Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Masasi
Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake za lala salama wilayani Masasi, katika viwanja vya Soko la Mkuti, Masasi Mjini.
Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Masasi, Mhe. Doyo ameahidi kuwa serikali yake, endapo atapewa ridhaa na wananchi, itarejesha reli ya Masasi, Dar es Salaam, ambayo ilisitisha shughuli zake mwaka 1972.
Amesema kuwa reli hiyo ilikuwa uti wa mgongo wa uchumi wa kusini, na kufufuliwa kwake kutachochea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. “Kupitia reli hii, wakulima wa korosho, na mazao mengine ya biashara wataweza kusafirisha bidhaa zao kwa gharama nafuu hadi masoko makubwa ndani na nje ya nchi,” amesema Mhe. Doyo.

Ameongeza kuwa, uwepo wa reli utarahisisha biashara, ajira, na uwekezaji, huku ukifungua fursa mpya kwa vijana na wanawake kupitia usafirishaji wa bidhaa, utalii, na huduma nyingine za kibiashara.
Aidha, Mhe. Doyo ameahidi kuanzisha Mkoa wa Kusini, utakaoundwa na wilaya za Newala, Nanyumbu, Tandahimba, Nachingwea, na Liwale, ikiwa atachaguliwa kuwa Rais. Amesema lengo kuu ni kupeleka huduma karibu na wananchi, kuongeza ufanisi wa usimamizi wa miradi ya maendeleo, na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kama afya, elimu, maji safi na barabara.
“Kupitia mkoa mpya wa kusini, wananchi hawatalazimika tena kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za serikali. Hii ni hatua muhimu ya kuwawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika maendeleo yao,” alisisitiza.
Msafara wa mgombea urais huyo unaelekea Dar es Salaam, Zanzibar, na Tanga, ambako ataendelea na mikutano yake ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu ujao.


