Rais Donald Trump wa Marekani atakutana na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine mjini Washington leo siku moja baada ya kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Urusi yaliyojadili hatua za kumaliza vita.
Trump amesema mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais Putin “yalikuwa mazuri” na wamekubaliana kufanya mkutano wa kilele mjini Budapest nchini Hungary mnamo wiki zinazokuja.
Atakutana na Rais Zeleskyy katika wakati anatafakari uwezekano wa kuipatia nchi hiyo makombora ya masafa marefu ili kuisaidia kuikabiliana na Urusi.
Inatazamiwa kuwa Zelenskyy atamsihi Trump aidhinishe Ukraine kupatiwa silaha hizo na mifumo zaidi ya ulinzi hasa kutokana na kuendelea kwa mashambulizi ya anga ya Urusi.
Usiku wa kuamkia leo Urusi iliishambulia miundombinu ya umeme ya Ukraine kwa droni na makombora na kusababisha ukosefu wa nishati hiyo muhimu kwenye mikoa kadhaa.
