Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Maendeleo la Kiswidishi linalotekeleza miradi ya maendeleo nchini kwa kushirikiana na wabia mbalimbali Vi Agroforesty limeandaa maonesho ya 10 ya kilimomisitu yanayotarajiwa kufanyika mjini Musoma.
Meneja Mkazi wa shirika hilo nchini Martha Olotu aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo muhimu linaadhimisha miaka 15 ya mafanikio katika matumizi endelevu ya ardhi, usalama wa chakula na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema maonesho hayo yatafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 15 Novemba mwaka huu katika kituo cha mafunzo cha kilimomisitu kilichoko Bweri Musoma na yanatarajiwa kuwaleta pamoja washiriki 6,000.
Alisema chini ya kauli mbiu ya ‘kilimomisitu kwa ukuaji jumuishi na endelevu’ maonesho hayo yatakuwa jukwaa la kitaifa la kubadilishana maarifa, mijadala ya kisera, na kuhamasisha ushirikiano wa pamoja .
Olotu alisema maonesho hayo yatawakutanisha wakulima, watafiti, watunga sera, wabia wa maendeleo, na sekta binafsi ili kuhamasisha kilimomisitu nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.

Aidha, alisema maonesho hayo yataonesha mchango wa kilimomisitu katika ustawi wa maisha ya wakulima wadogo, na uhifadhi wa baionuai, kuboresha mfumo wa chakula na mapato kwa kaya.
Alisema maonesho hayo yatasaidia kushughulikia changamoto za uhalibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuzungumzia vikwazo vya upatikanaji sawa wa teknolojia na mbinu za kuimarisha kilimomisitu.
Alisema maonesho hayo yataongozwa na programu ya siku tatu ambayo itajumuisha mijadala na uwasilishaji wa mada katika maeneo makuu matatu ambayo ni fursa za kiuchumi zinazozingatia uwepo wa vyanzo mbalimbali vya mapato vijijini na minyororo ya thamani jumuishi.
Alitaja mada nyingine kuwa ni mifumo ya ikolojia inayostahimili mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa baioanuai na afya ya udongo na mada ya mazingira yanayorahisisha utekelezaji wa mfumo wa sera, mifumo ya ufadhili, na usalama wa umiliki wa ardhi.
Olotu alisema maonesho hayo yatashirikisha wabia wa maendeleo kutoka mashirika ya kitaifa nakimataifa na kwamba ushiriki wao utaimarisha zaidi dhima ya maonesho haya kama nyenzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano katika kuunda mifumo ya kilimo jumuishi na yenye uwezo wa kustahimili mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kutakuwa na kampeni ya upandaji miti ambayo itafanyika katika Shule ya Msingi Mkiringo, Musoma na kwamba utaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, watumishi wa Vi Agroforestry, washirika wa sasa na wa zamani wa shirika hilo, pamoja na wakulima, wanafunzi na walimu, na wageni waalikwa watashiriki.
“ Ushirikiano huu unaonyesha mchango wa kilimomisitu katika kurejesha mifumo ya ikolojia, kuimarisha uhimilivu wa jamii, na kushirikisha vijana kama chachu katika kuleta suluhisho la mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Alisema katika kuadhimisha miaka 10 ya maonesho na miaka 30 ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini, shirika la Vi Agroforestry linatoa wito kwa wadau wa sekta binafsi na umma kuungana katika kusherekea safari ya miaka 10 ya maonesho ya kilimomisitu na mchango wake kwa Taifa na jamii za wakulima na wafanya baiashara.
“Viongozi wa kijamii, maafisa wa serikali, watafiti, na washirika wa sekta binafsi wanahimizwa kushiriki kwa lengo la kubadilishana maarifa pamoja na tutajenga mikakati ya utekelezaji na mapendekezo ya sera yatakayohakikisha kuwa kilimomisitu kinaendelea kuchangia ukuaji jumuishi na endelevu kwa watanzania wote,” alisema.

