Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wizara ya Maendeleo ya Vijana imeazimia kuanzisha jukwaa la kidijitali la huduma jumuishi (youth digital one stop platform) ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za ajira, mafunzo, fursa za mikopo, masoko, na huduma nyingine sehemu moja
Wizara pia imeahidi kuimarisha majukwaa ya kuwakutanisha vijana ili kusikiliza sauti zao, kujadili changamoto, kuwaunganisha na wadau.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara, Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema jukwaa hilo litakwenda sambamba na hatua za kisheria na kiutendaji kuelekea ukamilishwaji wa mfumo wa ushiriki wa vijana kitaifa, ikiwemo taratibu za utekelezaji wa Baraza la Vijana.
Aidha , katika eneo la ugunduzi na ubunifu, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu kwa kuendeleza vituo atamizi na vituo vya kulea wabunifu (innovation hubs), pamoja na kuhamasisha ubunifu unaozalisha ajira na bidhaa/huduma zenye ushindani.

‘’Tutaimarisha mifumo ya ulinzi wa kazi za ubunifu katika sanaa, michezo, filamu na muziki, ili vijana wanufaike kiuchumi kutokana na kazi’’amesema.
Nanauka amedai katika ziara zao mikoani wamebaini , masuala muhimu yanayohitaji hatua za haraka ikiwemo uhitaji mkubwa wa ajira na mafunzo ya vitendo; changamoto ya taarifa duni kuhusu fursa zilizopo; upungufu wa mitaji ushauri wa kibiashara; masoko,maadili,afya ya akili na matumizi ya madawa ya kulevya
‘’Tumejipanga kuhakikisha serikali inafikika kwa vijana kwa urahisi na kwa wakati, na tunatumia teknolojia kama nyenzo ya msingi ya kuharakisha huduma, kupokea maoni, na kuunganisha vijana na fursa.
Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa kanuni za ununuzi wa umma zinazoelekeza kutengwa kwa asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi wa umma kwa ajili ya makundi yenye kipaumbele ikiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Hii ni fursa muhimu kwa vijana kujenga biashara endelevu kupitia utoaji wa bidhaa na huduma kwa serikali na taasisi zake’’amesema
Kwa upande wa uwekezaji amesema uanzishaji wa viwanda, serikali inaendelea kukuza uwekezaji maalumu wenye kulenga ajira za vijana ikiwemo kupitia mfumo wa kongani na uwekezaji (TISEZA ) kwa kurahisisha taratibu, kupunguza urasimu, na kuvutia miradi itakayoongeza ajira na ujuzi kwa vijana.
‘’Mwelekeo huu unaenda sambamba na hatua za serikali za kuendeleza programu za uwekezaji, zinazoweka vijana katikati, ikiwemo uanzishaji wa mikakati ya vijana kumiliki na kuendesha miradi ya uzalishaji na viwanda vidogo.
Pamoja na upatikanaji wa mitaji, serikali imeanza kuweka msisitizo wa kuanzishwa na kuimarishwa kwa mifumo ya dhamana ya mikopo (credit guarantee schemes) ili kujibu changamoto ya muda mrefu ya vijana wengi kukosa dhamana (collateral) wanapohitaji mikopo ‘’amesema.
Nanauka amesema dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya mheshimiwa dkt samia suluhu hassan ni kuhakikisha vijana wanafikiwa walipo, wanasikilizwa kwa makini, na wanashirikishwa kikamilifu katika kujenga mustakabali wa taifa.
Aidha serikali inatambua kuwa vijana ndiyo nguvu kazi kubwa ya taifa na mhimili wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ,hivyo inaendelea kuweka misingi ya utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo 2050 .

Inayosisitiza ukuaji jumuishi unaoweka mwananchi katikati, ikijumuisha uwezeshaji wa vijana, upatikanaji wa ajira zenye staha, ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko, na matumizi ya sayansi na teknolojia kama nguzo za mageuzi ya uchumi.
Amesema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 imeweka dhamira ya kuzalisha ajira zenye tija zisizopungua milioni 8 katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kwa kuongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji, na kukuza sekta zenye fursa kubwa kwa vijana.
‘’Serikali imejipanga kuimarisha utekelezaji wa sera ya taifa ya maendeleo ya vijana ya mwaka 2007 (toleo la mwaka 2024) na kuhakikisha kuwa vijana wanaandaliwa vyema na wanapata fursa za kujiajiri na kuajiriwa.
Mikakati yetu itaelekezwa katika maeneo 13 ya kipaumbele yaliyoainishwa katika sera hiyo, ikiwemo elimu na mafunzo ya ufundi stadi; uvumbuzi na ubunifu; uchumi wa kidijitali; ukuzaji wa ajira; ushiriki wa vijana kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi;
Uzalendo na maadili; afya na ustawi; malezi na makuzi; taaluma ya maendeleo ya vijana; uongozi; usawa wa kijinsia; mazingira; na ujumuishwaji wa vijana wenye ulemavu’’amesema
Ameongeza kusema kuwa katika eneo la ajira, serikali kupitia wizara yenye dhamana ya kazi na ajira inaendelea kuandaa na kuimarisha mikakati ya kuongeza fursa za ajira ndani na nje ya nchi, ikijumuisha uimarishaji wa huduma za ajira, usajili na uidhinishaji wa waajiri na mawakala wa ajira, ulinzi wa haki za wafanyakazi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinganifu wa ujuzi na mahitaji ya soko.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha programu za mafunzo kazini na uzoefu wa kazi kwa lengo la kuwapa vijana uzoefu halisi wa kazi na kuongeza ushindani wao katika soko la ajira.
Aidha katika kuongeza ajira kupitia sekta zenye uzalishaji mkubwa, serikali inaendelea kutekeleza na kuratibu programu maalumu za kilimo-biashara, madini na uvuvi zinazolenga kuongeza tija, kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa thamani.

