Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepokea magari mawili aina ya Land Cruiser Prado kutoka Taifa la Qatar kwa ajili ya kuhudumia viongozi wanaokuja kwa ziara za kitaifa na kikazi nchini.
Qatar kama mshirika wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania alikubali ombi na ametoa magari hayo mapya kufuatia ombi la magari na pikikipiki za kuhudumia viongozi wa nje wawapo katika ziara nchini huku wakiendelea na mchakato wa kuleta pikipiki sita.

Akizungumza katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa nyaraka za magari hayo, Mheshimiwa Waziri, Balozi mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameishukuru Qatar kwa kuwa mdau mkubwa wa maendeleo Tanzania na kuahidi kutumia vyema misaada hii ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza katika kazi.
Akimkabidhi funguo za magari hayo Afisa Usafirishaji Mkuu, Bw. Maulid Mkenda, Mhe. Waziri Kombo amemhimiza kuyatunza magari hayo ili yadumu na kuleta tija na ufanisi.
Qatar pia imekuwa ikitoa ushirikiano katika masuala ya ajira kwa vijana kwa kutoa nafasi za ajira kwa madereva wa Kitanzania nchini Qatar huku nafasi nyingine zikiendelea kuja na kutangazwa.
Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema kuwa msaada huo unaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kidiplomasia kutokana na aina ya uhusiano unaojengwa hususan ukizingatia kuwa Qatar ni miongoni mwa mataifa yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na ushawishi wa kimataifa.
Tukio hilo limefanyika leo hii jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maafisa kutoka wizara husika na ujumbe wa ubalozi wa Qatar nchini, likiwa sehemu ya mwendelezo wa mashirikiano yanayokua katika eneo la nishati, utalii, elimu na ajira.









