MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA KUMUOMBEA BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE

ASISITIZA WANANCHI KUENDELEA KUMUOMBEA NA KUENDELEZA MEMA ALIYOFANYA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasihi Watanzania kuendelea kumuombea Baba wa Taifa hayati Mwalimu. Julius Kambarage Nyerere ili aendelee kupumzika kwa amani na awe mmoja wa Watakatifu.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati alipoungana na Viongozi, Waumini pamoja na Wananchi mbalimbali katika Ibada ya kumuombea Baba wa Taifa Mwalimu. Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Asizi, Mwanjelwa Mkoani Mbeya.

Amesema ni vema kila mmoja wetu hususani viongozi kufuata mfano mwema wa Baba wa Taifa ambaye alikuwa mwaminifu kwa Taifa la Tanzania na kulitakia mema wakati wote.

Aidha kwa niaba ya Serikali, Makamu wa Rais amewashukuru waumini na wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa kujitokeza kumuombea Baba wa Taifa wakati wa kumbukizi ya miaka 26 tangu kifo chake.

Ibada hiyo imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbeya Mhashamu Gervas Nyaisonga ambaye katika mahubiri yake amesema Baba wa Taifa alikuwa ni mtu aliyefuata maadili mema ikiwemo mwenendo haki, huruma, unyenyekevu na uaminifu.

Amesema Mwalimu Nyerere aliacha urithi wa kisiasa tangu wakati wa kuhangaikia uhuru, aliacha urithi wa Muungano wa Taifa pamoja na mageuzi ya kidemokrasia. Pia amesema kupitia Azimio la Arusha mwaka 1967 Mwalimu Nyerere aliacha urithi wa kijamii na kiuchumi ili kujenga jamii yenye usawa.

Askofu Mkuu Nyaisonga ameongeza kwamba, Mwalimu Nyerere alisisitiza elimu kwa lengo la kuondoa ujinga na kuweza kujitegemea, aliacha urithi wa utamaduni hususani kwa kusisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili, maadili na utu na aliweka maslahi ya Taifa mbele.

Pia amesema Baba wa Taifa alitoa mchango wa ukombozi wa kikanda na kimataifa kupitia usaidizi wake katika kuhakikisha mataifa mengine yanakuwa huru. Alitoa mchango katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, kushiriki kujenga diplomasia ya kusini mwa Dunia na kupigania usawa wa kiuchumi kati ya mataifa matajiri na mataifa yanayoendelea.

Amesema kupitia jitihada hizo na nyingine nyingi, ni hamasa kwa Watanzania kuendelea kumuombea Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ili aweze kusamehewa makosa yake na kuwa ​Mwenyeheri.

Ibada hiyo pia imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali.