MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuja na mkakati wa kuliwezesha taifa kujitosheleza kwa ngano ikiwemo serikali kuyatwaa mashamba yaliyochukuliwa na wawekezaji bila kuyaendeleza.
Pia, amewatoa hofu wakulima wa mbaazi nchini kuhusu soko la zao hilo ambapo ametaja hatua muhimu zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha bei ya mbaazi haishuki chini ya asilimia 70.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Hanang mkoani Manyara, Dk. Samia alisema serikali imejipanga vyema kumlinda mkulima nchini.

“Najua wakazi wa Hanang ni wakulima wazuri wa ngano na mazao mengine kama mbaazi na dengu. Lengo letu kitaifa kufikisha tani milioni moja ifikapo mwaka 2030 kutoka Hanang ili tuweze kujitegemea kwa mahitaji ya ngano,” alisisitiza.
Dk. Samia alieleza hatua zitakazochukuliwa katika kufikia lengo hilo ni kushughulikia mashamba makubwa ambayo yalitolewa kwa wawekezaji ambao hawajayaendeleza.
Hivyo, aliitaka Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uwekezaji kuangalia upya mikataba ya uwekezaji na namna yatakavyoweza kurudishwa mashamba hayo serikalini.
Alisema hatua hiyo itawezesha mashamba hayo kugawanywa kwa wakulima kisha kuzalisha mazao.
“Haipendezi kwamba tuna mashamba ambayo yanaweza kuzalisha ngano nyingi lakini tunaagiza ngano nyingi kutoka nje huku mashamba yamekaa bila kuzalisha.

Alisisitiza: “Tunakwenda kuyaangalia mashamba hayo. Tumeitaka mamlaka ya maeneo huru ya uwekezaji kuangalia jinsi tunavyoweza kuyachukua.”
Kuhusu shamba la Basotu, alisema serikali imeamua kuendelea na utaratibu uliopo kuwa chini ya msajiri wa hazina huku Halmashauri ya Hanang ikilisimamia.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kulitumia shamba hilo kwa gharama nafuu huku akiiagiza halmashauri kuweka gharama hizo wazi ili wakulima wazifahamu.
“Kwa sababu tumegundua kuna mambo mambo huko ndani, wakulima wanataka maeneo ya kulima lakini halmashauri mna mambo yenu. Kwa hiyo tunataka gharama ziwekwe wazi ili tuepushe vishoka katika shamba hilo,” alisisitiza.
Kuhusu bei ya mbaazi, alisema wanunuzi wa kati nao wanasababu nyingi ya kutelemsha bei ya zao hilo, hivyo serikali ipo katika majadiliano na India.
Alisema katika mazungumzo hayo hata kama bei imeshuka isiwe chini ya asilimia 70 ya msimu uliopita.
“Najua wanaotaka kushusha bei wana lawama nyingi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani lakini mfumo huu huu bei zinapopanda mfumo unafanyakazi pia.
“Kushuka na kupanda kwa bei ni mambo ya biashara, mazao yakiwa mengi sokoni bei zinashuka. Tukivuna sisi wengine hali ya hewa haikuwapendelea bei zinapanda,” alieleza.
UJENZI WA BARABARA
Dk. Samia alisema serikali imeendelea kujenga miundombinu ya barabara katika jimbo hilo zikiwemo Nangwa – Isambala – Kondoa kilometa 79 ambayo itajengwa kwa lami.
Vilevile barabara nyingine ni Mogito – Hydom kilometa 70 itajengwa kwa kiwango kitakachopitika mwaka mzima.
Akizungumzia ripoti ya Ngorongoro alipokuwa wilayani Karatu, Dk. Samia alisema tayari timu zilizoundwa kufanya utafiti katika eneo hilo zimeshakamilisha ripoti zake.
“Ndugu zangu wa Ngorongoro niwapongeze kwamba tumemaliza taarifa ambayo tuliweka timu mbili wafanye utafiti baina ya wataalamu wa serikali na wenyeji wa Ngorongoro.
Aliongeza: “Ripoti imeshakuja serikalini. Tumesita kutoa maamuzi kwa sababu tupo kwenye pilika hizi baada ya uchaguzi nikishapanga serikali, tutaipitia vizuri ile ripoti na tutoe maamuzi kwa wananchi wa Ngorongoro.”
Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, alimhakikishia Dk. Samia kwamba wananchi wa Hanang watajitokeza kwa wingi Oktoba 29 mwaka huu kumpigira kura za kishindo.
Mgombea Ubunge Jimbo la Hanang, Asia Hamlanga, alisema katika falsafa ya Kazi na Utu, Dk. Samia ametekeleza kwa vitendo falsafa hiyo.
Akizungumzia kuhusu kazi zilizofanyika ndani ya jimbo hilo, alisema Dk. Samia alitoa zaidi ya sh. bilioni 90 kwa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo iliyotekelezwa ni maji, elimu, nishati na afya ambayo imeongeza kasi ya maendeleo katika jimbo hilo.
“Tuna stendi mpya ya kisasa ambayo inafanyakazi. Jengo la utawala ujenzi unaendelea na zaidi ya sh. bilioni nne zimetengwa, ujenzi wa madarasa zaidi ya 10 katika Shule ya Sekondari Katesh,” alieleza.
Pia, Asia alieleza kuwa tayari wameshapokea sh. bilioni tano zitakazotumika kugharamia ukarabati wa barabara za ndani.
“Kwenye Utu Dk. Samia dunia inajua. Tulipata janga hapa (maporomoko ya udongo) tuliuona utu wako, serikali yako ilihamia hapa. Ulitusaidia wakati wa maporomoko. Ukatoa fedha za ujenzi wa daraja linalounganisha Hanang na Babati.
“Umewajengea watu wetu nyumba zaidi ya 100. Umeweza kuleta demokrasia, umeweza kuwaunganisha Watanzania, wafugaji walikuwa hawapokesheki umeingia wewe wameanza kukopesheka na hapa wamepata zaidi ya sh. milioni 400,” alieleza.