Mgombea Urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, amesema serikali ya chama hicho itahakikisha mchango wa sekta ya kilimo kwa uchumi wa nchi unakua na kufikia asilimia kati ya saba hadi tisa ndani ya miaka mitano ijayo.
Ahadi hiyo ameitoa jijini Mwanza wiki iliyopita wakati wa mkutano wa kampeni huku akisisitiza kilimo cha pamba atakirudisha enzi za Mwalimu Julius Nyerere.
Amesema serikali ya chama hicho inakusudia kufungamanisha kilimo na viwanda si tu kwa ajili ya uchakataji wa mazao na uzalishaji wa bidhaa hapahapa nchini, bali pia kutengeneza ajira kwa Watanzania na kuleta faida zingine na watatenga asilimia 10 ya bajeti kwa ajili ya uwekezaji.
Aidha, amesema serikali ya chama hicho itatoa miezi 18 tu kwa wamiliki wote wa viwanda visivyofanya kazi kuvifufua na wakishindwa wavirudishe kwa serikali sambamba na kusimamia utekelezaji wa kukamilika kwa wakati miradi ya kimkakati ikiwamo Reli ya SGR kutoka Mwanza hadi Kahama.
Amesema serikali ya chama hicho itahimiza urasimishaji ardhi ili kuvutia wawekezaji lakini pia kuhakikisha kila Mtanzania anapimiwa eneo lake ili kupanga matumizi sahihi ya ardhi.
Mgombea Ubunge wa chama hicho Jimbo la Ilemela, Evance Mabugo, ameahidi kuimarisha zaidi barabara za pembezoni na huduma za afya, hasa katika Zahanati ya Igoma kwa kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana wakati wote.
