Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kupooza umeme (substation) cha Handeni mkoani Tanga, unaolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wakazi na wawekezaji wa wilaya hiyo.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, Nyamwese amesema kwa sasa Wilaya ya Handeni ina wawekezaji wakubwa katika sekta mbalimbali, hali inayoongeza mahitaji ya nishati ya umeme wa uhakika na wenye nguvu.
“Kwa hiyo, kukamilika kwa substation hii kutaleta tumaini jipya kwa wakazi wa Handeni na wawekezaji. Wawekezaji wengi wanatamani kuja kuwekeza Handeni, lakini bado wanasuasua kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika na wenye uwezo wa kuendesha mitambo yao,” amesema Nyamwese.
Ameeleza kuwa mara baada ya kituo hicho kukamilika, kinatarajiwa kuvutia uwekezaji wa uhakika na kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi wilayani humo.
“Tuishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mipango aliyoiweka katika Awamu ya Sita. Katika kipindi cha kwanza ameweka msingi, na katika kipindi cha pili anaendelea kuikamilisha. Kupatikana kwa umeme wa uhakika katika eneo hili kutakuwa faida kubwa kwetu sote,” ameongeza.







