufaika na mchango wako.
“Wewe ni mama mwema sana na mwepesi sana kuchukua hatua, nchi yetu ina umoja, ina makabila 120,dini tofauti hakuna ugomvi wa kidini, Muungano uko imara na ni wa kuigwa duniani, nchi tulivu, maendeleo ya kiuchumi ni mazuri,”amesema.



