Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Moyo ya Jakata Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na Heart Team Africa (HTAF) wameanzisha shindano la insha shuleni ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha watanzania wanatambua hatari ya magonjwa ya moyo tangu wakiwa wadogo.
Shindano hilo lilizinduliwa Leo na Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa kwenye ofisi za HTAF jijini Dar es Salaam ambapo pia alikuwepo Mkurugenzi Mtendaji wa (JKCI), Dk Peter Kisenge na mratibu wa shindano hilo, Mwalimu Matuha Massati.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Dk Kisenge alisema kwenye shindano hilo, mshindi wa kwanza ataaondoka na 3,000,000 na kompyuta mpakato, mshindi wa pili kompyuta mpakato na 2,000,000, mshindi wa tatu atapata kishikwambi na 1,000,000.
Dk Kisenge alisema mshindi wanne atapata Sh 500,000 na cheti wakati mshindi wa tano atapata shilingi 300,000 na cheti.
Dk Kisenge alisema thamani ya shindano hilo ni kubwa sana hasa ikizingatiwa kuwa gharama za matibabu ya moyo ni kubwa na watu wengi hawana uwezo wa kumudu matibabu.
Alisema shindano hilo litasaidia kuhamasisha watu kutambua umuhimu wa kulinda afya ya moyo kuanzia wadogo hali ambayo itasaidia kupunguza mzigo serikali wa kutibu wagonjwa wa moyo.

Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa, alisema katika miaka 10 ya utoaji wa huduma za magonjwa ya moyo na mishipa hapa nchini, Taasisi hii imebaini changamoto mbalimbali katika utoaji na ufikiaji wa huduma ya moyo na mishipa.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo, Taasisi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa mfano, kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma za matibabu na namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kupitia matembezi.
Alisema JKCI ilianzisha miradi mbalimbali iliyolenga kujenga uelewa kwa umma kama Mradi wa “Moyo Wangu, Afya Yangu”.
“Moyo Wangu, Afya Yangu” ni mradi wa miaka mitatu (miezi 36) unalenga kuongeza uelewa na kukuza kinga ya Magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) – hususani magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa watoto wenye umri wa kwenda shule.

“Kwa msingi huo, shindano hili linalenga kutoa elimu na kuwafikia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na utatumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu unakuwa endelevu na wanafunzi wengi wanafikiwa kulingana na mazingira halisi ya shule zetu hapa nchini,” alisema
Alitaja njia zitakazotumika kuwa ni pamoja na vilabu vya afya shuleni, vipeperushi, elimu ya afya shuleni, vijarida, mabango, mashindano ya uandishi wa insha, midahalo, kampeni za afya na usafi wa mazingira nk.
Alisema mbinu hizo zote zitatumika kama majukwaa ya kuelimisha na kuwashirikisha wanafunzi ili kuwajengea uwezo na hatimaye waweze kuelimishana wao kwa wao(mwanafunzi kwa mwanafunzi) kupitia Klabu zao za Afya.
Mkurugenzi Mkuu wa HTAF, Dk Naizihijwa Majani alisema shindano hilo litawashirikisha wanafunzi wa kuanzia Kidato cha kwanza hadi kidato cha sita ambao watapewa zawadi mbalimbali.
Alisema mbali na zawadi hizo pia watajengewa uwezo ili wawe waelimisha rika katika shule zao na shule jirani pia na kwamba litafanyika kuanzia tarehe 08 Oktoba hadi tarehe 01 Novemba, 2025.

Mratibu wa shindano hilo kutoka Wizara ya Elimu, Mwalimu Matuha Massati, alisema mada itakayochaguliwa ili wanafunzi waandikie insha zao itatangazwa katika mitandao ya kijamii na ya taasisi ya JKCI, Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Alisema mada zitatangazwa pia kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na kupitia barua zitakazosambazwa kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI na Maafisa Elimu Mikoa na Halmashauri.
“Washindi wa shindano hili watatangazwa kupitia vyombo vya habari na mawasiliano yatafanyika kupitia mikoa, halmashauri na shule husika,” alisema
