Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekiel Wenje, amesema kuwa katika kipindi chake cha siku tatu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amebaini mambo mengi kuhusu maendeleo yaliyotekelezwa na Serikali.

Amesema kuwa awali alipokuwa nje ya chama hicho, alikuwa miongoni mwa waliokuwa wakikosoa Serikali kupitia mitandao ya kijamii bila kujua ukweli wa mambo.

Ameyasema hayo Oktoba 15, 2025 katika Viwanja vya Bashungwa, Kayanga wilayani Karagwe mkoa wa Kagera, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nimegundua usichokijua ni usiku wa giza. Zamani tulikuwa tunakosoa Serikali bila kusikiliza hizi takwimu, kumbe tulikuwa gizani,” amesema Wenje.

Aidha, amebainisha kuwa katika siku hizo tatu alizokaa ndani ya CCM amesikiliza takwimu za maendeleo zilizotolewa na wagombea na kubaini kazi kubwa iliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini. Amesema kelele ndogondogo zinazotolewa na baadhi ya watu zisimuogopeshe mgombea wa urais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani hata mbinguni kulikuwa na kelele na Yesu naye alipitia changamoto akiwa na wanafunzi wake wakatokea akina Yuda Iskarioti.

Wenje amekumbuka ziara yake ya kwanza Karagwe mwaka 2010, ambapo barabara kutoka Kyaka hadi Kayanga ilikuwa ya vumbi na safari ilichukua saa tano. Amesema kuwa hivi sasa safari hiyo inachukua dakika 45 pekee, jambo linaloonesha hatua kubwa ya maendeleo.

Aidha, amebainisha kuwa hakuna nchi duniani iliyowahi kufikia maendeleo ya mwisho, akitolea mfano Marekani kuwa licha ya uchumi wake mkubwa, bado inakabiliwa na changamoto za ajira na makazi.

Pia, amesema kuwa lengo la chama chochote cha siasa ni kushika dola kupitia uchaguzi, si maandamano, na kwamba chama chake cha zamani kimepoteza mwelekeo kwa kuruhusu wanaharakati wa mitandaoni kukiongoza.

“Mzee Kikwete alisema, ‘akili ya kuambiwa changanya na ya kwako’,” amesema Wenje.

Aidha, amewatahadharisha Watanzania kuwa wasifuate wanasiasa wanaoishi nje ya nchi wanaochochea maandamano, akiwalinganisha na kisa cha mchungaji Jim Jones aliyewapoteza wafuasi wake baada ya kuwashawishi kunywa sumu akidai wataenda mbinguni.