Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kuboresha na kuhakikisha haki za wananchi zinaheshimiwa katika utolewaji wa fidia kwa wale waliopoteza ardhi zao kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege Pemba.
Alizungumza hayo katika mkutano maalumu na wananchi wa Shehia ya Furaha, Wilaya ya Chake Chake, Pemba alisema haiwezekani kuona mamia ya watu wanaendelea kuzulumiwa kwenye Nchi yao tena bila ya huruma.

Othman alieleza kuwa amepokea taarifa za malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu malipo yasiyotimizwa ipasavyo, huku baadhi wakikosa kabisa fidia zao stahiki jambo ambalo limeongeza umasikini zaidi kwa wananchi hao.
‘’Hauwezekani mtu alikua na shamba yake ambayo anafanya shughuli za kilimo na ilikua inamuingizia kipato kuendesha familia leo unakwenda kumpa fedha ambazo haziendani kabisa na uhalisia wa eneo leke huu ni uonevu haupaswi kuvumiliwa’’alisema.
Amesisitiza kuwa katika serikali yake, kila mwananchi atahakikishiwa anapokea fidia yake kwa haki na kwa mujibu wa eneo alilochukuliwa.
“Si uungwana na si haki kwa mtu kuchukua ardhi ya wananchi kwa ajili ya maendeleo halafu wamiliki halisi wasipate haki zao. Serikali yangu itahakikisha mimi mwenyewe binafsi nitaisimamia hili kwa karibu,” alisema Othman.
Awali, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walizungumza kwa uchungu juu ya kile walichosema ni udhalilishaji na mamlaka zilizohusika katika utolewaji wa fidia.

Abdalla Seif mmoja wa wakazi aliyeathirika, alisema kuwa shamba lake lilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya uwanja wa ndege huku akipokea fidia ndogo mno, jambo ambalo limewaumiza wengi.
Huku hayo yakijiri baadhi ya wananchi wa eneo hilo walimueleza Othman Masoud kuchoshwa na utawala ulipo madarakani wakisema unaendelea kuwanyanyasa kila leo.
Ali Abdalla Juma alisema eneo lake ambalo limechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege angeamua kulizua lingeweza kufika ata milioni mia moja lakini fidia aliopewa haikufika hata milioni Hamsini.
Alisema hatua hiyo ni unyonyaji mkubwa ambao haupaswi kunyamazwa na kwa mara kadhaa amewahi kupaza sauti akisema hakuna hatua iliochukuliwa.
