Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
MIKOPO ya zaidi ya shilingi bilioni 27.2 zimetolewa kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO SACCOS) ikiwa ni sehemu ya mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa 57 wa TANESCO SACCOS uliofanyika mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO SACCOS, Omary Shabani, amesema kuwa hadi kufikia Agosti 31, 2025 mikopo hiyo imetolewa kwa wanachama 4,031 waliokidhi vigezo vya chama hicho.

Amesema TANESCO SACCOS imeendelea kuwa nguzo muhimu ya kiuchumi kwa wanachama wake.
“Tumetoa mikopo ya zaidi ya bilioni 27.3 kwa mwaka huu wa 2025, hatua inayothibitisha dhamira yetu ya kuwawezesha wanachama kifedha na kuwajengea uwezo wa kiuchumi,” amesema Shabani.
Amebainisha kuwa mbali na huduma za mikopo, chama hicho kimewekeza kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la ofisi na uwekezaji katika hisa zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 10.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza mapato, kupanua huduma na kudumu kwa ustawi wa chama hicho.

“Mpango wa TANESCO SACCOS ni kuendelea kusimamia rasilimali zake kwa uwazi na weledi ili kuhakikisha kila mwanachama ananufaika kwa usawa na chama kinakuwa endelevu kwa vizazi vijavyo,” amesema Shabani.
Kwa upande wake, Mhandisi Antony Mbushi aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), amesema Shirika linajivunia uwepo wa SACCOS hiyo kwa kuwa imekuwa chachu ya kuinua hali ya maisha ya wafanyakazi wake na mfano bora wa ushirika unaofuata taratibu, sera na misingi ya kisheria.
“TANESCO SACCOS imekuwa chombo muhimu cha kusaidia ustawi wa watumishi. Shirika litaendelea kushirikiana kwa karibu kuhakikisha chama hiki kinaimarika zaidi na kufanikisha malengo yake,” amesema Mbushi.




