Na: OR – MV, Kyela

Vijana wa Wilaya ya Kyela wameshukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuondoa zuio la wananchi kuacha kufanya kazi ifikapo saa 6 usiku kufuatia matukio ya baada ya uchaguzi mkuu ambapo kuanzia leo wananchi wanaruhusiwa kufanya kazi masaa 24.

Kauli hiyo ya Serikali imekuja ikiwa ni mafanikio ya ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka mara baada ya kuzungumza na vijana katika mkutano uliofanyika Soko la Kyela leo (27 Novemba 2025) baada ya vijana kuwasilisha malalamiko hayo.

Waziri Nanauka alitoa fursa ya vijana kutoa mawazo na maoni yao ambapo Saimon Charles alieleza kuwa kufuatia maandamano na vurugu za baada ya uchaguzi mkuu Serikali iliweka zuio la wananchi kufanya shughuli baada ya saa sita usiku hali ambayo imepelekea vijana hususan waendesha pikipiki na biashara ndogondogo kukosa kazi.

“Hapa Kyela kulala mwisho saa 6 usiku tunashindwa kujiachia, Polisi wanashinda barabarani kutuzuia na kutukamata hatua inayoleta hofu wakati maeneo mengine nchini wanafanya kazi muda wote,” alisema Saimon.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Nanauka alimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Kyela Josephine Manase atoe kauli ya Serikali kuhusu madai hayo ya vijana, ndipo aliposema kuwa kutokana na kurejea kwa hali ya utulivu wilayani humo sasa anatoa tamko kuwa shughuli za wananchi kuanzia leo zitafanyika muda wa saa 24.

Baada ya tamko hilo vijana walipokea kwa furaha na shangwe na kusema wameridhishwa na kufurahishwa na ziara ya Waziri Nanauka kwa kuwa imesadia kutatua changamoto na kero za vijana iliyodumu tangu uchaguzi mkuu uliopita.

Waziri Nanauka akizungumza na vijana hao, aliwaeleza kuwa dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunda wizara maalum ya vijana kwa lengo la kutaka kusikia mawazo na fikra za vijana nchini ambapo katika siku 100 za awali amesema atatekeleza masuala 13 ambapo kati yake sita yanahusu vijana.

Kuhusu suala la amani na utulivu, Waziri Nanauka amewaeleza vijana kuwa lengo la Serikali ni kuhaakikisha vijana wanaopambana kutafuta kipato chao cha halali wanatambuliwa na kusaidiwa kupitia wizara anayoingoza hivyo ataanzisha mfumo wa kisasa wa kidijitali utakaowezesha vijana kuwasiliana na wizara na kupata mrejesho.

Waziri Nanauka anaendelea na ziara yake mkoani Mbeya ambapo leo amekutana na vijana na wajasiliamali wanawake katika soko la Kyela na Ipinda ambapo vijana wamezungumza maoni na ushauri wao kwa Serikali.

Katika ziara hii Waziri Joel Nanauka anafuatana na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Dkt. Kedmon Mapama ambapo inaongozwa na kauli mbiu isemayo Vijana Tuyajenge, Tanzania ni Yetu inayolenga kuwaleta pamoja vijana kuzungumza ili kujenga kesho bora ya vijana wa Tanzania.