Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMesia, Kibaha

MEYA wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, ametoa onyo kwa baadhi ya watendaji wanaotekeleza majukumu yao kwa mazoea, akisema tabia hiyo inatia doa Manispaa na kuchochea kero kwa wananchi.

Aidha, Manispaa hiyo imetoa maelekezo kwa wataalamu wa ardhi kuanzisha kliniki ya ardhi itakayokuwa ikisikiliza na kushughulikia kero za wananchi kila Alhamisi, kwa lengo la kupunguza malalamiko yanayotokana na masuala ya ardhi.

Dkt. Nicas alisema hayo baada ya kuzungumza na wananchi wa Mtaa wa Kidimu, Kata ya Pangani, katika ziara yake ya kukutana uso kwa uso na wananchi kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero zao.

Alisisitiza kuwa hakuna mtendaji atakayesalia salama endapo atakwepa au kupuuza wajibu wa kushughulikia kero za wananchi.

โ€œTimu yote ya Manispaa tutakwenda eneo la tukio (site), Ni mwendo wa site, Wananchi watapata majibu ya papo kwa papo, “Moto huu hautazimika kwa sababu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani wasaidizi wake tushuke kwa wananchi, tuwasikilize na kuwasaidia wale wasio na pa kusemea,โ€ alieleza Dkt. Nicas.

Awali, wakizungumzia kero za ardhi, wananchi akiwemo Ramadhani Ngaleba, Sharifa Mkanje, Denis Mtegeki, Hashimu Bumbuli, Frolensi Mtao na Esther Chacha, walisema changamoto ya migogoro ya ardhi katika mitaa ya Kata ya Pangani ni kubwa, hususan katika eneo la mradi wa viwanja vya Vingunguti.

Sharifa Mkanje aliitaka Manispaa kukaa na watendaji wa Kitengo cha Ardhi ili kuondoa sintofahamu iliyopo kati yao na wananchi.

Kwa upande wake, Ofisa wa Kitengo cha Ardhi wa Manispaa ya Kibaha, Kennedy Thobias Mpanduji, alisema kuwa kuna mradi wa urasimishaji wa ardhi unaoendelea, ambapo zoezi la uhakiki wa maeneo ya wananchi na viwanja linatarajiwa kukamilika mwezi Januari 2026.

Alieleza kuwa baada ya zoezi hilo, changamoto za waliobaki zitabainika na hatua zitachukuliwa ikiwemo kuwapatia wananchi wengine viwanja mbadala ili waweze kulipia.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Mrisho Mlela, alisema Manispaa imepokea maelekezo na miongozo iliyotolewa na Meya na kwamba hatua za utekelezaji zinaanza mara moja.