Na Witness Masalu WMJJWM-Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza tija katika utumishi wao
Akitoa nasaha juu ya umuhimu wa kulinda afya kwa watumishi wa Wizara hiyo baada ya zoezi la upimaji wa afya lililofanyika tarehe 10, Novemba 2025, kwa kubainisha kwamba, mafunzo na vipimo vya kiafya ni sehemu ya utekelezaji wa muongozo wa utumishi unaotaka waajiri kuhakikisha wanazingatia afya kwa rasilimali watu ili watekeleze majukumu yao ipasavyo.

“Kama tunataka kuwa na tija katika maeneo yetu ya kazi ni muhimu kulinda afya zetu kwa kuhakikisha tunakula milo sahihi, Matunda, Kunywa maji ya kutosha pamoja na kufanya mazoezi ili kujiweka sawa na hatimaye tuweze kufikia hatima zetu uzeeni tukiwa salama.” amesema Wakili Mpanju.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa afya ya akili Dkt. Isack Rugemalila amesema kuna takribani magonjwa 297 ya akili na ili kuepuekana nayo katika mazingira ya kazi ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na dhamira ya kuwa sawa, kukwepa vichochezi vinayowanyima amani na furaha, kupumzika, kuachana na pombe, kula vizuri na kuweka mazingira mazuri kati ta watumishi.
Vilevile Mtaalam wa Magonjwa ya HIV/VVU kutoka hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Esidras Karol amesema takribani watu milioni moja nchini wanaishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi hivyo kutoa tahadhari kwa watumishi kuwa makini kwa kuepuka ngono zembe, kutokuchangia vifaa vyenye ncha kali na kuongezewa damu bila utaratibu sahihi.









